KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 18, 2012

Tarimba amshukia Nchunga


BAADA ya kuwa kimya kwa muda mrefu, mwenyekiti na rais wa zamani wa klabu ya Yanga, Tarimba Abbas amesema kuongoza klabu kubwa kama hiyo hakuhitaji elimu pekee bali pia ujanja wa kimpira.
Tarimba amesema Yanga ni klabu kubwa na yenye wanachama wengi wenye matumaini tofauti, hivyo inapaswa kuwa na viongozi wenye mbinu tofauti za kimpira.
Amesema tatizo alilolibaini kwa viongozi wa sasa wa Yanga chini ya Mwenyekiti, Lloyd Nchunga ni kukosa mbinu za mpira, ambazo alisema ni muhimu katika kuongoza klabu kubwa kama hiyo.
Tarimba alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV kuhusu mgogoro uliozuka hivi karibuni Yanga kati ya uongozi na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga alisema, viongozi na wanachama wa klabu hiyo wanapaswa kujifunza kupitia kwa Simba, ambayo ilifanya vizuri katika michuano ya ligi kuu na Kombe la Shirikisho msimu huu.
“Tunapaswa kukaa chini na kujiuliza kwa nini tuliteleza na tufanye nini ili kurekebisha hali hiyo kwa sababu Yanga ni klabu kubwa,”alisema.
Aliipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu na kucheza vizuri katika mechi za mwanzo za Kombe la Shirikisho kabla ya kutolewa na Al-Ahly Shandy ya Sudan kwa mikwaju ya penalti mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kufanya vizuri kwa Simba katika michuano hiyo, hakukutokana na kuonyesha kiwango cha juu cha soka, bali pia utulivu uliopo sasa ndani ya klabu hiyo.
Tarimba alisema viongozi wa Yanga hawapaswi kukimbilia kufanya usajili wa wachezaji wapya hivi sasa, badala yake wakae chini na kutafakari walipokosea na kuchukua hatua za kurekebisha hali hiyo.
“Kama timu haishindi ama kufanya vizuri, lazima tujiulize ni kwa nini?”Alisema Tarimba, ambaye aliwahi kuwa katibu mipango wa Yanga mwaka 1991 hadi 1993, mwenyekiti kuanzia mwaka 1999 hadi 2001 na rais wa klabu hiyo kuanzia 2001 hadi 2004.
Aliongeza kuwa, Yanga imekuwa ikitumia fedha nyingi kila mwaka kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya kutoka nje ya nchi, lakini hawatumiki ipasavyo na wengine hukata tamaa mapema kutokana na kutotimiziwa mahitaji yao.
Alisema wachezaji wanapaswa kutengenezewa mazingira mazuri ya kazi, ikiwa ni pamoja na kulipwa mishahara na posho kwa wakati, kinyume na hivyo, morari yao inashuka.
“Unapocheza na timu isiyo na matatizo kama vile Simba au Azam, huwezi kufanikiwa hata siku moja na kuongezeka kwa Azam kwenye ligi, kumeongeza ushindani mkali, hivyo tunapaswa kuwa makini zaidi,”alisema.
Tarimba alikiri kuwa, kipigo cha mabao 5-0 walichokipata kutoka kwa watani wao wa jadi Simba katika mechi ya mwisho ya ligi, kimewaumiza wengi na pia kuipaka Yanga doa lisilofutika.
“Ubingwa tumeukosa, halafu tumefungwa mabao mengi, kwa kweli katika zama hizi, hilo halikubaliki. Ni bora tuukose ubingwa, lakini tumfunge mnyama,”alisema.
Tarimba alisema kipigo hicho kilitokana na mlolongo wa matatizo mengi yaliyojitokeza ndani ya Yanga katika siku za hivi karibuni, lakini alikiri kuwa, Simba ipo juu kisoka ikilinganishwa na Yanga.
Alisema pia kuwa, uongozi wa Yanga haukuwa umejitayarisha kupambana na timu kama Simba na kusisitiza kuwa, hilo ni kosa kubwa katika pambano linalozihusisha timu hizo kongwe nchini.
Alipoulizwa msimamo wake kuhusu uamuzi wa wazee wa Yanga kutaka kuchukua timu, Tarimba alisema huenda walifanya hivyo kutokana na kukerwa na malalamiko ya wachezaji kutolipwa mishahara kwa miezi kadhaa.
Alisema binafsi anaunga mkono uamuzi huo wa wazee, hasa kutokana na tukio lililotokea Arusha, ambako basi la Yanga lilizuiwa na uongozi wa hoteli moja ya mjini humo kutokana na kuwepo kwa deni kubwa.
“Kusema kweli wazee wanapaswa kuheshimiwa, japokuwa wakati mwingine wanaweza kutumia vibaya nafasi hiyo. Mimi nawaunga mkono kwa walichotaka kukifanya, lakini pengine busara ingetumika zaidi,”alisema.
Tarimba alisema uongozi wa Yanga ulipaswa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika maandalizi ya mechi yao dhidi ya Simba badala ya kufanya kila kitu peke yao.
“Wachezaji walikuwa na kila sababu ya kukosa ari kwa sababu hawajalipwa mishahara na posho zao za mechi kadhaa na hawakuwa na sababu ya kutaka kujua kama pesa zipo au hazipo. Wengine wanategemewa na familia zao, sasa usipowalipa, wanaweza kufanya lolote,” alitahadharisha.
Hata hivyo, Tarimba alieleza kukerwa na kauli za kupingana zilizokuwa zikitolewa hadharani baina ya Nchunga na wazee wa Yanga kwa madai kuwa, zilikuwa zikizidi kuchochea mgogoro.
Akizungumzia uamuzi wa Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kuipoka Yanga pointi tatu katika mechi yake dhidi ya Coastal Union kwa kosa la kumchezesha beki Nadir Haroub Cannavaro, alikiri kwamba ulikuwa sahihi.
Alisema tatizo lilikuwa kwa uongozi wa Yanga kumchezesha beki huyo, ilihali alikuwa na kadi nyekundu aliyopewa kwa kosa la kupigana. Alisema benchi la ufundi la Yanga linapaswa kuweka mtu maalumu kwa ajili ya kurekodi kadi za wachezaji.
Hata hivyo, Tarimba alisema hakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, iliyoamuru pambano kati ya Mtibwa Sugar na Azam lirudiwe.
Alisema kuziamuru Mtibwa na Azam zirudiane, lilikuwa kosa kubwa na ni maamuzi yaliyopitwa na wakati kwa sababu siku zote Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) linasisitiza maamuzi ya uwanjani yabaki kama yalivyo.
Tarimba alisema TFF ilipaswa kuwaadhibu waliosababisha pambano hilo kuvunjika na kuyaacha matokeo ya mechi ya awali yabaki kama yalivyokuwa.
Alisema ni vyema ufike wakati kamati ndogo ndogo za TFF zitoe maamuzi kwa kuongozwa na kanuni badala ya matakwa ya watu wachache.
Aliongeza kuwa, TFF pia inapaswa kufuata kanuni za kimataifa katika kuendesha soka badala ya kutunga kanuni zake, ambazo haziendani na soka ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment