KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 27, 2012

Mechi ya Yanga na Zamalek kuchezwa saa 12 jioniMAKOCHA POULSEN (TAIFA STARS), ANGELS (MAMBAS)

Makocha Jan Poulsen wa Tanzania (Taifa Stars) na Gert Josef Angels wa Msumbiji (Mambas) kesho (Februari 28 mwaka huu) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya timu zao.

Taifa Stars na Mambas zitapambana Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni katika mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Mkutano huo na waandishi wa habari ambapo makocha hao pia watajibu maswali ya waandishi wa habari utafanyika saa 6 kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mambas iliwasili nchini jana (Februari 26 mwaka huu) ikiwa na wachezaji 19 na viongozi kumi. Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Francisco Muchanga, Clesio Bauque, Almiro Lobo, Manuel Fernandes na Francisco Massinga. Wengine ni Joao Rafael, Nelson Longomate, Joao Mazive, Zainadine Chavango, Osvaldo Sunde, Luis Vaz, Carlos Chimomole, Joao Aguiar, Edson Sitoe, Jeremias Sitoe, Stelio Ernesto, Elias Pelembe, Eduardo Jumisse na Simao Mate.

MECHI YA YANGA, ZAMALEK KUCHEZWA SAA 12

Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek na Yanga itachezwa Machi 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jeshi jijini Cairo kuanzia saa 12 jioni kwa saa za Misri.

Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mechi hiyo itachezwa bila washabiki kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.

WASOMALI KUCHEZESHA SIMBA, KIYOVU

Mwamuzi i Yabarow Hagi Wiish na wasaidizi wake Aweis Ahmed Nur na Abdirahman Omar Abdi, wote kutoka Somalia ndiyo watakaochezesha mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Kiyovu Sport ya Rwanda.

Kwa mujibu wa orodha ya waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), mwamuzi wa akiba kati mechi hiyo namba 14 itakayochezwa Machi 4 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam atakuwa Waziri Sheha wa Tanzania. Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya awali atakuwa Jean Marie V. Hicuburundi kutoka Burundi.

CAF imeziingiza moja kwa moja kati raundi ya kwanza timu 16 kutokana na ubora wake. Timu hizo ni ES Setif (Algeria), Interclube (Angola), Asec Mimosas (Ivory Coast), Enppi (Misri), AS Real Bamako (Mali), CO de Bamako (Mali) na CO Meknes (Morocco).

Nyingine ni WAC (Morocco), Warri Wolves (Nigeria), Heartland (Nigeria), St. Eloi Lupopo (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Us Tshinkunku (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Amal Otbara (Sudan), Al Ahly Shandy (Sudan), CSS (Tunisia) na CA (Tunisia).

Sunday, February 26, 2012

Wengi wajitokeza mbio za kujifurahisha za Vodacom

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Alhaji Mussa Samizi (kulia) akikabidhi zawadi ya Simu, fedha Tsh 80,000 na Mordem iliyo na kifurushi cha kuanzia 20,000/= kwa mshindi wa pili wa mbio za Vodacom Fun Run, Brazil Boay katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon 2012 zilizofanyika jana mjini Moshi. Katikati ni Mkuu wa Udhamini wa Vodacom, George Rwehumbiza.Mkuu wa Wilaya ya Moshi Alhaji Mussa Samizi (kulia) akikabidhi zawadi ya Simu, fedha Tsh 80,000 na Mordem iliyo na kifurushi cha kuanzia 20,000/= kwa mshindi wa tatu upande wa wanawake Natalia Elisante, wa mbio za Vodacom Fun Run, Brazil Boay katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon 2012 zilizofanyika jana mjini Moshi. Katikati ni Mkuu wa Udhamini wa Vodacom, George Rwehumbiza.Mkuu wa Wilaya ya Moshi Alhaji Mussa Samizi (kulia) akikabidhi zawadi ya Simu, fedha Tsh 100,000 na Mordem iliyo na kifurushi cha kuanzia 20,000/= kwa mshindi wa kwanza upande wa wanawake Jackline Sakilu, wa mbio za Vodacom Fun Run, Brazil Boay katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon 2012 zilizofanyika jana mjini Moshi. Katikati ni Mkuu wa Udhamini wa Vodacom, George Rwehumbiza.004. Baadhi ya washindi wa Vodacom 5 KM fun run wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Rukia Mtingwa kulia na Afisa Udhamini wa Vodacom Tanzania Ibrahim Kaude kushoto.


Ofisa Masoko Mkuu na Mahusiano akishiriki katika mbio za kujifurahisha za”Vodacom 5 KM fun run”


Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Rukia Mtingwa wa pili toka kushoto akifurahia jambo na baadhi ya watoto wenye ugonjwa wa ukimwi mara walipomaliza kushiriki katika mbio za kujifurahisha za “Vodacom 5 KM fun run”


Na Mwandishi Wetu, Moshi

Mbio za kujifurahisha za kilometa 5 za (Vodacom 5KM fun run) ambazo ni sehemu ya mbio za Kilimanjaro marathoni zimezidi kujizolea umaarufu kwa watu wengi wa rika tofauti kujitokeza kushiriki kwenye mbio hizo zilizofanyika jana/leo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mahusiano wa kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania ambao ndio wadhamini wa mbio hizo, Rukia Mtingwa katika mbio za mwaka huu jumla ya watu 10,000 wamejitokeza kushiriki kwenye mbio hizo tofauti na makadirio ya kawaida ya kupata jumla ya washiriki 5000 ambacho ndicho huwa kiwango cha juu .

Mtingwa alisema wengi wa washiriki katika mbio hizo kwa mwaka huu zimetokana na uhamasishaji mkubwa uliofanywa na vyombo vya habari na mvuto wa mbio hizo ambazo huambatana na manjonjo mbalimbali Kutoka kwa washiriki wake na zawadi za kuvutia zinatolewa na Vodacom.

Pamoja na mafanikio hayo Mtingwa alisema wao kama wadhamini wamepata changamoto kubwa katika mbio hizo hasa kwa mwaka huu kutokana na wakimbiaji wazoefu kujitosa kushiriki kwenye mbio hizo badala ya kuwaachia watu wengine ambao riadha sio fani yao .

“Kwa kweli mwaka huu tumekumbana na changamoto hiyo ya wakimbiaji profession kushiriki kwenye fun run ambazo sisi tunaona ni maalum kwa watu ambao riadhi si fani yao kwahiyo kipindi kijacho endapo tutaendelea na udhamini wa mbio hizi itabidi tuifanyie kazi changamoto hii,”alisema Mtingwa .

Aidha Mtingwa alisema changamoto ya kujitokeza washiriki wengi kwao ni faraja kubwa na watajipanga kukubaliana na haki hiyo ili kuendana na mazingira ya ukubwa wa mbio hizo kadiri watu watakavyokuwa wakijitokeza.

Washindi wa mbio za jana/leo kwa upande wa wanaume ni Gailet Ismail ambaye alichukua na nafasi ya kwanza na kujinyakulia simu ya mkononi aina ya ZTE S- 501,muda wa maongezi wa Sh 20,000, modem ya intaneti pamoja na M-Pesa ya Sh 100,000.

Brazil Boay alichukua nafasi ya pili na kuzawadiwa simu ,muda wa maongezi,modem ya intanert na M-Pesa ya Sh 80,000 wakati mshindi wa tatu alikuwa Fabiano Nelson ambaye naye alipata simu,muda wa maongezi,modem na M-Pesa ya Sh 60,000.

Na upande wa wanawake washindi walikuwa ni Jackline Sakilu,Catherine Iranga na Natalia Elisante ambao nao walijishindia zawadi sawa na zile walizopata wanaume , washindi wengi kuanzia nafasi wanne hadi 10 pamoja na wshiriki walioweza kumaliza mbio hizo nao walipata zawadi mbalimbali kutoka Vodacom.

Huo ni mwaka wa tano tokea Vodacom iwe mdhamini wa mbio za kilometa tano za kujifurahisha (Vodacom fun run) ambazo ni sehemu ya mbio maarufu za Kilimanjaro ambazo mwaka huu zimeadhimisha miaka 10 tokea kuanzishwa kwake .

SIMBA YAINGIA MKATABA NA PRIMETIME PROMOTION

Makamu Mwenyekiti Simba SC , Geofrey Nyange (Kaburu) wa tatu kulia akizungumza mbele ya Wanahabari (hawapo pichani),kuhusiana na KLABU ya soka ya Simba kuingia mkataba na kampuni ya Prime Time Promotions Ltd unaohusiana na Promosheni na Masoko (Promotion and Marketing) kwa ajili ya mechi ya Kombe la Shirikisho (CAF) kati ya Simba na Kiyovu Sport ya Rwanda. Kulia ni Mmoja wa Wakurugenzi wa Prime Time Promotions,Bw.Godfrey Mkama,Joseph Kusaga na shoto ni Katibu Mkuu wa Simba Bw.Evodius Mtawali

Makamu Mwenyekiti Simba SC , Geofrey Nyange (Kaburu) akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group,Bw.Joseph Kusaga mara baada ya makubaliano yao ya kufanya kazi pamoja mbele ya wanahabari (hawapo pichani),yaliyofanyika leo kwenye hotel ya Belimonte jijini Dar.


KLABU ya soka ya Simba ina furaha kubwa kuutangazia umma wa Watanzania kwamba imeingia mkataba na kampuni ya Prime Time Promotions/Clouds Media Group unaohusiana na Promosheni na Masoko (Promotion and Marketing) kwa ajili ya mechi ya Kombe la Shirikisho (CAF) kati ya Simba na Kiyovu Sport ya Rwanda.

Ushirikiano huo wa namna ya kipekee una lengo la kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanafahamu juu ya pambano hilo na wanahudhuria pambano hilo la kimataifa lakini pia kuweka mazingira ya kuvutia kwa makampuni na wafanyabiashara ili wawekeze katika mchezo huu kipenzi cha Watanzania.

Ingawa mkataba huu wa sasa baina ya Simba na Clouds unahusu mechi hii moja pekee, kuna kila dalili kuwa huu utakuwa mwanzo wa kampuni hizi mbili kufanya kazi kwa pamoja kwa muda mrefu kwa lengo la kuhakikisha mchezo wa soka unakua kwa faida ya taifa letu.

Kwa kuanzia tu, pamoja na mechi hii ya Kiyovu, Simba SC leo pia inatangaza kuanzisha kwa luninga ya klabu, Simba TV, ambayo lengo lake kubwa litakuwa ni kuonyesha shughuli za kila siku na matukio mbalimbali yanayohusiana na klabu yetu.

Clouds Media Group kupitia Clouds TV ndiyo watakaokuwa wakionyesha vipindi hivyo vya Simba mara moja kwa wiki mwanzoni lakini lengo ni kuwa na televisheni ambayo itakuwa inaonyesha habari za Simba saa 24 kila siku.

Ndiyo maana basi, sisi katika Simba, tunaamini kuwa ushirikiano huu baina ya Simba na Clouds unafungua njia ya maendeleo anuai katika kila nyanja inayohusiana na mchezo wa soka hapa nchini.

Simba SC inapenda kutumia fursa hii kukaribisha makampuni na wafanyabiashara kujitokeza kudhamini mchezo wa soka hapa nchini kwa vile uzoefu unaonyesha kuwa kuwekeza katika soka kunalipa.

Wenu Katika Mapinduzi ya Soka Tanzania

Geofrey Nyange

Makamu Mwenyekiti

Simba SC.

MSAFARA WA YANGA MISRI USIZIDI WATU 40Msafara wa Yanga utakaokuwa uwanjani kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek itakayochezwa wikiendi ijayo nchini Misri unatakiwa kuwa na watu wasiozidi 40.

Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yaliyotumwa jana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ni idadi hiyo tu inayotakiwa kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.

Adhabu ya Zamalek kutocheza mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila washabiki ilitolewa Aprili 20 mwaka jana na Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Mechi dhidi ya Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu hiyo iliyotakana na washabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka jana ilipocheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Hivyo kila timu (Yanga na Zamalek) katika mechi hiyo inatakiwa kuwa na wachezaji ambao wana leseni za CAF kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa 2012. Pia benchi la ufundi katika kila timu linatakiwa kuwa na watu watano.

Kwa klabu zote mbili, kila moja imeruhusiwa kuingia na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji wasiozidi kumi. Mbali ya klabu hizo mbili, wengine waliotajwa kuruhusiwa kuingia uwanjani ni vijana 20 watakaofanya kazi ya kuokota mipira (ball-boys). Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.

MSUMBIJI KUTUA NCHINI FEBRUARI 26

Timu ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) itawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa ndege ya South African Airways. Ndege hiyo yenye mruko namba SA 186 inatarajia kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7.55 mchana.

Msafara wa Mambas kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano (Februari 29 mwaka huu) saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa na watu 29. Kati ya hao, 19 ni wachezaji wakati waliobaki ni maofisa wa timu hiyo.

Mwamuzi wa mechi hiyo Farouk Mohamed na wasaidizi wake Ayman Degaish, B.T Abo El Sadat na Gihed Greisha kutoka Misri watawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa ndege ya Egypt Air. Kamishna ni Loed Mc Ian kutoka Afrika Kusini.

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa Jumanne (Februari 28 mwaka huu) katika vituo vya vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.

Thursday, February 23, 2012

Stars, DRC hakuna mbabe

Moja ya hekaheka zilizotokea kwenye lango la DRC wakati timu hiyo ilipomenyana na Taifa Stars jana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka suluhu.

Uhuru Selemani (kulia) wa Taifa Stars akiwania mpira na Mampuya Kimwaki wa DRC timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka suluhu.

Kocha wa Mafunzo ya Zbar ajipa matumaini


KOCHA Mkuu wa Mafunzo, Hemed Suleiman Moroko amesema kipigo walichokipata kutoka kwa Mucumane de Maputo ya Msumbiji hakijafuta matumaini yao ya kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika.
Moroko amesema katika mechi hiyo iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, wachezaji wake walicheza vizuri lakini hawakuwa na bahati ya kufunga mabao.
Katika mechi hiyo iliyochezwa usiku na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, Mafunzo ilipigwa mweleka wa mabao 2-0.
Ili isonge mbele katika michuano hiyo, Mafunzo italazimika kuishinda Macumane mabao 3-0 katika mechi ya marudiano, inayotarajiwa kuchezwa wiki mbili zijazo mjini Maputo.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Moroko alisema ameshazisoma mbinu za wapinzani wao na kuongeza kuwa, atatumia uzoefu wake wote kuwapa mbinu wachezaji wake ili washinde mechi ya marudiano.
“Mimi siwezi kusema kwamba tumefungwa na hapa ndio mwisho wetu. Naamini tunaweza kufika mbali safari hii kwa sababu vijana wangu wamecheza vizuri,”alisema kocha huyo. Aliwataka mashabiki wa soka wa Zanzibar wasiwe na wasiwasi kuhusu hatma ya timu yao na kuongeza kuwa, wamepania kuushangaza umma wa Wazanzibar kwa kushinda ugenini.
Katika mechi hiyo, Mafunzo ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya nane wakati Jaku Juma alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Capo Venancio wa Mucumane.
Dakika nne baadaye, Mucumane ilipata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wake, Maciricio, aliyeruka hewani na kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Luis Pereira.
Bao hilo liliongeza msisimko wa mechi hiyo huku Mucumane wakishangiliwa na kikundi kidogo cha ngoma ya Sindimba kutoka Dunga, wilaya ya kati.
Mucumana iliongeza bao la pili dakika ya 21 kupitia kwa Manuel Mbalango baada ya kipa Suleiman Janabi kukosea hesabu wakati alipotoka langoni kwa lengo la kuokoa mpira.
Licha ya mabadiliko kadhaa ya wachezaji yaliyofanywa na Kocha Moroko katika vipindi vyote viwili, hayakuweza kuisaidia timu hiyo kupata bao.
Vijana wangu walikosa umakini-Kocha
KOCHA Mkuu wa Jamhuri, Renatus Shija amesema kufungwa kwa timu yake na Hwange ya Zimbabwe, kulitokana na wachezaji wake kukosa umakini na kuwa na woga.
Shija alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya Jamhuri kuchapwa mabao 3-0 na Hwange katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Gombani.
Kocha huyo alisema Hwange si timu ya kutisha, lakini walifanikiwa kutoka uwanjani kutokana na vijana wake kuanza mechi hiyo kwa woga.
“Vijana wangu walianza kutulia baada ya dakika 15 za kwanza kumalizika na walicheza vizuri zaidi katika kipindi cha pili,”alisema kocha huyo.
Shija alisema katika kipindi hicho, timu yake ilipata nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini walishindwa kuzitumia vyema kutokana na washambuliaji wake kuwa na papara na kupiga mashuti hafifu.
Kocha huyo alikiri kuwa, kipigo hicho kimewaweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele kwa vile watalazimika kushinda mechi ya marudiano wiki mbili zijazo kwa mabao 4-0.
Hata hivyo, alijipa moyo kwa kusema kuwa, katika soka lolote linaweza kutokea na kwamba, iwapo watapata mechi mbili ngumu za kujipima nguvu, wanaweza kufanya vizuri.
Alisema wasiwasi pekee alionao ni kuhusu hali ya hewa ya mji wa Hwange, ambao upo kilometa 770 kutoka Harare, ambao joto lake hupanda hadi kufikia nyuzi 40 hadi 45.
Shija alisema ameuomba uongozi wa Jamhuri kuitafutia mechi mbili za kujipima nguvu nje ya Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya marudiano. Alisema angependa zaidi mechi hiyo ichezwe Sudan kwa vile hali ya hewa ya huko inafanana na ya Zimbabwe.
Mwamuzi adaiwa kumdunda mchezaji
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mwamuzi aliyekuwa akichezesha mechi ya mpira wa miguu katika michuano ya ligi daraja la pili wilaya ya kusini, anadaiwa kumpiga ngumi mchezaji, sambamba na kumuonyesha kadi nyekundu. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati timu za New Boys na Ranger Bulls za Mtende zilipokuwa zikimenyana katika uwanja wa Mwehe Makunduchi. Mwamuzi huyo, Baiye Maulid anadaiwa kumpiga ngumi mchezaji Khalid IddI Vuia wa New Boys muda mfupi baada ya kumuonyesha kadi nyekundu. Kufuatia kitendo hicho, uongozi wa New Boys umekiandikia barua Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wilaya ya kusini kumlalamikia mwamuzi huyo. Katibu wa New Boys, Mohamed Machanja alisema juzi kuwa, wameamua kukilalamikia chama hicho ili haki itendeke na kwamba wana matumaini ZFA haitapendelea upande wowote. Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, mwamuzi Baiye alikanusha kumpiga mchezaji huyo, akidai kuwa alichofanya ni kumsukuma kwa lengo la kujihami baada ya kumkamata sehemu nyeti za mwili wake. ''Si kweli kwamba nilimpiga. Nilichokifanya ni kujihami baada ya kunisogelea wakati nilipomuonyesha kadi nyekundu na alipofika karibu nami, akanikamata nyeti zangu,” alisema. Baiye alisema hawezi kusema mengi kuhusu tukio hilo kwa sababu ameshawasilisha ripoti yake katika ofisi za ZFA wilaya ya kusini na anachosubiri ni maamuzi yake.
Kwa upande wake, Khalid alikanusha kutaka kumdhuru mwamuzi huyo. Alisema alichokifanya ni kumsogelea kwa lengo la kumfahamisha jambo fulani.
ZFA yakiri waamuzi wanapokea rushwa
CHAMA cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wilaya ya Kusini Unguja kimekiri kuwa, baadhi ya waamuzi wa mchezo huo wamekuwa wakijihusisha na upokeaji rushwa ili wachezeshe kwa upendeleo.
ZFA imesema vitendo hivyo hufanyika katika mechi mbalimbali za michuano ya ligi daraja la pili na la tatu katika wilaya hiyo.
Mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amesema, timu nyingi za wilaya hiyo zimeanza kuwasilisha malalamiko kuhusu vitendo hivyo.
Kiongozi huyo aliyezungumza na Burudani mwishoni mwa wiki iliyopita alisema, baadhi ya waamuzi wamekuwa wakipindisha sheria kwa makusudi baada ya kupokea rushwa.
“Ni vitendo vya kusikitisha sana kwa sababu baadhi ya waamuzi wamekuwa wakipindisha sheria baada ya kupewa rushwa na hivyo kuzipendelea baadhi ya timu,”alisema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, waamuzi wengine wamekuwa wakipindisha sheria baada ya kupewa magunia ya mkaa na samaki badala ya pesa taslimu.
Alisema chama chake kimekuwa kikitupiwa lawama nyingi kutokana na uchezeshaji mbovu wa waamuzi wakati hakihusiki kupanga matokeo ama kutoa maelekezo yoyote kwa waamuzi.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kwa sasa chake chake hakiwezi kuchukua hatua yoyote kwa waamuzi wanaolalamikiwa kwa vile hakina ushahidi wa kujihusisha kwao na vitendo hivyo.
“Suala hili linahitaji uchunguzi wa kina, ukilihusisha jeshi la polisi ili upatikane ushahidi wa kutosha. Hatuwezi kumuhukumu mwamuzi bila ya kuwa na ushahidi,”alisema.

Habari zote na Abood Mahmoud, Zanzibar

Papic ataka mazoezi usiku


KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuiandalia timu mazoezi ya usiku kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Zamalek ya Misri.
Papic anataka Yanga ifanye mazoezi usiku kwa vile mechi yao ya marudiano dhidi ya Zamalek itachezwa katika muda huo.
Kiongozi mmoja wa Yanga alisema jana kuwa, watalifanyia kazi ombi hilo la Papic kwa vile ni la muhimu ili wachezaji waweze kuizoea hali hiyo.
“Ni kweli Papic amewasilisha ombi hilo kwa uongozi na tumeshaanza kulifanyia kazi. Kwa vile mechi yetu ya marudiano itachezwa usiku, ni vizuri wachezaji waizoee hali hiyo mapema,”alisema.
Yanga na Zamalek zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Cairo na upo uwezekano mechi hiyo ikachezwa bila watazamaji ama ikahamishiwa katika nchi nyingine.
Katika mechi ya awali iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kutokana na sare hiyo, kila timu inayo nafasi ya kusonga mbele iwapo itashinda mechi ya marudiano. Hata hivyo, Zamalek itakuwa na faida kubwa ya kucheza ugenini.

TFF yafuta uchaguzi wa DRFA


KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza kufuuta uchaguzi mkuu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ulioapangwa kufanyika Machi 18 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratias Lyatto kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa, uchaguzi huo umefutwa kutokana na katiba ya DRFA kutokidhi matakwa ya katiba ya TFF.
Kwa mujibu wa Lyatto, mchakato wa uchaguzi wa DRFA sasa utaanza upya mara baada ya kukamilika kwa marekebisho ya vifungu vya katiba ya chama hicho vinavyokinzana na matakwa ya katiba ya TFF kabla ya Agosti 10 mwaka huu.
Kufuatia uamuzi huo, kamati hiyo imesema uongozi wa sasa wa DRFA utaendelea kukaa madarakani hadi uchaguzi huo utakapofanyika kabla ya Agosti mwaka huu.
Lyattu alisema kamati yake imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia ushauri wa kamati ya sheria, katiba na hadhi kwa wachezaji kuhusu katiba ya DRFA.
“Kamati iliridhika na kukubaliana na ushauri wa kamati ya sheria, katiba na hadhi kwa wachezaji kwamba, katiba ya DRFA haikidhi matakwa ya katiba ya TFF,”alisema.

Stars, DRC kazi ipo leoKIKOSI cha timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, leo kinashuka dimbani kumenyana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa kujipima nguvu kwa timu zote mbili kabla ya kucheza mechi za michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Katika michuano hiyo, Taifa Stars imepangwa kumenyana na Msumbiji katika mechi itakayopigwa Februari 29 mwaka huu mjini Dar es Salaam wakati Congo itavaana na Shelisheli.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen na Kocha Msaidizi wa DRC, Mutubile Santos kila mmoja alitamba kuwa timu yake itaibuka na ushindi.
Poulsen alisema timu yake imejiandaa vyema kuikabili Congo na kuongeza kuwa, mchezo huo ni muhimu kwa kikosi chake kinachojiandaa kuvaana na Msumbiji.
Kocha huyo kutoka Denmark alisema, anatarajia mchezo huo utakuwa kipimo muhimu kwa timu yake kabla ya kuivaa Msumbiji na kuongeza kuwa, utamsaidia kubaini mapungufu ya timu yake.
Poulsen alisema ujio wa mchezaji Ali Badru anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Canal Suez ya Misri, utachangia kuongeza nguvu kwenye timu yake. Mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili nchini leo asubuhi.
Katika mchezo huo, Taifa Stars itawategemea zaidi wachezaji wake wazoefu kama vile Shadrack Nsajigwa, Juma Nyoso, Abdi Kassim, Mrisho Ngassa na Stephano Mwasika.
Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni Juma Kaseja, Shaaban Kado, Mwadini Ali, Nassor Said, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Jonas Gerald, Shaban Nditi, Shomari Kapombe, Salum Aboubakar, Mwinyi Kazimoto, Juma Javu, John Bocco, Uhuru Selemani na Nsa Job.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Congo, Santos, alisema timu yake imejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na kuongeza kuwa, wanatarajia utakuwa kipimo tosha kabla ya kuivaa Shelisheli.
Santos alisema wanaiheshimu Taifa Stars kuwa ni timu nzuri ndiyo sababu wamekubali kupambana nayo kwa lengo la kupima uwezo wa timu yake.

Simba yaipania KiyovuUONGOZI wa klabu ya Simba umeandaa mikakati kabambe kwa lengo la kuhakikisha wanaipa kipigo kikali Kiyovu ya Rwanda katika mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Mikakati hiyo ilianza kuandaliwa juzi katika kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo kilichofanyika mjini Dar es Salaam chini ya makamu mwenyekiti wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Katika kikao hicho, kamati hiyo ilijadili ripoti ya Kocha Milovan Cirkovic kuhusu mechi ya awali kati ya timu hizo iliyochezwa mjini Kigali, Rwanda.
Katika mechi hiyo, Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na Kiyovu na hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, Simba imepania kuishinda Kiyovu idadi kubwa ya mabao kwa lengo la kujenga heshima kwa klabu hiyo.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliieleza Burudani kuwa, moja ya sababu zilizoifanya timu hiyo ishindwe kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ni wachezaji kuathiriwa na hali ya hewa.
Kikao hicho kiliamua kuwa, timu iingie kambini mara baada ya Taifa Stars kumenyana na Msumbiji katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2013. Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Februari 29 mwaka huu.
Simba imeshindwa kuingia kambini mapema kujiandaa kwa mechi hiyo kutokana na wachezaji wake tisa kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, ambacho leo kitamenyana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mechi ya kirafiki.
Mbali na timu kuingia kambini mapema, kamati hiyo pia imepanga kuwazawadia wachezaji donge nono la fedha iwapo watashinda mechi hiyo na kusonga mbele.

Upendo Kilahiro kufanya makubwa tamasha la PasakaMWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili mwenye sauti nyororo, Upendo Kilahiro amekuwa wa kwanza kuthibitisha kushiriki katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, alisema mjini Dar es Salaam kuwa, Upendo amemthibitishia kwamba atashiriki tamasha hilo.

"Kilahiro tutakuwa naye kwenye tamasha na naamini kwamba mwaka huu tamasha hili litakuwa bora zaidi kutokana na kushirikisha waimbaji wengi wakali," alisema Msama.

Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo la aina yake, baada ya kufanyika Dar es Salaam, pia litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9.

Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi kadhaa za Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, Upendo alisema amepania kufanya mambo makubwa katika tamasha la mwaka huu na atapanda jukwaani kuimba 'live' na bendi yake ya Upendo Kilahiro. "Natoa mwito kwa mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi, watarajie kupata vitu vizuri na tofauti zaidi... watapata vitu vinono kwa vile tamasha hili linazidi kuwa bora zaidi. "

"Sikukuu ya Pasaka ni upatanisho kutokana na kifo cha Yesu Kristo aliyefia msalabani na kufufuka siku ya tatu... tutaienzi sikukuu hiyo kwa nderemo," alisema Upendo.

Mwanamuziki huyo anayeabudu katika Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam (Kwa Askofu Gamanywa), alisema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na mbali na kufanya mazoezi, pia atafunga na kusali ili Mungu amfanyie miujiza.

Aliwaomba mashabiki wamiminike kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 na Jamhuri Aprili 9 ili kuona mambo mazuri aliyowaandalia na kuongeza kuwa, kwa vile anamtukuza Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwakwe.

Alisema anatarajia kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo zilizotamba za Zindonga (alioimba kwa Kizulu), Unajibu Maombi na Ni Salama Rohoni. Upendo hivi sasa anatamba na albamu yake mpya ya Ficho Langu aliyoirekodi nchini Canada.

JENNIFER MGENDI NA UJIO MPYA WA INJILI


Salaam nyingi ziwafikie wapendwa.Naamini kwa neema ya Mungu, mmeuona mwaka 2012. Mimi pia, namshukuru Mungu.
Nachukua fursa hii kuwajulisha nilipo na ninapokwenda kwa mwaka huu na naomba kama kawa muwafikishie watanzania na wasomaji wenu kwa ujumla mambo haya. Natanguliza shukurani zangu za dhati.

DHAHABU.
Hii ni albamu yenye mkusanyiko wa baadhi ya nyimbo zangu za zamani kama vile Nini?, Nimrudishie nini Bwana, Nitafika lini?, Mbona washangaa njiani, Ulinipa sauti na nyinginezo ambazo zilitamba miaka ya 2001 na kurudi nyuma hadi mwaka 1995.

Albamu hii tayari ipo madukani katika mfumo wa audio cd yaani ni ya kusikiliza. Maandalizi ya video hii yanafanyika na panapo majajliwa, mwezi Agosti itakuwa imekamilika.
TEKE LA MAMA
Filamu hii ipo madukani na imewashirikisha watu mbalimbali kama Bahati Bukuku, Christina Matai, Senga, Lucy Komba na Godliver a.k.a Bibi Esta. Sio filamu ya kukosa kuangalia na uzuri wake unaweza kuiangalia ukiwa umetulia na familia yako bila kuwa na wasiwasi wa kuanza kuwatuma watoto dukani ili wasione picha chafu.
SHEREHE ZA MIAKA 15 YA HUDUMA.
Panapo majaliwa ya Mungu, natarajia kufanya tamasha la kusherehekea na kumshukuru Mungu kwa miaka 15 tangu nianze huduma ya uimbaji. Tamasha au sherehe hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 05 Agosti, 2012 katika ukumbi wa Landmark Hotel.Video ya album ya Dhahabu itazinduuliwa siku hiyo pia.
Maandalizi ya tamasha hili yanaendelea na litapambwa na waimbaji mbalimbali watakaoimba live siku hiyo. Sio siku ya kukosa na wote wenye mapenzi mema wanaombwa kujitokeza kwa wingi. Tutaendelea kuhabarishana kuhusu tukio hili kadri siku zinavyoendelea.
ALBAM MPYA

Maandalizi ya album mpya yanaendelea moyoni, lakini rasmi kabisa yataanza mara baada ya tamasha la mwezi wa Agosti na album hii mpya inatarajiwa kuingia sokoni mwezi Aprili mwaka 2013, tukijaliwa uzima.
Ni hayo tu ndugu zangu nawatakia siku njema

Wednesday, February 22, 2012

NCHUNGA: Tutabadili kikosi chetuMWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga amesema bado kikosi chao kina nafasi kubwa ya kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika licha ya kutoka sare ya bao 1-1 na Zamalek.
Nchunga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, ana imani kubwa kuwa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic atafanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Zamalek ya Misri.
Kiongozi huyo wa Yanga alisema tayari wameshampatia maelekezo Papic ya kukifanyia marekebisho kikosi chake ili kiweze kuibuka na ushindi.
Licha ya kupata nafasi nyingi za kufunga mabao, Yanga ilishindwa kutamba mbele ya Zamalek baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao 1-1. Mechi hiyo ilichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu mbili hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Cairo na timu yoyote itakayoshinda mechi hiyo itasonga mbele.
Nchunga alisema wamepata uhakika wa ushindi katika mechi ya marudiano baada ya kupona kwa baadhi ya wachezaji wao nyota kama vile kiungo Nurdin Bakari na kipa Yaw Berko.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa, baadhi ya wafadhili wa klabu hiyo wamejitokeza kuwapa motisha wachezaji kwa lengo la kuwaongezea ari ya kufanya vizuri, lakini hakutaja motisha hiyo.
Kuna habari kuwa, mechi hiyo huenda ikachezwa nchini Sudan, kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni wakati wa mechi ya ligi kati ya Al- Ahly na Al-Masry na kusababisha vifo vya mashabiki 74.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema sare waliyoipata dhidi ya Zamalek katika mechi yao ya awalihaijawakatisha tamaa ya kusonga mbele.
“Najua mechi ya marudiano itakuwa ngumu mjini Cairo, lakini nitahakikisha nawaandaa vyema vijana wangu,”alisema.

Zamalek yaikamia YangaMshambuliaji Amr Zaki wa Zamalek akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kusawazisha ilipomenyana na Yanga katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. (Na mpiga picha wetu).


KOCHA Mkuu wa Zamalek, Hassan Shehata amesema wapo tayari kurudiana na Yanga mahali popote, hata kama itakuwa nje ya Misri.
Shehata ameueleza mtandao wa cafoline wiki hii kuwa, wanachosubiri kwa sasa ni maelekezo kutoka Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Misri aliiongoza Zamalek kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Cairo, lakini upo uwezekano mkubwa kwa pambano hilo kuchezwa bila watazamaji ama kuhamishiwa katika nchi nyingine.
“Tunasubiri maamuzi ya CAF iwapo tutacheza Cairo au la, ‘ alisema Shehata.
Kocha huyo ameyaelezea matokeo ya sare kati yao na Yanga kwamba yalikuwa mazuri kwao na kuongeza kuwa walikuwa wakiyahitaji.
Aliisifu Yanga kuwa ni timu nzuri na yenye kocha mzuri, lakini alisisitiza kuwa, wana uhakika mkubwa wa kuitoa na kusonga mbele.
Kwa upande wake, mshambuliaji Amr Zaki wa Zamalek amesema hana uhakika kuhusu mahali itakapochezwa mechi yao ya marudiano dhidi ya Yanga.
Hata hivyo, Zaki amesema wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo na aliisifu Yanga kuwa ni timu nzuri. Zaki ndiye aliyeifungia Zamalek bao la kusawazisha.
CAF ndiyo yenye uamuzi wa mwisho iwapo pambano hilo la marudiano kati ya Yanga na Zamalek, lichezwe mjini Cairo bila watazamaji ama lihamishiwe katika nchi nyingine.
Hatua hiyo imekuja kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni mjini Port Said na kusababisha vifo vya mashabiki 74 wakati wa mechi ya ligi kati ya Al-Ahly na Al-Masry.
Kufuatia vurugu hizo, Shirikisho la Soka la Misri liliamua kusimamisha mechi zote za ligi nchini humo ili kupisha uchunguzi. Hadi sasa, bado shirikisho hilo halijatoa uamuzi wa kuruhusu ligi hizo ziendelee.

Mwisho, Meryl wapata mtoto wa kike


MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la Big Brother Africa mwaka 2008, Mwisho Mwampamba na mpenzi wake, Meryl wa Namibia wamepata mtoto.
Habari za kuaminika kutoka kwenye mitandao mbalimbali zimeeleza kuwa, Meryl amejifungua mtoto wa kike mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Whindhoek.
Mwisho na Meryl walishiriki katika shindano hilo mwaka 2008, ambapo Mwisho alishika nafasi ya pili nyuma ya Makubale wa Zambia, aliyeibuka mshindi.
Mwisho na Meryl walifunga ndoa mwaka 2011 baada ya kuonyeshana mapenzi mazito wakati wa shindano la Big Brother Africa-All Stars lililowashirikisha nyota wa zamani.
Kujifungua kwa Meryl ni mwendelezo wa baadhi ya washiriki wa shindano hilo kufunga ndoa na kupata watoto. Mwaka jana, washiriki wengine wa shindano hilo, Kevin wa Nigeria na Elizabeth Gupta wa Tanzania walipata mtoto wa kike.
Katika mwendelezo huo, pia wamo Quinn Sieber wa Afrika Kusini na Jennifer wa Msumbiji, ambao wanatarajia kupata mtoto hivi karibuni.
Kabla ya kushiriki shindano la Bib Brother Africa-All Stars, Mwisho alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki nyota wa kizazi kipya nchini, Rehema Chalamila ‘Ray C’, lakini haukudumu kwa muda mrefu.
Mtanzania huyo pia amejitokeza kuwa mwigizaji bora wa filamu, ambapo mbali na kucheza filamu kadhaa za kibongo, pia amewahi kucheza filamu mbili za Kinigeria.

Nina usongo na muziki- Rich Mavoko


MSANII anayechipukia katika muziki wa kizazi kipya nchini, Rich Mavoko amejigamba kuwa, ana hasira na usongo wa muziki.
Rich ametoa majigambo hayo wiki hii wakati ambapo kibao chake kipya cha Silali kimekuwa kikitamba katika vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini.
Alisema anamshukuru Mungu kuona kwamba, kibao chake hicho kimepokelewa vizuri na mashabiki na kinashika namba moja kwenye chati mbalimbali za radio.
“Wimbo mmoja, lakini mafanikio kibao. Hii ni ishara njema kwamba huko mbele mambo yatakuwa mazuri zaidi,”alisema.
Rich alisema licha ya ugeni wake katika fani, yeye ni msanii aliyekamilika kwa vile ana uwezo mkubwa wa kuimba na kurapu.
Alisema kimuziki, ameamua kufuata nyayo za msanii Diamond, ambaye amemuelezea kuwa ana kipaji cha hali ya juu kimuziki.
“Nampenda sana Diamond kwa sababu yupo kivyake vyake na anakubalika kote,”alisema.
Rich alisema kwake, anamuona Diamond kama msanii aliyekaa kizaramo zaidi kutokana na aina ya muziki anaopiga na ujumbe wake kwa jamii.

DUDU BAYA: Nani kasema nimefilisika?


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii nyota wa zamani wa muziki wa kizazi kipya, Godfrey Tumaini ameibuka na kusema si kweli kwamba ukimya wake kimuziki umetokana na kuishiwa.
Tumaini, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Dudu Baya alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ukimya wake umetokana na kujihusisha kwake zaidi na mambo ya biashara.
Alisema amefikia uamuzi wa kufanya biashara kwa vile hapendi kutegemea muziki katika maisha yake yote.
Alisema kupitia kampuni yake ya promosheni ya Tumaini Entertainment na ile ya ujenzi ya Mambaz Timbers, amekuwa akifanya vitu tofauti kwa lengo la kujiendeleza kimaisha.
Dudu Baya alisema yeye ni msanii tofauti na wengine wa muziki wa kizazi kipya nchini kwa sababu hategemei sana muziki huo kuendesha maisha yake.
“Sio kweli kwamba nimefilisika. Nimeamua kuiga maisha ya wasanii wengine walioendelea kimuziki kama vile Robert Kelly,”alisema.
“Nimekuwa nikiitumia kampuni yangu ya Tumaini Entertainment kuandaa maonyesho na matamasha mbalimbali ya muziki. Nachukua bendi na wasanii, nawaandalia maonyesho,”aliongeza.
Dudu Baya alisema kampuni yake ya Mambaz Timbers inajihusisha na utengenezaji na uuzaji wa vifaa vya ujenzi na kwamba, anamshukuru Mungu mambo yake yanakwenda vizuri.

Real Madrid yanywea kwa CSKA Moscow


MOSCOW, Russia
MCHEZAJI Debutant Wernbloom wa CSKA Moscow ya Russia juzi alizima furaha ya Real Madrid ya Hispania baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika za majeruhi.
Wernbloom alifunga bao hilo dakika ya 93 kwa shuti lililombabatiza beki Alvaro Arbeloa wa Real Madrid na kuzima furaha ya mashabiki wa timu hiyo waliokuwa na uhakika mkubwa wa kuiona timu yao ikitoka uwanjani na ushindi.
Katika mechi hiyo ya awali ya hatua ya mtoano iliyochezwa kwenye uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, Real Madrid ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 28 kupitia kwa Cristiano Ronaldo, likiwa bao lake la 38 msimu huu.
Kufuatia sare hiyo, timu yoyote itakayoshinda mechi ya marudiano itakayochezwa Machi 14 mwaka huu mjini Madrid, itasonga mbele.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji Karim Benzema wa Real Madrid alilazimika kutolewa uwanjani mapema baada ya kuumia. Nafasi yake ilichukuliwa na Gonzalo Higuain.
Kocha Jose Mourinho wa Real Madrid alikiri baada ya mechi hiyo kuwa, wapinzani wao walikuwa wagumu na wakali.
Hata hivyo, Mourinho alisema ameridhika na matokeo hayo, ingawa alilaumu kushindwa kupata mabao kipindi cha pili akidai Real Madrid ilicheza kwa kiwango bora.
"Tuliwabana wapinzani wetu, hawakuweza kupata nafasi ya kufunga. Tulipata nafasi nzuri za kufunga kipindi cha pili, lakini tulishindwa," alisema Mourinho.

Chelsea hoi kwa Napoli


NAPLES, Italia
MABAO yaliyofungwa na Ezequiel Lavezzi na Edinson Cavan jana yaliiwezesha Napoli ya Italia kuibwaga Chelsea ya England katika mechi ya awali ya mtoano ya ligi ya mabingwa wa Afrika iliyochezwa mjini hapa.
Katika mechi hiyo, Napoli iliichapa Chelsea mabao 3-1 na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza hatua ya robo fainali.
Kipigo hicho kimeziweka timu za England kwenye nafasi finyu ya kufuzu kucheza robo fainali, kufuatia wiki iliyopita Arsenal kupigwa mweleka wa mabao 4-0 na AC Milan ya Italia.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, Chelsea ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa mshambuliaji wake, Juan Mata kufuatia uzembe wa nahodha wa Napoli, Paolo Cannavaro.
Levezzi aliisawazishia Napoli dakika ya 38 baada ya kupokea pasi akiwa ndani ya mita 18 na kufumua shuti kali lililomshinda kipa Petr Cech wa Chelsea. Mabao hay
Cavani aliiongezea Napoli bao la pili baada ya kumtoka beki mmoja wa Chelsea kabla ya kumtengenezea pasi murua Levezzi aliyeongeza bao la tatu dakika ya 65. Licha ya kupata kipigo hicho, Kocha Mkuu wa Chelsea, Andre Villas-Boas alijigamba kuwa, bado wanayo matumaini ya kushinda mechi ya marudiano na kusonga mbele.
“Tuna hakika tunaweza kubadili matokeo kwenye uwanja wa Stamford Bridge kwa sababu ya nafasi tulizopata usiku wa leo. Napoli walikuwa makini mbele ya goli lakini sisi hatukuweza kufanya hivyo. Tulifanya makosa mengi na Napoli walitumia nafasi hiyo,”alisema.
Kocha huyo alikiri pia kuwa, atalazimika kuifanyia marekebisho safu yake ya ulinzi kwa vile ilichangia kwa kiasi kikubwa wapinzani wao kupata mabao mawili ya kwanza.
Katika mechi hiyo, Chelsea ilicheza bila ya nahodha wake, John Terry, ambaye ni majeruhi na anatarajiwa kufanyiwa operesheni hivi karibuni itakayomfanya akae nje ya uwanja kwa wiki sita.
Kocha Mkuu wa Napoli, Walter Mazzarri alisema timu yake ilikuwa na uwezo wa kushinda mabao manne, ambayo yangeiweka kwenye nafasi nzuri katika mechi ya marudiano itakayochezwa mjini London.
“Chelsea ilicheza vizuri kama tulivyotarajia,lakini tuliwazidi mbinu, hasa katika ushambuliaji. Tulikuwa na wakati mgumu dakika 15 za kwanza, lakini baada ya kusawazisha, tulitulia na kucheza vizuri,”alisema.
Hata hivyo, Walter alikiri kuwa pambano lao la marudiano litakuwa gumu kwa vile wapinzani wao wanao uwezo wa kupata mabao mawili nyumbani.

KHADIJA KOPA: Taarabu ya sasa ni bifu tupu


Anashangaa kuona wasanii na viongozi hawaelewani

Asema bifu la TOT, Muungano lililenga kutafuta pesa

MTUNZI na mwimbaji nyota wa muziki wa taarab nchini, Khadija Omar Kopa amesema vikundi vya muziki huo kwa sasa vimetawaliwa na chuki binafsi miongoni mwa viongozi wake.
Khadija amesema chuki hizo pia zimetawala miongoni mwa wasanii, ambao baadhi yao wamekuwa hawaelewani na kuchukiana kwa sababu zisizokuwa na msingi.
Mwanamama huyo, ambaye ni kiongozi wa kikundi cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT), alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1.
“Bifu la sasa ni bifu kweli kweli, sio la kutungiana nyimbo tu, utakuta kikundi fulani cha taarab hakielewani na kikundi kingine na hata wasanii wake nao hawaelewani, ‘ alisema.
Khadija alisema bifu la aina hiyo kamwe haliwezi kuleta maendeleo ya muziki huo, badala yake litaufanya muziki huo udumae na kupoteza umaarufu kwa mashabiki.
Alisema wakati vikundi vya TOT na Muungano vilipokuwa kwenye chati ya juu miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa 2000, viongozi na wasanii wake walikuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na kamwe hawakuwa na bifu.
Alisema bifu la vikundi hivyo wakati huo lililenga kutafuta pesa na kuviletea maendeleo, halikuwa bifu la kuchukiana na kujengeana uhasama kama ilivyo sasa kwa baadhi ya vikundi vya muziki huo.
“Wakati ule tulikuwa tunatunga nyimbo za kujibishana, lakini lengo letu lilikuwa ni kutafuta pesa,”alisema Khadija, ambaye ni miongoni mwa waimbaji wakongwe wa muziki huo wanaotesa hadi sasa.
Khadija alisema ilikuwa kawaida ya vikundi hivyo viwili vilivyokuwa vikiongozwa na John Komba na Norbert Chenga kuandaa maonyesho makubwa ya taarab na kuhudhuriwa na mashabiki wengi kuliko hivi sasa.
Alisema waliweza kufanya maonyesho ya aina hiyo katika viwanja vikubwa kama vile wa Uhuru, Dar es Salaam, Jamhuri-Morogoro na ukumbi wa Vijana-Dar es Salaam, ambapo walipata pesa nyingi.
“Katika baadhi ya maonyesho, tuliweza kupata shilingi milioni 30 kwa onyesho moja na kwa wakati ule zilikuwa pesa nyingi sana,”alisema mwanamama huyo.
Khadija alisema baadhi ya wakati, Komba na Chenga walipoona kikundi kimoja kikitetereka kimuziki, walikuwa wakikutana na kupanga mikakati ya kukiinua.
“Mbinu walizokuwa wakizitumia kuinuana ni kuandaa kitu fulani cha pamoja na kutoleana lugha za kiushindani, zisizokuwa na matusi na mashabiki walikuwa wakishawishika kirahisi kujitokeza kuhudhuria maonyesho yetu,”alisema.
Licha ya kikundi cha TOT kutosikika sana kwa sasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, Khadija bado anang’ara kimuziki kutokana na tungo zake mbalimbali, ambazo zimetokea kuteka hisia za mashabiki wa muziki huo. Baadhi ya tungo hizo ni kama vile Top in town.
Akizungumzia utunzi wa nyimbo za taarab, Khadija alikiri kuwa ni kazi ngumu na inayohitaji uvumilivu na kujituma. Alisema binafsi amekuwa akitunga nyimbo zake nyingi nyakati za usiku.
“Ninapoamua kutunga wimbo, huwa nakesha usiku kucha nikiandika mashairi. Naandika, nafuta, naandika tena hadi alfajiri,”alisema.
Aliongeza kuwa, kazi ya kutia muziki katika nyimbo zake huwa sio ngumu kwa vile huwaelekeza wapigaji wa ala upigaji anaoutaka nao hufanya hivyo.
Hata hivyo, Khadija alisema wakati mwingine anapokuwa stejini, hufanya vitu tofauti na alivyourekodi wimbo wake kutokana na kupandwa na mzuka.
Khadija alianza kupata umaarufu alipokuwa katika kikundi cha Culture cha Zanzibar, ambako aling’ara na vibao vyake kama vile Wahoi, Daktari na Kadandie.
Baadaye alihamia Bara, ambako alijiunga na kikundi cha TOT wakati kilipoanzishwa mwaka 1993 kabla ya kuwa miongoni mwa waanzilishi wa kikundi cha East African Melody. Pia aliwahi kuimbia kikundi cha Muungano.

Friday, February 17, 2012

Simba, Yanga zaingia vitani kesho

Felix Sunzu

Emmanuel Okwi

Hamisi KiizaHaruna Niyonzima


Msimbazi waahidi mamilioni kwa wachezaji

Nurdin, Taita, Telela wamtesa Kocha Papic

Kuiona Zamalek sh. 50,000 na sh. 3,000

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya klabu za Afrika, Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii wanaanza kampeni zao kwa kumenyana na timu za Zamalek ya Misri na Kiyovu ya Rwanda.
Wakati Yanga itavaana na Zamalek katika mechi ya michuano ya klabu bingwa Afrika itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba watakuwa wageni wa Kiyovu katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa siku hiyo kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali.
Mechi zote mbili zinatarajiwa kuwa ngumu kwa vile Zamalek na Kiyovu ni timu nzuri, hivyo Simba na Yanga zitalazimika kufanyakazi ya ziada ili ziweze kuibuka na ushindi.
Simba inatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Rwanda ikiwa na msafara wa watu 40, wakiwemo wachezaji 18 na viongozi watano wakati Zamalek inawasili nchini kesho kwa ajili ya mechi yake na Yanga.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa, maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika na kwamba msafara huo utaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda.
Kamwaga alisema Simba itakwenda Rwanda bila ya wachezaji wake wawili nyota, Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu kutokana na kuwa majeruhi. Alisema Sunzu anasumbuliwa na maumivu ya kichwa wakati Boban anasumbuliwa na nyama za paja.
Hata hivyo, Kamwaga alisema kikosi chao kipo imara na mapengo ya Boban na Sunzu hayawezi kuwaathiri katika mchezo huo kwa sababu wachezaji wengine wote wapo fiti.
Naye Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema wamepanga kuwazawadia wachezaji wa timu hiyo mamilioni ya pesa iwapo wataishinda Kiyovu na kusonga mbele katika michuano hiyo.
Rage alisema wametoa ahadi hiyo kwa wachezaji kwa lengo la kuwaongezea morari na kuwafanya wacheze kwa kujituma.
Wiki iliyopita, Simba iliwazawadia wachezaji wake sh. milioni 12 baada ya kuifunga Azam mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Japokuwa Rage hakutaka kuweka wazi kiasi cha pesa watakachowazawadia wachezaji wao, kuna habari kuwa tayari baadhi ya matajiri wa Simba wameshachangia zaidi ya sh. milioni 25.
Rage alisema vijana wake wapo imara na wamejipanga vizuri kwa ajili ya vita yao dhidi ya Kiyovu. Alisisitiza kuwa, ushindi dhidi ya Wanyarwanda ni lazima.
Kwa upande wa Yanga, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa alisema maandalizi yote kwa ajili ya mechi hiyo yamekamilika.
Mwesigwa alisema Zamalek imepangiwa kukaa kwenye hoteli ya Hyant, lakini inaweza kuhamia hoteli nyingine kwa kuongeza malipo iwapo itaamua kufanya hivyo.
Kwa kawaida, timu za Misri hupenda kukaa hoteli ya Serena (zamani Movenpick) ama New Africa kila zinapokuja nchini kucheza mechi za kimataifa.
Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic alisema juzi kuwa, bado ana wasiwasi kuhusu hali za wachezaji, Nurdin Bakari, Godfrey Taita na Salum Telela, ambao ni majeruhi.
Papic amesema kuumia kwa wachezaji hao ni pigo kubwa kwa Yanga kwa sababu kila mmoja ana mchango wake katika timu.
Kwa mujibu wa Papic, Taita na Telela wameumia mguu na watakuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa wakati Nurdin amefunguliwa plasta ngumu (POP) baada ya kuumia kidole.
Hata hivyo, kocha huyo kutoka Serbia alisema kikosi chake kipo imara na kwamba atawatumia wachezaji wengine waliopo kwa ajili ya kuziba mapengo yao.
Wakati huo huo, kiingilio cha juu katika mechi kati ya Yanga na Zamalek kitakuwa sh. 50,000 kwa VIP A na sh. 30,000 kwa VIP B.
Viingilio vingine ni VIP C sh. 15,000, viti vya machungwa sh. 7,000, viti vya bluu sh. 5,000 na viti vya kijani sh. 3,000.

AFC yashuka darajaTimu ya AFC ya Arusha imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya 94 KJ iliyokuwa ichezwe jana (Februari 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya FDL timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.

Si Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimamizi wa ligi hiyo Kituo cha Pwani wala Kamishna wa mechi hiyo Ramadhan Mahano waliokuwa na taarifa yoyote ya mapema juu ya AFC kushindwa kufika kituoni.

AFC ambayo mbali ya kushushwa daraja inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya kucheza Ligi ya Taifa msimu ujao. Sh. 500,000 kati ya hizo zitakwenda kwa timu ya 94 KJ iliyoingia gharama za kujiandaa kwa mechi hiyo ambapo wapinzani wao hawakufika uwanjani. Kundi C la ligi hiyo sasa linabakiwa na timu nne baada ya Manyoni FC ya Singida nayo kushuka daraja kwa kushindwa kucheza mechi yake dhidi ya Polisi Tabora iliyokuwa ifanyike Februari 12 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Timu zilizobaki katika kundi hilo ambalo baada ya mbili kujitoa hakuna itakayoshuka daraja ni 94 KJ ya Dar es Salaam, Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora.

Poulsen atangaza kikosi cha StarsKocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen leo (Februari 16 mwaka huu) ametangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Kabla ya kuivaa Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezwa Februari 29 mwaka huu. Kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki Februari 23 mwaka huu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) itakayofanyika kwenye uwanja huo huo. Wachezaji wapya walioitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Februari 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni viungo Jonas Gerald (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Kikosi kamili kinaundwa na makipa Shabani Kado (Yanga), Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam).

Mabeki ni nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Juma Jabu (Simba), Stephen Mwasika (Yanga) na Kelvin Yondani (Simba).

Viungo ni Jonas Gerard (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Shomari Kapombe (Simba), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Abdi Kassim (Azam).

Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam), Nizar Khalfan (Philadelphia Union, Marekani), Mrisho Ngasa (Azam), Ally Badru Ally (Canal Suez, Misri), Uhuru Selemani (Simba) na Nsa Job (Villa Squad).

Thursday, February 16, 2012

MAMBO YA TWANGA PEPETAMwimbaji wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta, Dogo Rama (kushoto) akicheza na mcheza shoo wa bendi hiyo, Maria Saloma wakati wa onyesho la siku ya wapendanao lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa Equator Grill, Temeke, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege).

KANUMBA: Nitafunga ndoa wakati utakapowadia


MSANII nguli wa uigizaji filamu nchini, Steven Kanumba amesema atafunga ndoa pale wakati utakapofika kwa vile suala hilo si la kukurupuka.
Akihojiwa katika kipindi cha One Actions cha kituo cha televisheni cha Clouds, akiwa mbele ya mama yake mzazi, Kanumba alisema suala la kufunga ndoa linahitaji umakini mkubwa.
“Siku zote mke mwema anatoka kwa Mungu. Yeye ndiye anayejua mke yupi atakayenifaa,”alisema msanii huyo, ambaye anamiliki kampuni ya Kanumba The Great Films.
“Mungu huwa hachelewi wala hawahi kumpatia mja wake mke bora. Hutoa kila kitu kwa wakati mwafaka,”aliongeza msanii huyo, ambaye anaongoza kwa kucheza filamu nyingi za kibongo.
Hata hivyo, Kanumba hakuwa tayari kusema ni lini anatarajia kufunga ndoa, lakini alisisitiza kuwa, atafanya hivyo baada ya kupata kibali kutoka kwa Mungu.
“Siwezi kusema ni lini nitafunga ndoa. Napenda kuoa, nataka kuoa, lazima mke atapatikana, lakini ni hadi pale atakapopatikana. Mungu akitoa kibali, nitaoa, ‘ alisema.
Wakati wa mahojiano hayo, mama wa msanii huyo alisema anapenda kumuona mwanaye akioa na kupata watoto yeye (mama) akiwa angali hai.
‘Unajua mama, mke anatoka kwa Mungu. Ana mipango yake. Bado hajafanya miujiza hiyo kwangu. Ipo siku nitaoa, nitapata watoto, lakini bado muda haujafika, ‘ alimweleza mama yake.
Hii ni mara ya kwanza kwa Kanumba kuzungumza hadharani masuala yanayohusu kufunga ndoa. Wadau wengi wa sanaa nchini wamekuwa wakimuuliza msanii huyo ni kwa nini hajafunga ndoa hadi sasa.
Amekuwa akiulizwa swali hilo kutokana na ukweli kwamba, msanii huyo ana kila kitu kinachoweza kumfanya aishi maisha mazuri hapa duniani, ikiwa ni pamoja na kuwa na nyumba nzuri na ya kifahari pamoja na magari ya bei mbaya.
Mbali na kumiliki nyumba na magari, imeelezwa pia kuwa, Kanumba ndiye msanii anayeongoza kwa utajiri miongoni mwa wacheza filamu wa kibongo, ikiwa ni pamoja na kumiliki kampuni yake ya kutengeneza filamu.
Akizungumza katika kipindi hicho, mama wa msanii huyo alisema kijana huyo alizaliwa mwaka 1986 na wakati wa kuzaliwa, alitanguliza miguu kwa vile alikaa vibaya tumboni.
Alisema jina la Kanumba ni la babu yake na maana yake ni mtu aliyeshindikana kurogwa. Alisema alipewa jina hilo kwa sababu wakati wa uhai wake, aliwahi kuugua na kuhisiwa angekufa kwa vile alirogwa, lakini akapona kwa miujiza ya Mungu.
Wakati huo huo, Kanumba amesema hakuna kitu rahisi popote pale duniani na kwamba ili mtu aweze kufanikiwa kimaisha, lazima akumbane na vikwazo vingi na vya kila aina.
Kanumba amesema hilo pia lipo katika tasnia ya filamu nchini kwa vile hakuna msanii anayeweza kupata mafanikio kirahisi bila kukumbana na vikwazo.
Msanii huyo alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa chuo maalumu kwa ajili ya mafunzo ya filamu nchini, (Tanzania Film Training Center) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.
“Nakumbuka baada ya kujiunga na kundi la sanaa la Kaole,nilikaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuonekana katika televisheni na nilikuwa natamani kweli, hasa pale nilipokuwa nikiwaona akina Mashaka wakiigiza, ‘alisema.
‘Lakini nafasi hiyo ilikuwa adimu kwangu, hivyo nilivumilia na wasanii nao wanapaswa kuwa wavumilivu, ndio maana wapo chuoni hapa,”alisema Kanumba.
Alimpongeza mkurugenzi wa chuo hicho, Emanuel Mlyamba ‘Pastor Mlyamba’ kwa kubuni wazo zuri la kufungua chuo hicho, akiamini kuwa kinaweza kuleta mageuzi makubwa katika fani hiyo.
Kanumba alisema amefarijika kuona kuwa, mtu aliyemkaribisha kwenye fani hiyo, ameweza kuanzisha chuo hicho kabla ya yeye kuwa na wazo hilo.
Gharama ya masomo katika chuo hicho ni sh. 480,000 kwa kozi ya miezi mitatu.

Sizitaki tuzo zenu-Dully Sykes


MSANII machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Dully Sykes amewataka waandaaji wa tuzo za muziki wa Kilimanjaro, waondoe jina lake kwenye orodha ya washindani wa tuzo za mwaka 2011.
Dully alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, alishatangaza kujitoa kwenye tuzo hizo tangu mwaka juzi hivyo anashangaa kuona waandaaji wameendelea kuorodhesha jina lake.
“Nilishawaambia, sitaki kuwemo tena katika tuzo zao, lakini nashangaa kuona wanaendelea kuniweka tu. Kwani wananiona mimi ndio msanii pekee?” Alihoji msanii huyo.
“Wakati ule wa hits kama nyambizi na zinginezo mbona hawakunipa tuzo? Au walidhani mimi ni msanii, ambaye ningeishia kati tu,” aliendelea kulalamika msanii huyo.
Alisema uamuzi wa waandaaji wa tuzo hizo kuendelea kumshirikisha kuziwania, umetokana na kubaini ukweli kwamba yeye bado ni mkali katika fani.
“Nimeshasema sitaki, sizitaji tuzo zenu,” alisisitiza msanii huyo, ambaye amewahi kutamba na vibao kadhaa kama vile Shekide.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa Dully, mratibu wa tuzo hizo kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Angelo Ruhala alisema hawana taarifa.
“Kama msanii ameamua kujitoa, basi aandike barua BASATA ya kujitoa, sio kuzungumza kwa maneno mitaani,”alisema.

Davina aibukia filamu ya Diana


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye msanii chipukizi wa filamu nchini, Halima Yahaya ‘Davina’ amerejea kwenye fani hiyo kwa kishindo.
Safari hii, Davina amecheza filamu mpya, inayojulikana kwa jina la Diana, ambayo imeongozwa na gwiji wa fani hiyo, Single Mtambalike ’Richie’.
Kuibuka upya kwa Davina kumekuja miezi kadhaa baada ya kudaiwa kuwa, aliamua kuipa fani hiyo kisogo kutokana na masuala ya uzazi.
Davina alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kwa sasa yupo tayari kwa ajili ya kazi na kuonyesha maajabu.
“Baada ya mapumziko ya muda, narudi kwa nguvu, nakuja na filamu ya Diana,”alisema mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.
”Ni filamu ambayo kila mtazamaji atakapoitazama, ataikubali. Unajua uwezo bado ninao, lakini kutokana na majukumu, niliamua kupumzika kidogo na sasa ni kazi tu,”alisema mwanadada huyo.
Kwa upande wake, Richie alisema baadhi ya wasanii huamua kupumzika kutokana na kutingwa na majukumu mengine ya kimaisha na si kumalizika kiusanii.
”Davina ni msanii mwenye kipaji na bado ana uwezo mkubwa katika fani na hilo litathibitika ndani ya filamu ya Diana,”alisema.
Mbali na Davina, wasanii wengine walioshiriki kucheza filamu hiyo ni Juma Chikoka ’Chopa’ na Catherine.

GENEVIEVE: Nimechoka kuishi pweke, nataka kuolewa


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nollywood, Genevieve Nnaji amekiri kuwa, amechoka kuishi mpweke na sasa anataka kuolewa na kuwa na familia.
Genevieve amesema ameishi pweke kwa miaka mingi na kwamba anajisikia vibaya pale anapowaona rafiki zake wengi wakiwa wameolewa.
Mcheza filamu huyo anayeshika namba tano kwa utajiri miongoni mwa waigizaji wa kike wa Nollywood, alisema hayo wiki hii kupitia mtandao wa twitter.
Kauli hiyo ya Genevieve ilitokana na mmoja wa rafiki zake wa utotoni, kumtumia picha ya siku ya harusi yake kupitia blackberry.
“Nimechoka kuishi maisha ya upweke, rafiki zangu wengi sasa wameolewa,”alisema Genevieve akimweleza rafiki yake huyo.
Kwa kipindi kirefu sasa, Genevieve amekuwa akihusishwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki nyota wanchi hiyo, D’Banj, lakini wote wawili wamekuwa wakikanusha madai hayo.
Genevieve na D’Banj walikaririwa kwa nyakati tofauti wakisema kuwa, uhusiano wao ni wa kawaida, kama vile wa kaka na dada.
Wakati huo huo, baadhi ya ndugu na marafiki wa mwigizaji mwingine nyota wa nchi hiyo, Rita Dominic wamemtaka aachane na maisha ya usichana, badala yake afunge ndoa.
Rita, ambaye anashika nafasi ya tatu kwa utajiri miongoni mwa waigizaji wa kike wa Nollywood, amekuwa akihusishwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu mwenzake, Jim Iyke.
Hata hivyo, urafiki wao ulikufa baada ya Jim kuonekana kuwa hayupo tayari kufunga ndoa na Rita.
Ndugu na marafiki hao wamemweleza Rita kuwa, muda wa kuishi kiusichana umekwisha na kwamba kwa sasa anahitaji kuwa na mume na watoto.
Rita pia amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume kadhaa, lakini hakuna yeyote kati yao aliyeonyesha dhamira ya kutaka kumuoa.

Mzee Yusuph, Ally J, Thabiti kumalizana ubishi Machi 2

MZEE Yusuph

THABITI Abdul

ALLY J


WASANII nguli wa kupiga kinanda katika muziki wa taarab nchini, Mzee Yusuph, Ally J na Thabiti Abdul wanatarajia kumaliza ubishi kati yao Machi 2 mwaka huu.
Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa muziki huo, limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala, Dar es Salaam.
Yusuph ni kiongozi wa kundi la Jahazi, Ally J ni rais wa kundi la Five Stars wakati Thabiti ni mmoja wa wakurugenzi wa kundi la Mashauzi Classic.
Magwiji hao wa kupapasa kinanda, wamekubaliana kupambana kwa lengo la kumaliza ubishi wa muda mrefu juu ya nani mkali kati yao.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ally J alisema pambano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya mameneja wao.
“Kusema ule ukweli, Mzee Yusuph ni mdogo kwangu. Wakati anaanza kupiga kinanda East African Melody na baadaye Zanzibar Stars, mimi ndiye niliyemshauri aachane na fani hiyo, nikamtaka ajikite zaidi katika uimbaji,”alisema Ally J.
Aliongeza kuwa, alimpa ushauri huo Yusuph baada ya kuona uwezo wake katika kupiga kinanda ni mdogo na kipaji chake kipo kwenye uimbaji zaidi.
Ally J alisema amepiga kinanda katika nyimbo nyingi zilizoimbwa na Yusuph kama vile Kipendacho roho, Pwani ya Kiwengwa na nyinginezo, na alikuwa akimpa shavu kwa kumwita jina lake katika nyimbo hizo kutokana na ukali wake.
“Sasa nashangaa anaposema yeye ndiye kanifundisha kupiga kinanda. Asingeweza kunitaja kwenye nyimbo zake kama nisingempigia kinanda vizuri,”alisema.
Ally J alisema inawezekana Yusuph na Thabiti wamemzidi umri, lakini katika kupiga kinanda, hakuna anayemuweza kati yao.
Alisema hata kama ataamshwa saa 10 usiku kutoka usingizini, ana uwezo wa kupiga kinanda katika wimbo wowote.
Majigambo hayo ya Ally J yamekuja siku chache baada ya Yusuph kumponda yeye na Thabiti kwa madai kuwa ni wachanga katika fani ya upigaji wa kinanda katika taarab.
Yusuph alisema pia kuwa, yupo tayari kupambanishwa na wasanii hao wawili wakati wowote na mahali popote kwa vile ana uhakika mkubwa wa kuwatoa nishai.
Juhudi za kumtafuta Thabiti ili kuzungumzia pambano hilo hazikuweza kufanikiwa kwa vile simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Mwanamuziki wa Nigeria afunika tamasha la Busara


MWIMBAJI nguli wa muziki wa Nigeria, Nneka Egbuna mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya shoo ya aina yake na ya kihistoria katika tamasha la tisa la Sauti za Busara.
Tamasha hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Ngome Kongwe mjini hapa, lilihudhuriwa na mashabiki lukuki, ambao walivutiwa na muziki wa mwanadada huyo.
Kabla ya kutinga kwenye tamasha hilo, Nneka alifanya maonyesho katika nchi za Kenya, Rwanda na Uganda.
Katika onyesho la juzi, Nneka aliimba nyimbo kadhaa kutoka katika albamu yake mpya, aliyoiachia mwaka jana, iitwayo ‘ Soul is Heavy’.
Baadhi ya nyimbo hizo zilikuwa zikizungumzia mapenzi, machungu na alizipiga katika mahadhi ya reggae, hio hop, R&B na vintage soul.
Mwanadada huyo alikuwa akiimba huku akisaidiwa na Garry Sullivan kutoka Marekani (drums), Emmanuel Ngolle Pohossi kutoka Cameroon (besi), Jonas ‘Mo’ Da Silva Pinheiro kutoka Brazil (gita) na Nis Goetting kutoka Ujerumani (kinanda).
Akizungumza wakati wa onyesho hilo, Nneka alisema rushwa ni ugonjwa wa kijamii, ambao ulikuwa ukipigwa vita na marehemu Fela Anikulapo Kuti wa Nigeria. Alisema rushwa ina athari kubwa kwa bara la Afrika na kutolea mfano wa jimbo la Niger Delta, alikozaliwa na kukulia.
Mara baada ya kumaliza kupiga nyimbo zake, mashabiki waliohudhuria tamasha hilo hawakutaka ashuke jukwaani. Waliomba aendelee kuwaburudisha. Uimbaji wake na ujumbe alioubeba umedhihirisha kuwa muziki unatumia lugha, ambayo inaweza kufikisha ujumbe kirahisi zaidi.
Mwanamuziki huyo alirekodi albamu yake ya kwanza mwaka 2005 inayokwenda kwa jina la ‘Victim of truth’ na kufuatiwa na No Longer At Easy aliyoitoka mwaka 2008.
Tamasha hilo la tisa lilipambwa kwa burudani kutoka kwa wanamuziki mbalimbali maarufu kutoka nchi za Afrika na vikundi vya muziki tofauti vya Tanzania.
Wanamuziki kutoka nje waliopamba tamasha hilo ni Hanitra kutoka Madagascar, kikundi cha Camirata kutoka Sudan, Fredy Massamba kutoka Congo, Super Mazembe kutoka Kenya na Ogoya Nengo kutoka Japan.
Kikundi cha Mashauzi Classic kinachoongozwa na Isha Ramadhani nacho kilikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki kutokana na nyimbo zake maridhawa kama vile Mama nipe radhi na Tugawane ustaarabu.

MZEE GURUMO NA WANAWE
MWANAMUZIKI mkongwe, Muhidin Mwalimu 'Gurumo' (wa pili kushoto), akiongoza safu ya waimbaji wa bendi ya Msondo Ngoma wakati ilipotumbuiza katika ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita. Kutoka kushoto ni Eddo Sanga, Hassan Moshi na Juma Katundu. (Picha na Emmanuel Ndege).

Simba ipo gado-Kaburu


TIMU ya soka ya Simba inaondoka nchini kesho kwenda Rwanda kwa ajili ya mechi yao ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ’Kaburu’ alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu yake itakwenda Rwanda ikiwa na wachezaji 18 na viongozi watano.
Kaburu alisema Simba inakwenda Rwanda huku ikiwa imechukua tahadhari kubwa kwa hofu ya kuhujumiwa na wapinzani wao.
Alizitaja baadhi ya tahadhari walizochukua kuwa ni pamoja na kuwa makini na hoteli watakayopangiwa na wenyeji wao na uwanja watakaotumia kwa mazoezi.
Kiongozi huyo wa Simba alisema wamepata taarifa kutoka kwa mashushu wao kwamba, Kiyovu imepanga mbinu chafu za nje ya uwanja kwa lengo la kuwatisha na kuwapa hofu wachezaji na viongozi wa timu hiyo.
Alisema tayari baadhi ya watendaji wa Simba wameshatangulia kwenda Rwanda kwa ajili ya kuweka mambo sawa na pia kuhakikisha wanapambana na mbinu hizo.
"Tumejiandaa vizuri, tulipata kanda za michezo mbalimbali ya Kiyovu na tumezifanyia kazi. Kocha amepanga vizuri programu yake kuhakikisha tunashinda mjini Kigali,"alisema.
Kaburu amewashukuru maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kwa kuwapa ushirikiano mkubwa katika kujiandaa na mechi hiyo.
Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kwenda Rwanda ni makipa Juma Kaseja, Ally Mustapha, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Saidi Nassoro, Juma Jabu, Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Haruna Moshi na Mwinyi Kazimoto.
Wengine ni Salum Machaku, Edward Christopher, Ramadhani Singano, Gervas Kago, Rajabu Isihaka, Uhuru Selemani, Felix Sunzu na Emmanuel Okwi.
Simba na Kiyovu zinatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali na kurudiana wiki mbili baadaye mjini Dar es Salaam.

RD Dar aipasha YangaMKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik ameutaka uongozi wa klabu ya Yanga kuacha kupapatikia kuwasajili wachezaji wenye majina makubwa.
Badala yake, Sadik ameitaka klabu hiyo kuwekeza zaidi kwenye soka ya vijana ili iweze kuibua vipaji vipya na kuviendeleza.
Sadik alitoa mwito huo mwishoni mwa wiki iliyopita katika hafla ya kuichangia timu hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Peackok mjini Dar es Salaam.
Alisema anashangaa kusikia klabu ya Yanga ikihaha kutaka kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Mrisho Ngasa, iliyemuuza kwa mamilioni ya pesa kwa klabu ya Azam msimu uliopita.
Mkuu huyo wa mkoa alisema huu si wakati mwafaka kwa Yanga kumsajili tena mchezaji huyo kwa kutumia fedha nyingi wakati wapo vijana wengi wenye vipaji na uwezo wa kuitumikia timu hiyo.
Sadik alisema Yanga imekuwa ikipoteza fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni bila sababu wakati baadhi yao uwezo wao kisoka upo chini ikilinganishwa na wazalendo.
Alisema wakati umefika kwa Yanga kuwa na programu maalumu ya kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza kama ilivyokuwa miaka ya 1970, ambapo wachezaji wengi waliong’ara baadaye, walichezea timu ya vijana ya klabu hiyo.
Mkuu wa mkoa alisema Yanga inapaswa kuiga mfano wa watani wao wa jadi Simba kwa kuwa na timu za vijana wa umri mbalimbali kwa lengo la kuwaendeleza ili waje kuitumikia timu hiyo miaka ijayo.

Niyonzima: Zamalek inafungikaKIUNGO wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima amesema licha ya wapinzani wao, Zamalek kuwa ni timu kali, lakini wanafungika.
Niyonzima amesema kinachotakiwa kufanywa na wachezaji wa Yanga ni kucheza kwa ari na kujituma huku wakiwa na malengo.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda alisema hayo wiki hii alipokuwa akizungumzia maandalizi yao kwa ajili ya pambano lao na Zamalek.
Yanga na Zamalek zinashuka dimbani keshokutwa kumenyana katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Niyonzima alisema japokuwa Zamalek ni moja ya timu tishio barani Afrika, inaweza kufungwa na Yanga kama wachezaji watatimiza wajibu wao ipasavyo.
Alisema amewahi kucheza na Zamalek alipokuwa akichezea timu ya APR ya Rwanda na waliweza kuifunga mjini Kigali na kutoka nayo sare mjini Cairo.
‘Hakuna timu isiyofungika katika soka. Ni kweli timu za Misri zina mbinu nyingi, hasa zinapocheza kwao, lakini zinafungika,”alisema.
Kiungo huyo tegemeo wa Yanga alisema kuvurunda kwa timu yake katika baadhi ya mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara hakuna maana kwamba haina uwezo wa kuikabili Zamalek.
Alisema mechi za ligi ni tofauti na zile za michuano ya kimataifa na kwamba wachezaji hubadilika zaidi wanapopambana na timu ngumu.
”Katika ligi, timu zinakuwa zimezoeana na kufahamiana sana kimchezo, lakini katika mechi za kimataifa, wachezaji wanabadilika. Hivyo usishangae ukiiona Yanga inacheza tofauti itakapokutana na Zamalek,”alisema.
Amewataka wachezaji wenzake wa Yanga kucheza kwa ari na kujituma katika mechi hiyo huku wakiwa na dhamira ya ushindi na kusonga mbele.
Amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwataka wafike uwanjani kwa wingi kuishangilia na kuondokana na hofu kwamba timu yao inaweza kufungwa idadi kubwa ya mabao.

Sunday, February 12, 2012

BURIANI WHITNEY HOUSTON!


MWANAMUZIKI nyota wa Marekani na mcheza filamu nguli wa Holywood, Whitney Houston amefariki dunia ndani ya chumba cha hoteli ya Beverly Hilton mjini Los Angeles.

Mwili wa Houston (48) ulikutwa bafuni ndani ya chumba alichopanga na kuna habari kuwa, kabla ya kifo chake, alitumia dawa za kulevya na pombe. Mwanamuziki huyo alifariki saa 9.55 alasiri.

Hadi sasa, chanzo cha kifo cha mwanamuziki huyo hakijafahamika japokuwa Ijumaa jioni, alikuwa na baadhi ya rafiki zake wakinywa pombe katika baa ya hoteli hiyo.

Whitney alipangwa kutumbuiza katika sherehe za utoaji wa tuzo za Grammy, lakini mauti yalimkumba saa chache kabla ya sherehe hizo kuanza.

Gari la polisi liliwasili katika hoteli hiyo dakika chache baada ya muhudumu kupiga simu akieleza kwamba kuna mtu amekufa kwenye moja ya vyumba vilivyomo ghorofa ya nne.

Whitney alikuwa gwiji wa muziki wa pop na ndiye mwanamuziki anayetajwa kwamba, alikuwa na sauti nzuri. Baadhi ya nyimbo zake zilizompatia umaarufu mkubwa ni pamoja na I will always love you na Saving all my love for you.

Whitney alianza kujihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya baada ya kufunga ndoa na mwanamuziki mwingine nyota wa nchi hiyo, Bob Brown, aliyezaa naye mtoto mmoja wa kike, Bobbi Kristina.

Polisi wa Los Angeles wamesema inaweza kuchukua wiki sita hadi nane kuweza kubaini chanzo cha kifo cha mwanamuziki huyo.

Zambia mabingwa Afrika


LIBREVILLE, Gabon
TIMU ya soka ya taifa ya Zambia, Chipolopolo juzi iliweka historia ya aina yake baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuibwaga Ivory Coast kwa penalti 8-7 katika mechi kali na ya kusisimua ya fainali iliyochezwa mjini hapa.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa suluhu.
Katika kupigiana penalti tano tano, wachezaji nyota wa Ivory Coast, Didier Drogba, Yaya Toure na Gervinho walipoteza.
Zambia imetwaa kombe hilo miaka 19 tangu wanasoka na viongozi wake 18 walipofariki katika ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1993 nchini Gabon. Zambia ilirejea Gabon kwa lengo la kuweka historia ya kuwaenzi wanasoka hao.
Drogba ndiye aliyeikosesha Ivory Coast ushindi baada ya kupoteza penalti yake ndani ya dakika 90 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.
Zambia: Mweene,Musonda (Nyambe Mulenga 11), Sunzu, Himonde, Nkausu, Sinkala, Lungu, Chansa, Christopher Katongo, Kalaba, Mayuka, Nyambe Mulenga (Felix Katongo 74).
Subs Not Used: Kalililo, Kasonde, Mbesuma, Chamanga, Chivuta, Chintu, Kangwa, Sakuwaha, Titima.
Booked: Nyambe Mulenga.
Ivory Coast: Barry, Tiene, Toure, Bamba, Gosso, Zokora (Konan 75), Tiote, Toure Yaya (Bony 86), Gervinho, Kalou (Gradel 63), Drogba.
Subs Not Used: Yeboah, Boka, Doumbia, Coulibaly, Keita, Lolo, Eboue,Gnanahouan.Booked: Tiote, Bamba.
Referee: Badara Diatta (Senegal).