KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 3, 2012

Yanga, Polisi na utovu wa nidhamu

ILIKUWA Machi 10 mwaka huu wakati Yanga ilipomenyana na Azam katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ni pambano lililovuta hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, si tu kutokana na ushindani wa kisoka uliopo kati ya timu hizo, bali pia kila moja ilipania kushinda ili kujiweka kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.
Katika dakika za mwanzo, pambano hilo lilionekana kuwa zuri kutokana na kila timu kuonyesha soka ya kiwango cha juu huku mashabiki wakilipuka mayowe ya kuzishangilia. Ndani ya dakika 20 za mwanzo, Azam ikahesabu bao la kuongoza.
Mambo yalianza kubadilika baada ya wachezaji wa timu zote mbili kuanza kuonyeshana ubabe na hatimaye mwamuzi Israel Nkongo kumwonyesha kadi nyekundu kiungo Haruna Niyonzima baada ya kumpa kadi ya pili ya njano.
Ni kuanzia wakati huo, pambano hilo liligeuka uwanja wa vurugu. Wachezaji wa Yanga walimvamia Nkongo na kuanza kumpa kipigo huku nahodha wao Shadrack Nsajigwa akijitahidi kuwatuliza, lakini ilikuwa vigumu.
Kutokana na vurugu hizo, Nkongo aliamua kumtoa nje kwa kadi nyekundu beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa kosa la kutaka kumpiga. Yanga ikalazimika kucheza ikiwa na wachezaji tisa na hadi pambano lilipomalizika, ilichapwa mabao 3-1.
Kufuatia vurugu hizo, Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliwafungia wachezaji watano wa Yanga na kuitoza klabu hiyo faini ya jumla ya sh. milioni moja. Wachezaji waliofungiwa ni Cannavaro, Nurdin Bakari, Omega Seme, Jerry Tegete na Stephano Mwasika.
Mbali ya kuwafungia wachezaji hao, kamati hiyo pia iliwatoza faini
ya sh. 500,000 kila mmoja. Adhabu zote hizo zilitolewa kwa mujibu wa kanuni za ligi.
Hata hivyo, Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF iliamua kupunguza adhabu hizo baada ya Yanga kukata rufani, lakini iliongeza adhabu ya faini kwa wachezaji wote watano.
Vurugu zilizofanywa na wachezaji wa Yanga si tu kwamba ziliwashtua mashabiki wa soka nchini, bali pia ziliitia doa ligi hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa, matukio ya aina hiyo yalishasahaulika katika mchezo wa soka.
TFF ilikemea vikali vurugu hizo na kuwataka viongozi wa Yanga kusimamia nidhamu ya wachezaji wao. Pia uongozi wa Yanga uliomba radhi kwa mashabiki wa soka kutokana na vurugu hizo na kuahidi kuwa, kosa hilo halitajitokeza tena.
Mchezaji Mwasika, ambaye picha za video zilimwonyesha dhahiri akimtandika ngumi Nkongo, naye alimuomba radhi mwamuzi huyo pamoja na mashabiki wa soka nchini na kuahidi kutorudia kosa hilo. Mwasika alifungiwa kucheza mechi zote zilizosalia msimu huu baada ya kamati ya nidhamu kutengua adhabu yake ya kufungiwa kwa mwaka mmoja.
Tukio lingine lililoitia doa kubwa ligi hiyo msimu huu ni lile la wachezaji wa Polisi Dodoma kumpa kipigo mwamuzi Martin Saanya baada ya mchezo kati yao na Azam uliochezwa Aprili 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kufuatia vurugu hizo, Kamati ya Ligi ya TFF iliwafungia kucheza mechi tatu kila mmoja wachezaji tisa wa Polisi na pia kuwatoza faini ya sh. milioni moja kila mmoja.
Wachezaji wa Polisi waliofungiwa kwa mujibu wa kanuni ya 25(g)(iii) ni Noel Msekwa, Frank Sindato, Abdallah Matila, Bantu Admin, Salmin Kisi, Madope Mwingira, Sihaba Mkude, Kaliyasa Mashaka na Ibrahim Massawe. Iwapo wachezaji hao watahama Polisi na kujiunga na timu nyingine, watahama na adhabu zao.
Dosari nyingine iliyojitokeza katika ligi hiyo msimu huu ni Yanga kupokonywa pointi tatu katika mechi yake dhidi ya Coastal Union kwa kosa la kumchezesha beki Cannavaro wakati alikuwa na kadi nyekundu kwa kosa la kupigana.
Kitendo cha Yanga kumchezesha Cannavaro katika mechi hiyo kiliwashangaza wadau wengi wa soka kwa vile kanuni za ligi zipo wazi kwa mchezaji mwenye kadi nyekundu kwa kosa la kufanya vurugu uwanjani.
Wapo wadau waliowatupia lawama viongozi na benchi la ufundi la Yanga kwa kosa hilo huku wengine wakiilaumu kamati ya nidhamu na usuluhishi ya TFF, ambayo ilimpungumzia adhabu Cannavaro na wachezaji wengine wa klabu hiyo.
Kasoro nyingine ilijitokeza katika pambano kati ya Azam na Mtibwa Sugar lililochezwa Aprili 23 mwaka huu kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Pambano hilo lilishindwa kumalizika baada ya Mtibwa Sugar kugomea adhabu ya penalti iliyotolewa na mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma katika dakika ya 88. Mwamuzi akaamua kuvunja pambano hilo.
Kinachoshangaza, ripoti ya mwamuzi na kamisaa zilitofautiana kuhusu sababu za kuvunjika kwa pambano hilo. Mwamuzi hakusema alisubiri kwa muda gani kabla ya kulivunja wakati kamisaa alisema pambano lilivunjika kabla ya dakika 15 za kusubiri.
Kutokana na utata huo, kamati ya ligi iliamua kumuondoa Msangi na wasaidizi wake, Samuel Mpenzu na Abdalla Uhako kwenye orodha ya waamuzi wa ligi hiyo na kuipa Azam ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Uamuzi wa kamati hiyo ulizua malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa soka. Wapo walioilalamikia kamati kwa kushindwa kuiadhibu Mtibwa Sugar kulingana na kanuni, ambapo timu inayogomea mchezo, hutakiwa kushuka daraja.
Lakini wadau wengine wameilalamikia kamati kwa kuipa ushindi Azam wakati kosa lilifanywa na mwamuzi, ambaye aliamua kuvunja pambano huku wachezaji wa Mtibwa wakiwa bado wapo uwanjani.
Kamati ya ligi pia iliwaadhibu baadhi ya makamisaa kwa kushindwa kufika kwenye mechi walizopangiwa kusimamia bila kutoa taarifa na wengine walipewa onyo kali kutokana na ripoti za mechi walizosimamia kuwa na mapungufu.
Kutokana na kasoro hizo, ni vyema TFF ijipange vizuri zaidi ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali wachezaji watakaoendelea kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kupiga waamuzi uwanjani.
TFF pia inapaswa kuwa makini na makamisaa wanaoshindwa kutimiza wajibu wao. Pengine ni vyema TFF iwe na makamisaa wachache wanaofahamu na kutimiza wajibu wao kuliko kuwa na utitiri wa makamisaa, lakini wasiotambua vyema majukumu yao.

No comments:

Post a Comment