KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 24, 2012

Azam kucheza Kombe la Kagame

WASHINDI wa pili katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, Azam wamepata nafasi ya kushiriki katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu.
Kuingizwa kwa Azam katika michuano hiyo, kutaifanya Tanzania Bara iwakilishwe na timu tatu. Zingine ni mabingwa watetezi Yanga na mabingwa wa ligi kuu, Simba.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, maandalizi ya michuano hiyo yanakwenda vizuri.
Angetile alisema kwa vile Yanga itashiriki michuano hiyo kama mabingwa watetezi, Tanzania Bara imepewa nafasi zingine mbili kutokana na kuwa mwenyeji.
Kwa mujibu wa Angetile, tayari wadhamini wa michuano hiyo wameshapatikana na wanatarajiwa kutangazwa hivi karibuni katika mkutano wa viongozi wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa mashindano hayo kuchezwa Dar es Salaam. Katika mashindano ya mwaka jana, Yanga ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali.
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alikaririwa wiki iliyopita akisema kuwa, baraza lake linafurahia mashindano hayo kuchezwa Dar es Salaam kutokana na wingi wa mashabiki na mapato makubwa.
Musonye alisema mashindano hayo na ya le ya Kombe la Chalenji yalikuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuhudhuriwa na mashabiki wengi, ikilinganishwa na yanapofanyika katika nchi zingine zinazounda CECAFA.
Mwaka jana mashindano hayo yalitakiwa kufanyika Zanzibar, lakini kwa sababu ya uukosefu wa fedha, yalihamishiwa Sudan, ambayo nayo ilishindwa kuyaandaa kutokana na matatizo ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Musonye, mapato ya viingilio yaliyopatikana katika mechi za mashindano hayo mwaka jana yalikuwa sh. bilioni 1.2 (dola 763,358 za Marekani).
Musonye alisema maandalizi kwa ajili ya mashindano ya mwaka huu yapo kwenye hatua za mwisho na yanatarajiwa kugharimu dola 600,000 (sh. milioni 944).
Mashindano ya mwaka jana yalidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Castle. TBL ilidhamini mashindano hayo kwa sh. milioni 300.

No comments:

Post a Comment