KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 17, 2012

Rachel, nyota mpya ya THT


MSANII chipukizi wa kundi la Tanzania House of Talent (THT), Winfrida Josephat ‘Rachel’ amewataka wasanii wenzake wa muziki wa kizazi kipya kuacha kuwategemea wakongwe wanapotaka kutoka.
Rachel, mmoja wa wasanii wanaochipukia katika kundi hilo, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, msanii anayetaka kutoka, anapaswa kusimama mwenyewe.
Msanii huyo, ambaye kwa sasa anatamba na kibao chake cha Kizunguzungu, alisema msanii chipukizi anaweza kumshirikisha msanii mkongwe katika kurekodi nyimbo yake, lakini bado asiweze kutoka.
“Unatakiwa usimame wewe mwenyewe. Ningetaka kufanya hivyo, ningeweza kumshirikisha Barnaba au Linah, lakini nilitaka kutoka kivyangu,”alisema mwanadada huyo.
Rachel, ambaye anashabihiana kwa sura na umbo na msanii mkongwe wa fani hiyo, Rehema Chalamika ‘Ray C’ amesema, mafanikio aliyoyapata kimuziki katika kipindi kifupi yametokana na jitihada zake binafsi na pia kujiamini.
Alisema ili msanii aweze kupata mafanikio, anapaswa kufanyakazi zake kwa kujiamini yeye mwenyewe bila ya kutegemea msaada wa wasanii wakongwe.
Mwanadada huyo wasanii wa kundi la THT hupata nafasi za kurekodi nyimbo zao baada ya kupita kwenye hatua mbalimbali.
Akitoa mfano, Rachel alisema baada ya msanii kutunga wimbo wake, anapaswa kuupeleka kwa viongozi wa kundi hilo, ambao huupitia mmoja mmoja kabla ya kutoa maoni.
“Wimbo wa msanii kabla ya kuamriwa urekodiwe, unapitiwa na watu wengi na kila mmoja atatoa maoni yake. Yupo atakayesema ufanyiwe marekebisho, mwingine atasema haufai, mwingine atasema kiongezwe kitu fulani, hivyo ndivyo utaratibu ulivyo,”alisema.
Kwa mujibu wa Rachel, kwa sasa anajiandaa kurekodi nyimbo zake zingine kwa kushirikiana na kiongozi wa bendi ya Mashujaa, Charles Baba, Ray C na Barnaba.
Alisema ameamua kumshirikisha Ray C kwa sababu ndiye aliyemuahidi kufanya hivyo baada ya kumshuhudia katika mahojiano yake ya kwanza kupitia kwenye luninga.
“Ray C alinipa ahadi hiyo baada ya kuniona kwenye luninga. Hadi sasa tunaendelea kuwasiliana kwa simu, lakini kama unavyojua, mwenzangu ni mtu wa shughuli nyingi,”alisema.
Rachel alikiri kuwa, wimbo wake wa Kizunguzungu umetungwa na msanii mwenzake, Barnaba kwa vile bado hajaanza kutunga nyimbo zake mwenyewe.
Alikiri pia kuwa, kwa sasa amekuwa akipata pesa kutokana na kushirikishwa na baadhi ya wasanii wenzake wa THT kama vile Linah, Barnaba na Ditto kwenye maonyesho yao mbalimbali.
Alikanusha madai kuwa, amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Barnaba. Alisema amekuwa akimchukulia msanii huyo kama kaka yake kwa sababu ni mtu anayemuheshimu.
Rachel alisema kwa sasa anaye mchumba na anampenda kuliko kitu kingine chochote.
Binti huyo taanusi alisema alilazimika kuhama kutoka nyumbani kwa shangazi yake kwa vile alikuwa akimbana sana kiasi cha kumzuia kufanya mambo yake binafsi
Kwa sasa, watu wengine muhimu kwa Rachel ni viongozi wake wa THT na wasanii wenzake wa kundi hilo, hasa Barnaba, ambaye amemwelezea kuwa, amekuwa akimpa sapoti kubwa na kumpa moyo.
Rachel alizaliwa Februari 25, 1992 katika hospitali ya Maweni mkoani Kigoma. Alianza shule ya msingi mwaka 1998 katika shule ya msingi Muungano na baadaye sekondari ya Unit Commercial, zote za Dar es Salaam na kuishia kidato cha tatu kutokana na matatizo ya kifamilia.

No comments:

Post a Comment