KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 18, 2012

CECAFA yafurahia Kombe la Kagame kuchezwa Dar


KATIBU Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye amesema baraza lake linafurahia zaidi michuano ya Kombe la Kagame inapofanyika katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti la East African Business Week mapema wiki hii, Musonye alisema wameamua mashindano ya mwaka huu yafanyike tena Tanzania kutokana na mafanikio yaliyopatikana mwaka jana.
Musonye alisema mashindano hayo na ya le ya Kombe la Chalenji yalikuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuhudhuriwa na mashabiki wengi.
Aliitaja sababu nyingine ya kuhamishia mashindano hayo Tanzania kuwa ni uhakika wa udhamini na mapato makubwa ya viingilio.
Mwaka jana mashindano hayo yalitakiwa kufanyika Zanzibar, lakini kwa sababu ya uukosefu wa fedha, yalihamishiwa Sudan, ambayo nayo ilishindwa kuyaandaa kutokana na matatizo ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Musonye, mapato ya viingilio yaliyopatikana katika mechi za mashindano hayo mwaka jana yalikuwa sh. bilioni 1.2 (dola 763,358 za Marekani).
Mashindano hayo yalikuwa na mvuto zaidi kuanzia hatua ya robo fainali, ambapo wenyeji Simba na Yanga walicheza na timu tofauti na mechi zao kuvunja rekodi ya kuhudhuriwa na mashabiki wengi.
Musonye alisema maandalizi kwa ajili ya mashindano ya mwaka huu yapo kwenye hatua za mwisho na yanatarajiwa kugharimu dola 600,000 (sh. milioni 944).
Mashindano ya mwaka jana yalidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Castle. TBL ilidhamini mashindano hayo kwa sh. milioni 300.
"Kwa sasa tunasubiri timu kuthibitisha ushiriki wao ili tuweze kupanga ratiba ya timu 12 zinazotarajiwa kushiriki mwaka huu," alisema Musonye.
Mashindano hayo yamekuwa yakidhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame tangu mwaka 2002. Kabla ya udhamini wa Kagame, mashindano hayo yalijulikana kwa jina la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na yalianzishwa mwaka 1974.
Timu zilizoshiriki mashindano ya mwaka jana ni Ulinzi (Kenya), Ports (Djibouti), St George (Ethiopia), El Merreikh (Sudan), Red Sea (Eritrea), Elman (Somalia), APR na Etincelles (Rwanda), Bunamwaya (Uganda), Vital'O (Burundi) na wenyeji Simba na Yanga za Tanzania Bara.
Mabingwa watetezi wa michunao hiyo ni Yanga iliyoifunga Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali.

No comments:

Post a Comment