KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 2, 2012

Mashabiki 74 wa soka wauawa Misri









CAIRO, Misri
WATU 74 wamefariki dunia na wengine 248 kujeruhiwa baada ya kutokea vurugu wakati wa mechi ya ligi kati ya timu zenye upinzani wa jadi za Al-Masry na Al-Ahly.
Vurugu hizo zilizuka katika mji wa Port Said wakati Al-Masry ilipokuwa ikiongoza kwa mabao 3-1, ushindi ambao umeelezwa kuwa ni wa kihistoria kwa timu hiyo dhidi ya wapinzani wao.
Mara baada ya Al-Masry kupata bao la tatu, mamia ya mashabiki wake walivamia ndani ya uwanja na kuanza kuwashambulia wachezaji wa Al-Ahly, mashabiki wao na maofisa wa usalama.
Mchezaji wa zamani wa klabu ya Tottenham ya England, Hossam Ghaly alinusurika katika vurugu hizo. Ghaly, aliyeichezea Tottenham mechi 34 kati ya mwaka 2006 hadi 2009, ni nahodha wa Al-Ahly na alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 75.
Imeelezwa kuwa, wakati vurugu hizo zilipoanza, Ghaly alikuwa kwenye vyumba vya wachezaji.
Mashabiki wa Al-Masry waliwakimbiza wachezaji wa Al-Ahly na kuwashambuliaji mashabiki wao katika kila kona ya uwanja, wakiwatupia mawe, fataki na chupa za maji.
Ofisa mmoja wa usalama wa uwanja huo alikaririwa akisema kuwa, wachezaji kadhaa wa Al-Ahly walijeruhiwa kutokana na vurugu hizo, lakini hakuna aliyepoteza maisha.
Mshambuliaji Mohamed Abo Treika wa Al-Ahly alizielezea vurugu hizo kuwa ni sawa na vita.
“Hii siyo soka. Hii ni vita na watu wanakufa mbele yetu,”alisema Abo Treika na kulalamikia kukosekana kwa ulinzi madhubuti na gari za kubeba wagonjwa.
Nyota huyo wa Al-Ahly alitoa mwito kwa Shirikisho la Soka la Misri (EFF) kusimamisha michuano ya ligi hiyo mara moja kutokana na hali kuwa mbaya.
“Siku ya leo haiwezi kusahaulika,”alisema mchezaji huyo.
Timu hizo mbili zimekuwa na uhasama wa muda mrefu na kila zinapokutana, hutokea mapigano na matukio ya umwagaji damu baina ya mashabiki wao.
Mara baada ya vurugu hizo kumalizika, pambano lingine la ligi hiyo kati ya Ismailia na Zamalek lililopangwa kuchezwa mjini Cairo lilifutwa ili kuomboleza vifo vilivyotokea Port Said.
Televisheni ya taifa ya Misri ilionyesha sehemu kadhaa za uwanja wa Cairo ukiwa umechomwa moto na mashabiki wenye hasira, ambao walikerwa na uamuzi wa kufutwa kwa pambano hilo.
Mtangazaji wa televisheni hiyo alisikika akisema kuwa, mashabiki wenye hasira wa Zamalek walipinga uamuzi huo na kuamua kuwasha moto katika baadhi ya maeneo ya uwanja huo.
Hali ya usalama nchini Misri imekuwa duni tangu maandamano makubwa ya wananchi yaliyofanyika mwaka jana na kumng’oa madarakani, Rais Hosni Mubarak.
Vurugu za juzi zinatishia kuiingiza nchi hiyo kwenye matatizo mengine mazito.
Chama cha Muslim Brotherhood, ambacho kina wabunge wengi kwenye bunge la nchi hiyo, kimewashutumu watu wanaomuunga mkono Mubarak kwa madai kuwa, ndio waliochochea vurugu hizo wakati wa mechi hiyo.
EFF imeshatangaza kusimamisha michuano ya ligi kwa muda usiojulikana kutokana na vurugu hizo.
Shirikisho hilo jana lilitoa taarifa mbili, moja ikitangaza kusimamishwa kwa ligi hiyo na nyingine ikitangaza muda wa maombolezo wa siku tatu.
Rais wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Sepp Blatter ametoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zake kutokana na vurugu hizo.
“Nimestushwa na kusikitishwa sana baada ya kupata taarifa za tukio hili na vifo vilivyotokea na watu wengine kujeruhiwa,” alisema Blatter.
“Hii ni siku nyeusi katika soka. Tukio kama hili halifikiriki na halipaswi kutokea tena,”aliongeza.

No comments:

Post a Comment