KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 30, 2012

KINNAH PHIRI: Wanasoka wa Tanzania hawajiamini

WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Taifa Stars kimeondoka nchini leo kwenda Ivory Coast, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Malawi, Kinnah Phiri amesema tatizo kubwa la wanasoka wa Tanzania ni kutojiamini. Phiri alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya Taifa Stars kutoka suluhu na Malawi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, kocha huyo anaelezea masuala mbalimbali kuhusu kikosi cha Taifa Stars.
SWALI: Timu yako ya soka ya taifa ya Malawi leo imecheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Taifa Stars. Ni kipi ulichokibaini kwa Taifa Stars katika mechi hiyo?
JIBU: Kwanza kabisa napenda kumpongeza kocha mpya wa Taifa Stars, Kim Poulsen kwa kupewa kazi ya kuinoa timu hiyo, kuchukua nafasi ya Jan Poulsen, ambaye niliwahi kukutana naye katika mechi kama hii.
Kwa ujumla, mtindo aliokuja nao Kim unaonyesha wazi kuwa, ana mwelekeo mzuri kwa kuita vijana wengi, ambao ndio damu changa kwenye kikosi, lakini nina hakika kwamba atakumbana na changamoto nyingi.
Changamoto hizo ni pamoja na kupigiwa kelele nyingi kutoka kwa mashabiki, hasa wale ambao wanapenda maendeleo ya haraka na kusahau kwamba mchezo wa soka unahitaji kuwekezwa mapema kwa kuwaandaa vijana tangu wakiwa wadogo.
Kitu kingine muhimu kwa watanzania kukitambua ni kwamba, kocha yeyote anapokabidhiwa timu kwa mara ya kwanza, ni lazima ichukue muda mrefu kwa wachezaji kuuelewa mfumo wake na kucheza anavyotaka. Hii ni kwa sababu wachezaji wameshazoea kucheza kwa mfumo waliofundishwa na kocha wa zamani.
Ni kweli katika kikosi cha sasa cha Taifa Stars wapo wachezaji wachache waliofundishwa na Jan Poulsen, lakini inawezekana kabisa kuwa, mfumo aliokuja nao Kim Poulsen ni tofauti, licha ya wote wawili kutoka nchi moja ya Denmark.
Katika mazingira haya, ni wazi kwamba zitajitokeza kasoro hizi na zile kwenye timu ya Taifa Stars, lakini baada ya wachezaji kuzoea, bila shaka mambo yanaweza kubadilika.
SWALI: Umegundua kasoro ipi kwa wachezaji wa Taifa Stars baada ya kucheza nao mechi ya leo?
JIBU: Tatizo pekee kubwa nililolibaini kwa wachezaji wa Taifa Stars ni kutojiamini wanapokuwa uwanjani. Inawezekana tatizo hili limetokana na mashabiki kuwazomea kwa vile siku zote mashabiki wanataka timu inapocheza nyumbani, ifanye vizuri.
Na ilivyo kawaida ni kwamba, mchezaji anapozomewa na mashabiki wake, anavunjika nguvu haraka kutokana na kuathirika kisaikolojia na ni rahisi kwa timu nzima kupoteana na kupoteza mchezo. Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa baadhi ya wachezaji, hawakuwa wakijiamini na ndio sababu kila mmoja alicheza kwa kutumia kipaji chake badala ya mfumo unaoeleweka.
Pamoja na kujitokeza kwa dosari hizo, nina hakika iwapo Taifa Stars itapewa muda zaidi, itakuwa na kikosi kizuri kwa sababu mafanikio yoyote katika soka, hayawezi kupatikana ndani ya wiki mbili ama mwezi mmoja.
SWALI: Malawi inakwenda kucheza na Uganda katika mchezo wa kusaka nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2014. Nini maoni yako kuhusu uwezo wa kikosi chako?
JIBU: Kwanza nimefurahi sana kupata mechi moja ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars kwa sababu ni moja ya timu nzuri na ninazoziheshimu. Sikutarajia iwapo Taifa Stars ingekuwa na wachezaji wengi vijana na wazuri kwa sasa. Kwa maana hiyo, nimepata kipimo kizuri sana.
Zipo kasoro chache zilizojitokeza kwenye kikosi changu baada ya kucheza mechi hiyo. Miongoni mwa kasoro hizo ni wachezaji wangu wa safu ya kiungo na ushambuliaji kujisahau. Nitalifanyia kazi tatizo hilo baada ya mechi yetu inayofuata dhidi ya Zanzibar na nina hakika hadi siku tutakapocheza na Uganda, mambo yatakuwa mazuri.
Jambo la msingi ni kwamba kikosi changu nacho kinaundwa na wachezaji wengi wapya na vijana waliochanganyika na wakongwe. Nina hakika baada ya kuelewana vyema, wataweza kuifikisha nchi yetu mbali katika mashindano haya makubwa duniani.
SWALI: Unatoa ushauri gani kwa Taifa Stars ili iweze kufanya vizuri katika mechi yake dhidi ya Ivory Coast itakayochezwa mwezi ujao?
JIBU: Ushauri wangu kwa Taifa Stars ni kwamba, iwapo watapata mazoezi ya pamoja kwa muda mrefu na kufuata mafunzo ya kocha wao, wataweza kufanya vizuri katika mechi yao dhidi ya Ivory Coast. Jambo la msingi kwa wachezaji ni kujiamini na kuondoa woga wa kukumbana na wachezaji wenye majina makubwa duniani. Wakifanya hivyo, nina hakika kazi ya kukabiliana na Ivory Coast haitakuwa kubwa. Lakini wakicheza kinyume na hapo. huenda mambo yakawa magumu kwao.
Kama ulitazama vizuri mechi yetu dhidi ya Taifa Stars, tuliwazidi sana kimchezo,hasa kipindi cha pili, ambapo walionekana kuchoka na kutoa nafasi kwa timu yangu kufanya mashambulizi mengi. Inawezekana wachezaji wa Taifa Stars hawakupewa mazoezi ya kuongeza pumzi na kupeana pasi za uhakika ndio sababu walipoteza mipira mingi. Mara nyingi badala ya kusukuma mashambulizi mbele, walirudisha mipira nyuma.
Sote tunafahamu kwamba Ivory Coast inaundwa na wachezaji karibu wote wanaocheza soka ya kulipwa barani Ulaya na wenye majina makubwa. Hivyo wachezaji wa Taifa Stars wakicheza kwa kuhofia majina hayo, wanaweza kupata matatizo. Lakini wakiwaona ni sawa kama wao, wanaweza kupata matokeo mazuri ugenini. Ni kweli kwamba Didier Drogba na Solomon Kalou wana uwezo mkubwa kwa kupiga chenga na kuwatoka mabeki wa timu pinzani, lakini ukiwabana kisawasawa, ni rahisi kuwadhibiti. Tatizo ni kwamba, ukiwapa nafasi moja tu, ni rahisi kwao kuitumia vizuri kupata bao.
Kitu kingine muhimu ni kwamba wachezaji wa Taifa Stars hawapaswi kuwa na papara wanapoingia kwenye lango la timu pinzani, hali inayosababisha wapoteze mipira mingi. Nina hakika kocha mwenzangu amelibaini tatizo hilo na atalifanyia kazi.
Cha msingi ni kwamba katika soka lolote linaweza kutokea. Kama wachezaji wa Taifa Stars watadhamiria kwa dhati kuishangaza dunia, hilo linaweza kutokea.
SWALI: Kwenye kikosi chako cha Malawi umejaza wachezaji wengi wanaocheza soka ya kulipwa nje. Unadhani hiyo ni njia nzuri ya kuiwezesha timu yako kufanya vizuri katika michuano hii?
JIBU: Nilichojaribu kukifanya ni kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa soka ya kimataifa kuliko kutegemea vijana pekee. Lakini asilimia kubwa ya wachezaji wangu ni vijana waliotapakaa katika nchi mbalimbali za kusini mwa Afrika, ambako wanacheza soka ya kulipwa.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu vipaji kwa wanasoka wa Tanzania? Unadhani vipo vipaji vya kutosha?
JIBU: Ndio. Ni kweli wachezaji wengi wa Tanzania wana vipaji vya kucheza soka, lakini tatizo kubwa ni kutojiamini na ndio sababu utaona kuwa, idadi ya wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka ya kulipwa nje ni ndogo ikilinganishwa na Malawi.

No comments:

Post a Comment