KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 18, 2012

HANNAH: Siwezi kutoa penzi ili nipate umaarufu


LAGOS, Nigeria
MSANII chipukizi wa filamu nchini Nigeria, Hannah Ojo amesema kamwe hawezi kutoa penzi kwa mtu yeyote ili aweze kupewa nafasi ya kucheza filamu.
Hannah, ambaye ana matumaini makubwa ya kuwa mwigizaji nyota wa Nollywood katika siku zijazo amesema, amewahi kushawishiwa kufanya hivyo mara kadhaa, lakini alikataa.
Akizungumza na mtandao wa naijerules wiki hii, Hannah alisema hataki kupata umaarufu kwa njia ya mkato.
Msanii huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema, anafahamu wazi kuwa, vitendo hivyo vimekuwa vikiwabeba wacheza filamu wengi wa kike wa Nigeria, lakini kwake haiwezekani.
“Unaweza kubaki ulipo, lakini haitakuwa milele. Kama wewe ni mwigizaji mzuri, hata kama unafanyakazi ndogo ndogo, kuna wakati utapata mafanikio kama watayarishaji na waongozaji filamu wataridhishwa na kazi zako,”alisema.
Hannah, ambaye ni mkazi wa jimbo la Ekiti alisema, amewahi kutoa pesa mara kadhaa ili apatiwe nafasi ya kucheza filamu, lakini baadhi ya watayarishaji wamekuwa wakimkatisha tamaa.
Alisema yupo tayari kuendelea kutoa pesa ili acheze filamu nyingi, lakini sio kupata nafasi hiyo kwa njia ya kutoa penzi.
Hannah, ambaye alijitosa kwenye fani hiyo mwaka 2005 alisema, baadhi ya wakati alikuwa akiombwa pesa ili asajiliwe kwenye baadhi ya kampuni za filamu, lakini mwisho wa siku alishtukia akitapeliwa.
“Unaweza kulipa pesa ili usajiliwe, lakini mwisho wa siku hakuna lolote wanalofanya. Watakupa maelezo ya filamu, unapoteza muda wako kuyasoma, kwenda mazoezini na mwisho wa siku hawatengenezi filamu yoyote. Unaweza kutumia wiki mbili kwa mazoezi, lakini pesa zako na nguvu zako zinapotea,”alisema binti huyo mrefu na mwenye sura jamali.
Kwa mujibu wa Hannah, tangu alipojitosa kwenye fani hiyo, amecheza filamu tatu na tamthilia kadhaa. Filamu alizocheza ni My Story, Wrong Passion, Edge of Paradise, Needle’s Eye, Burning Spear, Private Sector na Clinic Matters.
Hannah alisema ana hakika kwa uwezo wa Mungu, ipo siku atapata mafanikio makubwa kupitia fani hiyo na anaamini wakati wenyewe ndio sasa.
Alipoulizwa ni kitu gani chenye mvuto kwenye mwili wake, mwanadada huyo alisema ni sura, matiti na urefu wake.
“Kitu cha kwanza kinachowavutia wanaume kwangu ni matiti na nafikiri hata macho yangu nayo yanawavutia,”alisema.
Alipoulizwa iwapo atapewa nafasi ya kuwa mwigizaji mkuu katika filamu kwa sharti la kufanya mapenzi na mtayarishaji, Hannah alisema hayupo tayari kufanya hivyo kwa mtu yeyote.
“Siwezi kufanya hivyo kwa sababu hiyo haipaswi kuwa njia ya kupata mafanikio. Sikuwahi kufanya hivyo tangu nilipoanza uigizaji na kamwe sitathubutu kufanya hivyo,”alisisitiza.
Alipoulizwa iwapo anaweza kucheza picha za uchi, Hannah alisema kamwe hawezi kufanya kitu kama hicho, lakini alidokeza kuwa, anaweza kubusiana na mwanaume.
“Huwezi kuwa maarufu kwa kucheza filamu za uchi. Uigizaji ni kufanya kile unachokiweza. Unapaswa kuwa na viwango. Nawafahamu baadhi ya wasanii, ambao hawajawahi kucheza filamu za uchi, lakini wameweza kupata mafanikio makubwa,”alisema.
Matarajio makubwa ya Hannah ni kuwa mwigizaji maarufu nchini Nigeria. Amewataka watayarishaji wa filamu kumpa nafasi ili athibitishe uwezo wake.

No comments:

Post a Comment