KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 1, 2012

Odama sasa kutengeneza filamu zake mwenyewe


BAADA ya kung’ara kwa muda mrefu katika fani ya uigizaji filamu, mwanadada Jenifer Kyaka ‘Odama’ sasa ameamua kuwa mtayarishaji wa fani hiyo.
Odama alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ameanzisha kampuni yake ya J. Production kwa ajili ya kazi hiyo.
Mwanadada huyo alisema amefikia uamuzi wa kuanzisha kampuni hiyo kwa lengo la kutimiza ndoto yake ya kuwa mjasiliamali.
Odama alisema kampuni hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya kurekodi filamu atakazokuwa akizitayarisha yeye mwenyewe.
Hata hivyo, Odama alisema kampuni hiyo pia itakuwa ikitoa huduma ya kupiga picha za filamu kwa ajili ya watayarishaji wengine.
“Kwa sasa hali ya ushindani ni kubwa sana kwa hiyo kama hauna kampuni kwa ajili ya utayarishaji wa filamu zako, utasumbuka na hata kuharibu kazi yako, “alisema.
“Unapotumia kampuni ya nje, unakutana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa kazi zako, lakini pia unakosa usimamizi wa kazi hiyo,” aliongeza mwanadada huyo mwenye umbo na sura jamali.
“Unaweza kupoteza muda mwingi kwani unapompatia kazi mtendaji hata kama ana kazi nyingi hasemi, hali ambayo inaweza kuharibu ratiba yako kwa kucheleweshewa kazi na hata kuharibiwa,”alisema Odama.
Mwanadada huyo aliwalalamikia wahariri wa filamu, ambao sio waaminifu kwa madai kuwa ndio chanzo kikubwa cha filamu nyingi kuchelewa kuingia sokoni ama kuharibika.
Odama ni mmoja wa wasanii waliopo kwenye tasnia ya filamu kwa miaka mingi, akiwa amecheza filamu zaidi ya 36 kati ya hizo, tisa akiwa ameshiriki kama mtayarishaji.
Baadhi ya filamu zilizompatia umaarufu mkubwa ni pamoja na All about love, Odama, Shumileta na Rude.
Alisema filamu ya Rude ameitengeneza kupitia kampuni yake ya J Production na tayari imeshakamilika. Alisema filamu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni wakati wowote.
“Ni filamu nzuri sana kuanzia uigizaji, hadithi yake na hata wasanii walioigiza wako juu katika tasnia ya filamu. Wapenzi wa filamu zangu wajiandae kupokea kazi ya ukweli,” anasema Odama.
Washiriki wengine waliocheza filamu ya Rude ni Stanley Msungu ‘Chotara la Kihehe, Ruth Suka ‘Mainda’ na wengineo.

No comments:

Post a Comment