KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 8, 2012

STEVE: Tutamkumbuka JK akiondoka madarakani



MSANII nyota wa vichekesho nchini, Steve Mengere ‘Nyerere’ amesema haijawahi kutokea na haitatokea kwa kiongozi wa nchi kupenda sanaa kama ilivyo kwa Rais Jakaya Kikwete.
Steve alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
Msanii huyo mahiri kwa kuigiza sauti ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alisema, binafsi amepata mafanikio makubwa kiusanii baada ya kuingia madarakani Rais Kikwete.
“Mimi nasema Rais Kikwete akiondoka madarakani, wasanii watamkumbuka sana kwa sababu haijawahi kutokea na haitatokea kiongozi wa nchi anayependa sanaa kama JK,”alisema.
Aliitaja faida nyingine aliyoipata kiusanii tangu JK alipoingia madarakani kuwa ni kupata nafasi ya kukaa naye karibu na pia kula naye chakula.
“Lakini kikubwa zaidi ni Rais Kikwete kujua kwamba kuna mtu anaitwa Steve Nyerere,”alisema msanii huyo mwenye vituko na makeke.
Steve alisema kwa sasa maisha yanamwendea vizuri kwa sababu pesa ndogo ndogo hazimpigi chenga. Alisema filamu yake mpya ya Mr. President, iliyozinduliwa hivi karibuni imemweka kwenye chati ya juu zaidi.
Msanii huyo alikiri kuwa, sanaa ya vichekesho pia imemwezesha kutembelea mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kufikisha ujumbe kwa njia ya vichekesho.
Steve alisema moja ya malengo makubwa aliyonayo katika siku zijazo ni kuwa mwanasiasa. Alisema anavutiwa sana na mambo ya siasa na anapenda siku moja awe mbunge ama kiongozi wa chama.
Hata hivyo, Steve alikiri kuwa ni vigumu kwa wasanii nchini kupata mafanikio makubwa kiusanii kutokana na kutokuwa na umoja. Alisema sababu kubwa inayowafanya wasanii wasiwe na msimamo ni njaa.
“Wasanii hatuna viwango maalumu vya malipo kwa kazi tunazozifanya. Wewe ukikataa malipo ya shilingi 500,000 kwa kuona ni kiwango kidogo, mwenzako atapokea. Na ukitaka ulipwe shilingi milioni moja, utakufa na njaa,”alisema.

No comments:

Post a Comment