KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 24, 2012

LILIAN INTERNET: Niliwahi kucheza shoo nikiwa na mimba ya miezi sita



KWA mwonekano, Lilian Joseph Tungaraza ni msanii mwenye mvuto. Umbile lake, uso wake na rangi yake ni miongoni mwa vitu vinavyomfanya avutie kumkodolea macho. Kwa kifupi ni kwamba ameumbwa na kuumbika.
Sifa nyingine aliyonayo mwanadada huyu, maarufu zaidi kwa jina la Lilian Internet ni kwamba, ni hodari mno wa kulishambulia jukwaa kwa minenguo ya aina yoyote. Ni mwepesi wa kuchezesha maungo ya mwili wake mithili ya binadamu asiyekuwa na mifupa.
Kwa sasa, Lilian ni mmoja wa wacheza shoo nyota wa bendi ya muziki wa dansi ya Mashujaa, akitokea Twanga Pepeta International, aliyodumu nayo kwa zaidi ya miaka sita.
Uamuzi wa Lilian kujiunga na Mashujaa ulipokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa muziki nchini. Wapo wanaoamini kuwa, huo ni mwendelezo wa bendi ya Mashujaa kuibomoa Twanga Pepeta.
Wanaamini hivyo kwa sababu ni miezi michache tu iliyopita Mashujaa ilimnyakua mwimbaji nyota wa Twanga Pepeta, Charles Gabriel ‘Chalz Baba’ na baadaye mpiga gita la solo Ally Akida na mpiga tumba, MCD.
Lakini kwa upande wake, Lilian anapingana na dhana hiyo. Anasema aliamua kuihama Twanga Pepeta kwa lengo la kutafuta maslahi bora zaidi.
Akizungumza katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five wiki hii, Lilian alisema licha ya kulipwa pesa nyingi ili ajiunge na Mashujaa, amekuwa akipata malipo mazuri ya mshahara na pia fedha za matibabu, usafiri na nyumba.
Mbali na hilo, Lilian alisema amejiunga na Mashujaa kwa lengo la kupata uzoefu zaidi katika harakati zake hizo za kusaka maisha mazuri kupitia muziki.
“Nilipokuwa Twanga Pepeta, nilijiona kama vile nimebaki peke yangu. Wenzangu wote niliokuwa nao walihama. Nilijiona mpweke. Ndio sababu nilipopata ofa hii, sikusita mara mbili,”alisema msanii huyo.
“Sikuondoka Twanga Pepeta kwa kumkimbia mtu ama kugombana na mtu yeyote. Lengo langu ni kutafuta maslahi mazuri zaidi. Kama ni Twanga Pepeta, niliitumikia kwa miaka mingi, nikaona inatosha,”aliongeza.
“Kama unakaa na mume kwa miaka kadhaa na kuona huzalishi chochote, huwezi kuendelea kuishi naye, lazima utafute mume mwingine,” alisema msanii huyo huku akicheka.
Lilian alikiri kuwa, kazi ya kucheza shoo katika bendi za muziki ni ngumu na inazo changamoto nyingi, lakini amekuwa akijitahidi kukabiliana nazo.
Akitoa mfano, alisema baadhi ya mashabiki wa kiume wamekuwa wakipenda kuwadhalilisha wanapokuwa stejini kwa kuwatuza pesa kwa kuziingiza kwenye sehemu zao za siri.
“Kuna siku nilistukia nikitiwa singi (kusukumizwa kichwa) stejini na mwanamke, ambaye sikumjua. Nadhani huyo dada alipomuona bwanaake akija kunitunza, alikasirika akidhani nina uhusiano naye,”alisema Lilian huku akitabasamu.
Kutokana na ugumu wa maisha, Lilian alisema kuna wakati alipokuwa Twanga Pepeta, alilazimika kuendelea kucheza shoo stejini huku akiwa mja mzito wa miezi sita hadi kiongozi wake alipomzuia kwa hofu ya mimba kuharibika.
Lilian, ambaye ana mtoto mmoja wa kiume alisema, hapati tabu ya kumtunza mwanaye kwa vile amekuwa akiishi na dada yake bila ya kuwa na matatizo yoyote.
Alisema anamshukuru Mungu kwamba mtoto huyo si mlinzi na hana muda wa kutaka kujua mama yake yupo wapi, anafanya nini na kwa nini anachelewa kurudi nyumbani.
Lilian ameeleza kushangazwa kwake na baadhi ya wasichana, ambao ni wasanii ama wanamuziki wanaopenda kubadili rangi ya miili yao kwa kujichubua.
“Wao hudhani weupe ndio kivutio kwa mashabiki wanapokuwa stejini. Ni vizuri ujivunie rangi yako ya asili. Mimi sipati tabu katika hilo kwa sababu naipenda rangi yangu. Sipotezi muda kupaka madawa,”alisema.
Mwanadada huyo pia alikanusha madai kuwa, wacheza shoo wengi wa kike wamekuwa wakitumiwa na wanaume kwa kuwataka kimapenzi na kuwageuza vimada. Alisema uhuni ni tabia ya mtu na kwamba hata wasanii wa kiume wapo wanaotekwa kimapenzi na mashuga mami.
Alipoulizwa iwapo ni kweli viuno vya stejini vinafanana na vile vya kitandani wakati wa kufanya mapenzi, Lilian alitoa kicheko na kusema hilo haliwezekani.
“Ni kweli wapo wanaume wengi wanaodhani kwamba, akimchukua mcheza shoo wa kike na kwenda naye kufanya mapenzi, atampa viuno kama vile anavyokata stejini. Hilo haliwezekani kabisa,”alisema msanii huyo huku akiangua kicheko.
Lilian anavutiwa sana na mcheza shoo mwenzake, Super Nyamwela, ambaye yupo katika bendi ya Extra Bongo. Alisema Nyamwela ndiye mwalimu wake na pia mshauri wake mkuu katika masuala ya muziki na maisha kwa jumla.
Alikiri kuwa, kazi ya kucheza shoo ni ngumu na kwamba wacheza shoo wa kike wanahitaji muda mrefu wa kupumzika na kula chakula kizuri mara kwa mara ili kulinda afya zao.

No comments:

Post a Comment