TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20, The
Tanzanites mwishoni mwa wiki iliyopita ilijiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza
fainali za Kombe la Dunia baada ya kuichapa Msumbiji mabao 10-0.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, The Tanzanites,
inayofundishwa na Kocha Rogasiun Kaijage, ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao
5-0.
Kutokana na ushindi huo, The Tanzanites sasa inahitaji sare ya aina yoyote wakati timu hizo
zitakaporudiana wiki mbili zijazo mjini Maputo. Msumbiji itaweza kusonga mbele iwapo tu
itashinda mechi hiyo mabao 11-0, kitu ambacho hakuna anayeamini kwamba kinaweza
kutokea.
Licha ya kuibuka na ushindi huo mkubwa wa mabao, vijana wa Tanzanites walionyesha soka
ya kiwango cha juu na kuwafanya wapinzani wao wachanganyikiwe mapema. Bila shaka
walicheza kwa kufuata maelekezo ya kocha wao.
Safu ya ulinzi ya timu hiyo ilicheza kwa utulivu mkubwa, huku mabeki wa kati,Fatuma Issa na
Anastazia Anthony wakitumia akili zaidi katika kuokoa mashambulizi na kumfanya kipa wao,
Celina Julius asipate misukosuko mingi.
Safu ya kiungo, iliyokuwa ikiundwa na Deonisia Daniel na Amina Ali na ile ya ushambuliaji
iliyokuwa ikiundwa na Vumilia Maarifa, Neema Paul, Shelder Boniface na Theresa Yona nazo
zilicheza kwa uelewano mkubwa, hasa kipindi cha pili.
Vijana wa The Tanzanites walionekana kukosa uelewano katika dakika za mwanzo za
mchezo huo, lakini hilo lilitokana na ugeni wao katika mashindano makubwa kama hayo na pia
kutozoea kucheza mbele ya idadi kubwa ya mashabiki.
Walianza kubadilika baada ya Neema Paul kufunga bao la kuongoza dakika ya sita na
mfungaji bora wa michuano ya kimataifa ya Airtel Rising Stars, Shelder Boniface kuongeza
la pili dakika ya 24.
Kuanzia wakati huo, The Tanzanites ilianza kutawala mchezo huku viungo wake, Deonisia na
Amina wakitawala dimba la kati na kuwafanya mashabiki waliofika uwanjani kushuhudia
mechi hiyo kuweweseka kwa furaha muda wote.
Deonisia na Amina waliongeza mabao mengine mawili dakika ya 32 na 41. Bao la Deonisia
lilikuwa tamu zaidi kwani alifunga kwa mpira wa adhabu uliotinga moja kwa moja wavuni.
Cheche za The Tanzanites zilidhihirika zaidi kipindi cha pili wakati Neema Paul, Shelder,
Amina na Stumai kufunga mabao mengine matano na kuweza rekodi ya kuwa timu ya kwanza
ya wanawake kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao.
Kiwango kilichoonyeshwa na mabinti hao kimedhihirisha wazi kuwa, Kaijage ni kocha
aliyepaswa kupewa timu hiyo mapema zaidi kutokana na ukweli kwamba, anatumia mbinu
tofauti na zilizokuwa zikitumiwa na makocha wa zamani wa Twiga Stars, Charles Boniface
na Mohammed Rishard Adolph.
Kuna wakati Boniface na Adolph walipokwenda kuhudhuria mafunzo ya ukocha nje ya nchi,
Kaijage alikabidhiwa kwa muda jukumu la kuinoa Twiga Stars na akaiwezesha kuibuka na
ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Eritrea.
Katika mechi hiyo, wachezaji wa Twiga Stars walionyesha soka ya kufundishwa. Kila
aliyeshuhudia mechi hiyo, alirejea nyumbani moyo wake ukiwa umeridhika si tu kutokana na
ushindi huo mkubwa, bali pia kiwango kilichoonyeshwa na timu hiyo.
Hilo lilijirudia tena katika mechi kati ya The Tanzanites na Msumbiji. Kila aliyekuwepo
uwanjani, alionekana kufurahia aina ya mchezo ulioonyeshwa na mabinti wa Kitanzania na
uwezo walioonyesha wa kufunga mabao.
Kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na The Tanzanites katika mechi dhidi ya Msumbiji, ni
wazi kwamba mabinti hao wameanza kuwiva, wanafundishika na wana uwezo mkubwa wa
kuichezea Twiga Stars katika siku zijazo.
Jambo la msingi ni kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na wadau wa soka,
kuiunga mkono timu hiyo kwa nguvu zote ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Kilichojidhihirisha ni kwamba, Twiga Stars na The Tanzanites zinahitaji changamoto mpya,
ari mpya na mbinu mpya hivyo mabadiliko ya uendeshaji wake ni muhimu kwa wakati huu.
Pamoja na mwanzo mzuri wa The Tanzanites, inasikitisha kuona kuwa, TFF haikutoa hamasa
ya kutosha kwa mashabiki kufika uwanjani kwa wingi kuishangilia. Vilevile ilishangaza kuona
kuwa, TFF ilipanga viingilio vya juu wakati inafahamu wazi kwamba, timu za wanawake
hazina mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka nchini.
Pengine lingekuwa jambo la muhimu kwa TFF kuweka viingilio vya chini kwenye maeneo yote
ya uwanja ili mashabiki wengi zaidi wahamasike kwenda kuishangilia. Ingekuwa vyema zaidi
iwapo TFF ingeweza kiingilio maalumu kwa wanawake ili kuwavutia waipende timu yao.
Ikumbukwe kuwa, wakati Mkwasa alipotangaza kujiuzulu kuifundisha Twiga Stars,
malalamiko yake makubwa yalikuwa ni timu hiyo kutothaminiwa na TFF na kutopata
maandalizi mazuri kama ilivyo kwa timu ya wanaume, Taifa Stars.
Uamuzi uliochukuliwa na Mkwasa ulikuwa wa kijasiri na ulistahili kupongezwa kwa sababu
ulionyesha wazi jinsi alivyokuwa tayari kuwajibika kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo
bila kujali kiini cha tatizo kipo wapi.
Ukweli ni kwamba, Mkwasa atakumbukwa kwa kuifikisha juu timu hiyo, akiiwezesha kushiriki
fainali za Afrika miaka mitatu iliyopita nchini Afrika Kusini, ikiwa ni mara ya kwanza katika
historia ya timu hiyo.
Safari ya Twiga Stars kisoka ilianza mbali, miaka ya mwishoni mwa miaka ya 1990, wakati
huo ikiwa inaundwa na wachezaji wengi kutoka timu ya Sayari, iliyokuwa na maskani yake
Magomeni, Dar es Salaam.
Twiga Stars ilipitia mikononi kwa makocha wengi. Alikuwepo marehemu Suleiman Gwaje,
akaja marehemu Iddi Machuppa na baadaye ikawa chini ya Mkwasa na Adolph. Kabla ya
Mkwasa kujiuzulu, alikuwa akiinoa timu hiyo kwa kushirikiana na Nasra Juma kutoka
Zanzibar.
Mafanikio ya Twiga Stars kimataifa yalianza kuonekana chini ya Mkwasa, ambaye ndiye
aliyeiongoza katika fainali za Afrika, fainali za All Africa Games na fainali za COSAFA. Kwa
jumla, kocha huyo ndiye aliyeiingiza Twiga Stars kwenye ramani ya kimataifa kisoka.
Hata hivyo, kushindwa kwa Twiga Stars kufanya vizuri katika michuano ya mwaka jana
kuliacha maswali mengi, hasa kutokana na kiwango cha chini ilichoonyesha katika mechi za
kirafiki dhidi ya Zimbabwe, Afrika Kusini na Ethiopia.
Katika mechi hizo tatu, wachezaji wa Twiga Stars walishindwa kucheza kwa uelewano na
ilikuwa haieleweki aina ya mfumo wanaocheza. Pia hawakuwa na stamina ya kutosha. Ilikuwa
kama vile ni timu iliyofanya mazoezi kwa kipindi kifupi.
Ni dhahiri kwamba uwezo wa Mkwasa kuinoa timu hiyo ulikuwa umepungua na alihitajika
mtu mwingine kuchukua nafasi yake. Hii ni kwa sababu alikaa na wachezaji wa timu hiyo kwa
miaka mingi hivyo inawezekana walimzoea kupita kiasi na pengine heshima yao kwake ilianza
kupungua.
Ieleweke kuwa, kocha anapozoeana na kuwa karibu na wachezaji kwa miaka mingi, ni rahisi
heshima na nidhamu kuanza kushuka kwa vile watamuona na kumchukuluia kama mwenzao.
Bravo TFF kwa kumteua Kaijage kuwa mrithi wa Mkwasa na ni jukumu la viongozi wapya wa
TFF kuipatia timu hiyo huduma zote muhimu na ikiwezekana kuitafutia wadhamini ili iweze
kufika mbali zaidi.