KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 16, 2012

KANUMBA: Nitafunga ndoa wakati utakapowadia


MSANII nguli wa uigizaji filamu nchini, Steven Kanumba amesema atafunga ndoa pale wakati utakapofika kwa vile suala hilo si la kukurupuka.
Akihojiwa katika kipindi cha One Actions cha kituo cha televisheni cha Clouds, akiwa mbele ya mama yake mzazi, Kanumba alisema suala la kufunga ndoa linahitaji umakini mkubwa.
“Siku zote mke mwema anatoka kwa Mungu. Yeye ndiye anayejua mke yupi atakayenifaa,”alisema msanii huyo, ambaye anamiliki kampuni ya Kanumba The Great Films.
“Mungu huwa hachelewi wala hawahi kumpatia mja wake mke bora. Hutoa kila kitu kwa wakati mwafaka,”aliongeza msanii huyo, ambaye anaongoza kwa kucheza filamu nyingi za kibongo.
Hata hivyo, Kanumba hakuwa tayari kusema ni lini anatarajia kufunga ndoa, lakini alisisitiza kuwa, atafanya hivyo baada ya kupata kibali kutoka kwa Mungu.
“Siwezi kusema ni lini nitafunga ndoa. Napenda kuoa, nataka kuoa, lazima mke atapatikana, lakini ni hadi pale atakapopatikana. Mungu akitoa kibali, nitaoa, ‘ alisema.
Wakati wa mahojiano hayo, mama wa msanii huyo alisema anapenda kumuona mwanaye akioa na kupata watoto yeye (mama) akiwa angali hai.
‘Unajua mama, mke anatoka kwa Mungu. Ana mipango yake. Bado hajafanya miujiza hiyo kwangu. Ipo siku nitaoa, nitapata watoto, lakini bado muda haujafika, ‘ alimweleza mama yake.
Hii ni mara ya kwanza kwa Kanumba kuzungumza hadharani masuala yanayohusu kufunga ndoa. Wadau wengi wa sanaa nchini wamekuwa wakimuuliza msanii huyo ni kwa nini hajafunga ndoa hadi sasa.
Amekuwa akiulizwa swali hilo kutokana na ukweli kwamba, msanii huyo ana kila kitu kinachoweza kumfanya aishi maisha mazuri hapa duniani, ikiwa ni pamoja na kuwa na nyumba nzuri na ya kifahari pamoja na magari ya bei mbaya.
Mbali na kumiliki nyumba na magari, imeelezwa pia kuwa, Kanumba ndiye msanii anayeongoza kwa utajiri miongoni mwa wacheza filamu wa kibongo, ikiwa ni pamoja na kumiliki kampuni yake ya kutengeneza filamu.
Akizungumza katika kipindi hicho, mama wa msanii huyo alisema kijana huyo alizaliwa mwaka 1986 na wakati wa kuzaliwa, alitanguliza miguu kwa vile alikaa vibaya tumboni.
Alisema jina la Kanumba ni la babu yake na maana yake ni mtu aliyeshindikana kurogwa. Alisema alipewa jina hilo kwa sababu wakati wa uhai wake, aliwahi kuugua na kuhisiwa angekufa kwa vile alirogwa, lakini akapona kwa miujiza ya Mungu.
Wakati huo huo, Kanumba amesema hakuna kitu rahisi popote pale duniani na kwamba ili mtu aweze kufanikiwa kimaisha, lazima akumbane na vikwazo vingi na vya kila aina.
Kanumba amesema hilo pia lipo katika tasnia ya filamu nchini kwa vile hakuna msanii anayeweza kupata mafanikio kirahisi bila kukumbana na vikwazo.
Msanii huyo alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa chuo maalumu kwa ajili ya mafunzo ya filamu nchini, (Tanzania Film Training Center) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.
“Nakumbuka baada ya kujiunga na kundi la sanaa la Kaole,nilikaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuonekana katika televisheni na nilikuwa natamani kweli, hasa pale nilipokuwa nikiwaona akina Mashaka wakiigiza, ‘alisema.
‘Lakini nafasi hiyo ilikuwa adimu kwangu, hivyo nilivumilia na wasanii nao wanapaswa kuwa wavumilivu, ndio maana wapo chuoni hapa,”alisema Kanumba.
Alimpongeza mkurugenzi wa chuo hicho, Emanuel Mlyamba ‘Pastor Mlyamba’ kwa kubuni wazo zuri la kufungua chuo hicho, akiamini kuwa kinaweza kuleta mageuzi makubwa katika fani hiyo.
Kanumba alisema amefarijika kuona kuwa, mtu aliyemkaribisha kwenye fani hiyo, ameweza kuanzisha chuo hicho kabla ya yeye kuwa na wazo hilo.
Gharama ya masomo katika chuo hicho ni sh. 480,000 kwa kozi ya miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment