KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 24, 2012

NYAMWELA: Sina mpango wa kurudi tena Twanga Pepeta

MCHEZA shoo maarufu nchini, Hassan Mussa ‘Super Nyamwela’ amesema hana mpango wa kurejea katika bendi yake ya zamani ya Twanga Pepeta International.
Nyamwela amesema muziki kwa sasa ni kama mchezo wa soka hivyo msanii ama mwanamuziki anapaswa kufanyakazi kimkataba na kwa kuzingatia maslahi bora zaidi.
Dansa huyo machachari alisema hayo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Ten.
“Kusema ule ukweli, siwezi kurudi Twanga Pepeta, nipo Extra Bongo kimkataba,”alisema dansa huyo, ambaye pia ni mahiri kwa ubunifu wa minenguo mbalimbali.
“Muziki kwa sasa ni sawa na mchezo wa soka. Msimu ukiisha, unatafuta timu nyingine na kuingia nayo mkataba,”aliongeza msanii huyo.
Alisema kinachofanyika kwa sasa ni maelewano kati ya msanii na viongozi wa bendi na kwamba kinachozingatiwa ni maslahi kati ya pande zote mbili.
Dansa huyo alisema kubadili maisha ni jambo zuri kwa mtu yeyote na kuongeza kuwa, jambo la msingi la kuzingatia ni kutazama kipi bora kati ya umaarufu na kuwa na maisha mazuri.
Nyamwela alisema yeye ni tofauti na wacheza shoo wengi wa Bongo kwa sababu mbali ya kucheza stejini, anaimba, kurapu na kutunga nyimbo.
“Hadi sasa nimesharekodi albamu mbili na zipo sokoni. Hivyo usimuone mcheza shoo ukamdharau kwamba hana lolote. Wengine tunafanyakazi hii kwa malengo,”alisema.
Dansa huyo ametamba kuwa, anazo kila sababu za kujivunia kuwapika wacheza shoo wengi wa Bongo. Alisema katika wacheza shoo 100 wa Kibongo, asilimia 99 wamepitia kwake.
Nyamwela anao watoto wawili aliozaa na mkewe wa kwanza, Halima White, ambaye kwa sasa ni marehemu. Alisema kwa sasa, anajiandaa kuoa mke wa pili.
Msanii huyo alianza kujihusisha na muziki wa dansi mwaka 1990 kabla ya kuanzisha kundi lake lililokuwa likijulikana kwa jina la Billbums, ambalo lilikuwa likifanya maonyesho yake katika ukumbi wa Club Billicanas, Dar es Salaam.
Kundi hilo lilifanyakazi kwenye ukumbi huo kwa miaka mitano na lilikuwa na nguvu kuliko bendi za muziki wa dansi. Alisema akiwa katika kundi hilo, aliweza kujifunza vitu vingi kuhusu muziki, vikiwemo vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment