KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, May 12, 2012

SIMBA YAFANYIWA KITU MBAYA SUDAN


Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum
WAPINZANI wa Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), Al Ahly Shendi ya Sudan, tayari wameanza visa.
Leo hii, wachezaji na viongozi wa Simba wametelekezwa kwa takribani masaa matano hotelini na wenyeji hao ambao walikuwa wameahidi kuipeleka Simba katika mji wa Shendi.
Wenyeji wa Simba nchini hapa ambao ni Shendi na Chama cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA), walikuwa wameahidi jana kwamba Wekundu wa Msimbazi wataanza safari ya kwenda Shendi mara baada ya kupata kifungua kinywa saa tatu asubuhi.
Hata hivyo, hadi kufikia saa nane mchana, hakukuwapo na basi lolote au mwakilishi yeyote wa kutoka Shendi au SFA aliyekwenda kwenye Hoteli ya Safiga ilikofikia Simba na kwa mujibu wa mawasiliano, walidai kwamba wamekwama kwenye foleni.
Hali hiyo ilisababisha wachezaji na viongozi wa Simba kushinda nje ya hoteli hiyo wakiwa wamekaa nje kwenye viti vichache, huku wengine wakiwa wamesimama tu kwa muda wa zaidi ya masaa mawili hadi matatu kwa vile muda wa kutoka hotelini ulikuwa umepita.
Kwa mujibu wa kanuni ya 14 (b) ya mashindano yanayosimamiwa na CAF, timu yeyote inatarajiwa kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine katika muda ambao unakubalika, labda kama imechelewa yenyewe.
Kuna umbali wa kilomita 150 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum iliko Simba hadi mji wa Shendi na kama Simba itachelewa kuondoka jijini hapa, maana yake ni kwamba itashindwa kufanya mazoezi leo jioni na hivyo Shendi na SFA wamekiuka kanuni hiyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alieleza kuchukizwa kwake na tukio hilo akisema linaonyesha namna Shendi na SFA walivyojipanga kutumia mbinu za nje ya uwanja kushinda pambano hilo la marudiano.
Katika pambano la kwanza lililofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
“Sisi tulitaraji kukumbana na yote haya ambayo tunayaona sasa. Wanajua kwamba hawataweza kuishinda Simba ndani ya uwanja na hivyo wameamua kutumia mbinu chafu.
“Bahati nzuri, wachezaji wetu, benchi la ufundi na sisi viongozi tumejiandaa kikamilifu kwa mambo kama haya. Hata hivyo, tutapeleka mashitaka yetu kwa kamisaa wa mechi yetu kwa vile wao Shendi walipokuja Dar tuliwahudumia vizuri kwa kila kitu,” alisema.
Kutokana na kuchelewa huko kuondoka, hoteli ya Safiga haikuwa imeandaa chakula cha mchana kwa wachezaji na ilibidi Rage na daktari wa timu, Dk. Cosmas Kapinga, waende kutafuta “vipoza njaa” kwa wachezaji wa Wekundu wa Msimbazi.
Kwa upande wake, Dk. Kapinga alisema inachofanyiwa Simba ni kitu ambacho kwa kitaalamu kinaitwa uchoshwaji wa kisaikolojia, lengo lake likiwa kuiathiri timu kiakili.
“Katika mazingira kama haya, wachezaji na viongozi wanashindwa kufikiria kuhusu mechi na badala yake wanafikiria kuhusu adha wanazozipata. Kama watakuwa hawajaandaliwa vizuri kisaikolojia, hii inaweza kuwa mbaya. Kwa bahati nzuri, wachezaji wa Simba wameandaliwa vizuri kwenye eneo hilo,” alisema Kapinga.

No comments:

Post a Comment