KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

Dewji aizawadia Chipolopolo sh. mil 22


MWANAMICHEZO na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji amekunwa na mafanikio ya timu ya soka ya Taifa ya Zambia `Chipolopolo’ na amethibitisha furaha yake hiyo kwa kumpatia kila mchezaji wa timu hiyo kitita cha dola 500 za Kimarekani (sh. 750,000).
Kutokana na kiwango hicho cha fedha, Dewji amelazimika kutoka zaidi ya dola 13,000 (sh milioni 22.1 ) kwa ajili ya wachezaji 23 na viongozi wa timu hiyo waliopo Gabon, moja ya nchi mbili zilizoandaa michuano hiyo mikubwa barani Afrika. Nyingine ni Guinea ya Ikweta.
Dewji, aliyeiwezesha Simba kucheza fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, alikabidhi kiasi hicho cha fedha kwa Rais wa Shirikisho la Soka Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya katika ghafla fupi iliyofanyika jana Lusaka, Zambia.
Akikabidhi fedha hizo kwa Bwalya, Dewji ambaye yuko nchini humo kwa shughuli za biashara, alisema ameguswa na mafanikio ya Zambia katika michuano hiyo, ambayo yamerejesha heshima ya soka kwa nchi za kusini mwa bara la Afrika.
“Zambia ni majirani zetu, tunapakana nao. Lazima tujivunie mafanikio haya kwa sababu si ya Zambia peke yao, bali ya ukanda huu wote,” alisema Dewji na kuongeza kuwa, Zambia ni ndugu wa kweli na waliwahi kuwa wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambalo Tanzania ni miongoni mwa wanachama wake.
Mbali na kuizawadia Zambia, Dewji alisema atakuwa tayari kufanya hivyo kwa timu yoyote itakayofanya vizuri, ikiwamo timu ya soka ya Tanzania, `Taifa Stars’.
“Kama timu inatoka ukanda huu, sitabagua, nitawatuza kwa heshima wanayoileta. Hata Twiga Stars wamefanya vizuri hivi karibuni nimewazawadia, lakini si busara kutangaza kila kitu, hata kwa vitu vidogo," alisema.
Dewji ameahidi kumwaga fedha zaidi kwa Zambia iwapo wataifumua Ghana katika mchezo wa nusu fainali. Mchezo huo ulitarajiwa kufanyika jana usiku.
“Nitawapa fedha zaidi na pia nitawakumbuka kwa zawadi maalumu wajane wa wachezaji waliokufa katika ajali ya ndege iliyotokea Pwani ya Gabon mwaka 1993,” alisema Dewji, Mkurugenzi wa kampuni ya Simba Trailers inayounda bodi za magari makubwa, yakiwemo ya mizigo na ya abiria.
Zambia iliyopo Gabon chini ya nahodha Christopher Katongo, ilitua katika fainali za mwaka huu kwa kiapo cha kuwafuta machozi Wazambia ambao miaka 19 iliyopita walipoteza kikosi chote cha kwanza kilichokuwa gumzo wakati huo barani Afrika.
Wachezaji waliokufa katika ajali hiyo ni Efford Chabala, John Soko, Whiteson Changwe, Robert Watiyakeni, Eston Mulenga, Derby Makinka, Moses Chikwalakwala, Wisdom Mumba Chansa, Kelvin "Malaza" Mutale, Timothy Mwitwa, Numba Mwila, Richard Mwanza, Samuel, Moses Masuwa, Kenan Simambe, Godfrey Kangwa, Winter Mumba na Patrick "Bomber".

No comments:

Post a Comment