KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

Ini edo, Rita wakacha kikao cha kuwapatanisha


LAGOS, Nigeria
WACHEZA filamu wa kike wenye mvuto nchini Nigeria, Ini Edo na Rita Dominic wamekacha kuhudhuria kikao kilichoitishwa kwa lengo la kuwasuluhisha.
Kikao hicho kilichoitishwa wiki iliyopita, kililenga kumaliza bifu la muda mrefu kati ya wacheza filamu hao, ambao ni miongoni mwa matajiri watano wa Nollywood.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na wacheza filamu hao zimeeleza kuwa, wote wawili walikwepa kuhudhuria kikao hicho kwa visingizio mbalimbali.
Baadhi ya marafiki wa Ini na Rita ndio walioitisha kikao hicho, kilichopangwa kufanyika kwenye hoteli moja mjini Lagos.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, Rita alitoa udhuru akidai kuwa, alikuwa bize katika kutayarisha filamu yake mpya ya The Meeting wakati Ini alidai kuwa, alikwenda kuhudhuria shughuli muhimu.
Kwa muda mrefu sasa, akina dada hao wenye sura na maumbo yenye mvuto, wamekuwa hawaelewani huku kila mmoja akijigamba kuwa ni zaidi ya mwenzake.
Baadhi ya marafiki wa wacheza filamu hao, wamekuwa hawaifurahii hali hiyo na uadui uliopo kati yao na ndio sababu walipanga kuwakutanisha ili kumaliza tofauti zao.
Hata hivyo, marafiki hao wameonekana kukata tamaa baada ya Ini na Rita kushindwa kuhudhuria kikao hicho cha kuwapatisha.
Akinadada hao walianza kuwa na bifu mwaka jana baada ya Rita kuuponda utaratibu wa kuwateua washindi wa tuzo za mwigizaji bora, kupitia mtandao wa twitter.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Ini ndiye anayeshika namba moja kwa utajiri miongoni mwa wacheza filamu wa kike nchini Nigeria. Mwanadada huyo anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Naira milioni 130.
Licha ya kukumbwa na vikwazo vingi, mafanikio aliyoyapata Ini hadi sasa ni makubwa, ikiwa ni pamoja na kutayarisha filamu zake mwenyewe na ni mwigizaji pekee wa kike anayecheza filamu nyingi zaidi kwa mwaka.
Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, picha zake zimekuwa zikitumika kwenye matangazo ya Globacom, Noble Hair na kumwingizia Naira milioni 90. Anamiliki vitega uchumi vingi pamoja na maduka ya nguo na mitindo.
Naye Rita anashika nafasi ya tatu kwa utajiri nchini Nigeria ambapo mapato yake yanakadiriwa kufika Naira milioni 100. Ni mwigizaji wa kike mwenye mvuto zaidi Nollywood, ambaye amekuwa akiingia mikataba ya matangazo na kampuni mbalimbali kama vile Nokia, Globacom na Arik Air.Kwa sasa, anaandaa filamu yake, ambayo inatarajiwa kuanza kuonyeshwa hivi karibuni nchini Nigeria.

No comments:

Post a Comment