KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 18, 2012

Azam yawakana Okwi na Berko


KLABU ya Azam imesema haina mpango wa kuwasajili kipa Yaw Berko wa Yanga na mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Simba.
Katibu Mkuu wa Azam, Idrisa Nassoro alisema mjini Dar es Saalam wiki hii kuwa, wachezaji hao hawana nafasi kwenye kikosi cha timu hiyo.
Nassoro alisema taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki iliyopita kwamba wachezaji hao wameshasajiliwa na Azam hazina ukweli wowote na ni za uzushi.
“Azam itafanya usajili wake kutokana na mapendekezo ya Kocha John Stewart, ambaye kwa sasa yupo likizo Uingereza, lakini hatuna mpango wowote na Okwi ama Berko,”alisema.
Kwa mujibu wa Nassoro, usajili wa timu hiyo msimu ujao utazingatia zaidi wachezaji kutoka kikosi cha pili cha timu hiyo, ambacho kimekuwa kikifanya mazoezi kwa takriban mwaka mmoja sasa chini ya makocha wa kigeni na wazalendo.
Hata hivyo, Nassoro alisema mchezaji pekee wa kigeni waliyeamua kumsajili kwa ajili ya msimu ujao ni George Otieno kutoka Kenya. Alisema wamemsajili mchezaji huyo kutokana na kuridhishwa na kiwango chake.
“Tuna imani na matumaini makubwa na kikosi chetu, hivyo hatuhitaji mchezaji kutoka Simba au Yanga,”alisisitiza.
Nassoro alisema pia kuwa, Azam itaendelea kuwa chini ya Kocha Stewart msimu ujao baada ya kuiletea mafanikio makubwa katika misimu miwili iliyopita.
Alisema tangu mwaka 2000, hakuna timu nyingine ya ligi kuu zaidi ya Simba na Yanga iliyowahi kushika nafasi ya pili ama kutwaa ubingwa, hivyo kocha huyo anastahili kupongezwa.
Akizungumzia timu ya vijana ya Azam, Nassoro alisema imekuwa ikitoa wachezaji wengi wazuri kwenye timu za taifa za vijana wa chini ya miaka 17 na 20, hivyo wataendelea kuienzi kwa kuipatia huduma zote muhimu.
Nassoro alisema uongozi wa Azam unataka kuona timu hiyo ikiwa na hadhi kubwa barani Afrika kama ilivyo kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
“Ndoto zetu ni kubwa, sawa na Mlima Kilimanjaro. Tunataka Azam iwe zaidi ya TP Mazembe, lakini ni kazi kubwa, lazima mtoke jasho,”alisema.
Katibu Mkuu huyo wa Azam alisema, katika kutimiza ndoto hizo, moja ya mipango yao ya baadaye ni kufanya upanuzi wa uwanja wao wa soka wa Chamazi.
Alisema kwa sasa, hawawezi kuutumia uwanja huo kwa mechi za kimataifa kutokana na kutokidhi viwango, hivyo watalazimika kuutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ama viwanja vingine.
Nassoro alisema pia kuwa, katika kujiandaa kwa michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani,wamepanga kwenda kuweka kambi nchini Afrika Kusini.
Alisema uwepo wa Azam katika ligi na michuano ya kimataifa, ni kuzitangaza kampuni zilizo chini ya Azam, ambazo zimetapakaa katika nchi zote zinazopataka na Tanzania.
Alizipongeza Simba na Yanga kwa kufanya mambo makubwa katika kuendeleza soka nchini na kuongeza kuwa, mafanikio yao hayapaswi kubezwa.
Aliongeza kuwa, lengo la Azam ni kufika mbali zaidi katika mashindano ya kimataifa na ndio sababu wameamua kuanza maandalizi mapema.
“Rome ni mji mzuri duniani na watu wengi wanaupenda, lakini uzuri wake haukutokana na kazi ya siku moja. Hatutaki kuwana visingizio vya maandalizi mabovu ama kukosa huduma,”alisema.
“Timu yetu inaendeshwa kibiashara. Huwezi kusikia mchezaji anadi haki zake au hajalipwa. Kama wengine wameweza, kwa nini sisi tushindwe,”alisisitiza.

No comments:

Post a Comment