KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 1, 2012

Mbeya City Boys yachangiwa mil. 27/-

Na Solomon Mwansele, Mbeya
WADAU wa michezo mkoani Mbeya wameichangia timu ya soka ya Mbeya City Boys jumla ya sh. milioni 27.2 ili iweze kufanya vizuri katika michuano ya ligi daraja la kwanza.
Mbali na kiasi hicho cha pesa, wadau hao pia wameipatia timu hiyo mipira 18 na seti kadhaa za jezi.
Michango na vifaa hivyo vya michezo vilitolewa na wadau hao katika harambee iliyoongozwa na mkuu wa mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro.
Katika harambee hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Mbeya Paradise iliyopo Soweto mjini hapa, Kandoro aliichangia timu hiyo shilingi milioni moja.
Mbeya City Boys imefuzu kucheza mzunguko wa pili wa michuano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara baada ya kufanya vizuri katika mzunguko wa kwanza.
Akizungumza na wadau hao, Kandoro alisema kiwango cha pesa kilichochangwa na wadau hao kimeonyesha jinsi walivyo na mapenzi na timu hiyo, inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
“Lakini ili tuweze kufikia malengo haya, ni vyema wananchi wa Mbeya wajenge umoja na utulivu mkoani hapa ili shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea kustawi zaidi,”alisema.
Aliongeza kuwa, mtiririko na mafanikio ya timu hiyo katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, yameonyesha kila dalili kwamba itaendela kufanya vizuri katika mzunguko wa pili.
Kandoro alisema uendeshaji wa michezo ni gharama kubwa, na ndiyo sababu ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetengeneza sera ya kuhakikisha michezo yote nchini inaendelezwa.
Mkuu wa mkoa alisema hakuna serikali, inayoweza kuendesha michezo yote, hivyo ni vyema wadau wa michezo watambue kuwa, wanalo jukumu kubwa la kusaidia uendeshaji wa baadhi ya timu.
”Hili litafanikiwa kwa wadau wa michezo kujitokeza kufadhili timu zetu. Michezo inasaidia kuufanya mji uwe na uchangamfu katika uchumi wake,” alisema
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Juma Idd alisema uongozi kwa kushirikiana na wadau, wamejipanga kuhakikisha Mbeya City Boys inafuzu kucheza ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.
Idd alisema wamekuwa wakitiwa moyo na wadau wa michezo wa Mbeya kutokana na kujitoa kwao kikamilifu kuisaidia timu hiyo ili kufanikisha malengo yake.
“Wananchi wa Mbeya wameikubali timu yao ya Mbeya City Boys, na sisi tunatambua wazi bila ushirikiano wa wadau wa michezo, tukabaki peke yetu, hatuwezi kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Idd.

No comments:

Post a Comment