KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 1, 2012

Gabon yaipa kibano Tunisia


FRANCEVILLE, Gabon
WENYEJI Gabon juzi walitwaa uongozi wa kundi C katika michuano ya soka ya fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Tunisia bao 1-0.
Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang ndiye aliyeiwezesha Gabon kutoka uwanjani na pointi zote tatu baada ya kuifungia bao hilo la pekee dakika ya 63.
Aubameyang alifunga bao hilo baada ya kutengenezewa pasi safi na nahodha wake, Daniel Cousin. Kipa Rami Jeridi wa Tunisia alijikuta akiusindikiza mpira huo wavuni badala ya kuokoa.
Licha ya kipigo hicho, Tunisia imeungana na Gabon kufuzu kucheza robo fainali kutoka kundi hilo. Kwa mujibu wa ratiba, Gabon sasa itakutana na mshindi wa pili wa kundi D wakati Tunisia itacheza na mshindi wa kwanza wa kundi hilo.
Kocha Mkuu wa Gabon, Rohr aliwapongeza wachezaji wake kwa kuendeleza ari ya ushindi licha ya kufuzu mapema hatua ya robo fainali.
Kocha Mkuu wa Tunisia, Trabelsi alisema alilazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji katika mechi hiyo kwa lengo la kuwalinda wachezaji wake wenye kadi za njano.
Wakati huo huo, Morocco juzi ilimaliza mechi za kundi C kwa ushindi baada ya kuichapa Niger bao 1-0 mjini Libreville.
Bao pekee na la ushindi la Morocco lilifungwa na mshambuliaji Younes Belhanda dakika 11 kabla ya pambano hilo kumalizika.

No comments:

Post a Comment