KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 1, 2012

Wapiganaji 10 kuiongoza Yanga Misri


VIONGOZI 10 ‘wapiganaji’ wa klabu ya Yanga wanatarajiwa kuiongoza timu hiyo kwenda Misri kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, msafara wa Yanga utakuwa na wachezaji na viongozi wasiopungua 40 na utaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri.
Sendeu alisema kamati ya utendaji ya Yanga imeamua viongozi 10 waandamane na timu hiyo kwenda Misri kwa ajili ya kuwatoa hofu wachezaji na pia kukabiliana na vitendo vyovyote vya hujuma.
Alisema msafara wa timu hiyo utaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Haki za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa.
Aliwataja viongozi wengine watakaofuatana na timu hiyo kuwa ni Mwenyekiti, Lloyd Nchunga na Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa. Wengine ni wajumbe wa kamati ya utendaji Ally Mayay, Mussa Katabalo, Tito Solo, Theonest Rutashobora, Seif Ahmed, Kibwana Matokeo na Abdalla Bin Kleb.
Hata hivyo, Sendeu hakuwa tayari kutaja kikosi cha wachezaji kinachotarajiwa kwenda Misri, lakini alisema wachezaji sita wataachwa kutokana na sababu mbalimbali.
Aliwataja wachezaji watakaoachwa kuwa ni Yaw Berko, Salum Telela, Mohamed Mbegu, Godfrey Bonny.
Wachezaji wanaotarajiwa kuwemo kwenye msafara huo ni makipa Shaaban Kado na Saidi Mwalami. Mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Godfrey Taita, Nadir Haroub, Athumani Iddi, Chacha Marwa.
Viungo na washambuliaji ni Seif Kijiko, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Hamizi Kiiza, Davis Mwape, Kenneth Asamoah, Shamte Ally, Kigi Makasi, Jerry Tegete na Pius Kisambale.
Yanga na Zamalek zinatarajiwa kurudiana keshokutwa katika mechi itakayopigwa kwenye uwanja wa jeshi mjini Cairo. Mechi hiyo haitakuwa na watazamaji na kila timu imeruhusiwa kuingia na watu wasiozidi 40.
Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Ili ifuzu kusonga mbele, Yanga italazimika kuishinda Zamalek ama kutoka nayo sare ya idadi kubwa ya mabao, ambayo yataiwezesha kunufaika na mabao mengi ya ugenini.

No comments:

Post a Comment