KOCHA Mkuu wa Mafunzo, Hemed Suleiman Moroko amesema kipigo walichokipata kutoka kwa Mucumane de Maputo ya Msumbiji hakijafuta matumaini yao ya kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika.
Moroko amesema katika mechi hiyo iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, wachezaji wake walicheza vizuri lakini hawakuwa na bahati ya kufunga mabao.
Katika mechi hiyo iliyochezwa usiku na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, Mafunzo ilipigwa mweleka wa mabao 2-0.
Ili isonge mbele katika michuano hiyo, Mafunzo italazimika kuishinda Macumane mabao 3-0 katika mechi ya marudiano, inayotarajiwa kuchezwa wiki mbili zijazo mjini Maputo.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Moroko alisema ameshazisoma mbinu za wapinzani wao na kuongeza kuwa, atatumia uzoefu wake wote kuwapa mbinu wachezaji wake ili washinde mechi ya marudiano.
“Mimi siwezi kusema kwamba tumefungwa na hapa ndio mwisho wetu. Naamini tunaweza kufika mbali safari hii kwa sababu vijana wangu wamecheza vizuri,”alisema kocha huyo. Aliwataka mashabiki wa soka wa Zanzibar wasiwe na wasiwasi kuhusu hatma ya timu yao na kuongeza kuwa, wamepania kuushangaza umma wa Wazanzibar kwa kushinda ugenini.
Katika mechi hiyo, Mafunzo ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya nane wakati Jaku Juma alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Capo Venancio wa Mucumane.
Dakika nne baadaye, Mucumane ilipata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wake, Maciricio, aliyeruka hewani na kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Luis Pereira.
Bao hilo liliongeza msisimko wa mechi hiyo huku Mucumane wakishangiliwa na kikundi kidogo cha ngoma ya Sindimba kutoka Dunga, wilaya ya kati.
Mucumana iliongeza bao la pili dakika ya 21 kupitia kwa Manuel Mbalango baada ya kipa Suleiman Janabi kukosea hesabu wakati alipotoka langoni kwa lengo la kuokoa mpira.
Licha ya mabadiliko kadhaa ya wachezaji yaliyofanywa na Kocha Moroko katika vipindi vyote viwili, hayakuweza kuisaidia timu hiyo kupata bao.
Vijana wangu walikosa umakini-KochaKOCHA Mkuu wa Jamhuri, Renatus Shija amesema kufungwa kwa timu yake na Hwange ya Zimbabwe, kulitokana na wachezaji wake kukosa umakini na kuwa na woga.
Shija alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya Jamhuri kuchapwa mabao 3-0 na Hwange katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Gombani.
Kocha huyo alisema Hwange si timu ya kutisha, lakini walifanikiwa kutoka uwanjani kutokana na vijana wake kuanza mechi hiyo kwa woga.
“Vijana wangu walianza kutulia baada ya dakika 15 za kwanza kumalizika na walicheza vizuri zaidi katika kipindi cha pili,”alisema kocha huyo.
Shija alisema katika kipindi hicho, timu yake ilipata nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini walishindwa kuzitumia vyema kutokana na washambuliaji wake kuwa na papara na kupiga mashuti hafifu.
Kocha huyo alikiri kuwa, kipigo hicho kimewaweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele kwa vile watalazimika kushinda mechi ya marudiano wiki mbili zijazo kwa mabao 4-0.
Hata hivyo, alijipa moyo kwa kusema kuwa, katika soka lolote linaweza kutokea na kwamba, iwapo watapata mechi mbili ngumu za kujipima nguvu, wanaweza kufanya vizuri.
Alisema wasiwasi pekee alionao ni kuhusu hali ya hewa ya mji wa Hwange, ambao upo kilometa 770 kutoka Harare, ambao joto lake hupanda hadi kufikia nyuzi 40 hadi 45.
Shija alisema ameuomba uongozi wa Jamhuri kuitafutia mechi mbili za kujipima nguvu nje ya Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya marudiano. Alisema angependa zaidi mechi hiyo ichezwe Sudan kwa vile hali ya hewa ya huko inafanana na ya Zimbabwe.
Mwamuzi adaiwa kumdunda mchezajiKATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mwamuzi aliyekuwa akichezesha mechi ya mpira wa miguu katika michuano ya ligi daraja la pili wilaya ya kusini, anadaiwa kumpiga ngumi mchezaji, sambamba na kumuonyesha kadi nyekundu. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati timu za New Boys na Ranger Bulls za Mtende zilipokuwa zikimenyana katika uwanja wa Mwehe Makunduchi. Mwamuzi huyo, Baiye Maulid anadaiwa kumpiga ngumi mchezaji Khalid IddI Vuia wa New Boys muda mfupi baada ya kumuonyesha kadi nyekundu. Kufuatia kitendo hicho, uongozi wa New Boys umekiandikia barua Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wilaya ya kusini kumlalamikia mwamuzi huyo. Katibu wa New Boys, Mohamed Machanja alisema juzi kuwa, wameamua kukilalamikia chama hicho ili haki itendeke na kwamba wana matumaini ZFA haitapendelea upande wowote. Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, mwamuzi Baiye alikanusha kumpiga mchezaji huyo, akidai kuwa alichofanya ni kumsukuma kwa lengo la kujihami baada ya kumkamata sehemu nyeti za mwili wake. ''Si kweli kwamba nilimpiga. Nilichokifanya ni kujihami baada ya kunisogelea wakati nilipomuonyesha kadi nyekundu na alipofika karibu nami, akanikamata nyeti zangu,” alisema. Baiye alisema hawezi kusema mengi kuhusu tukio hilo kwa sababu ameshawasilisha ripoti yake katika ofisi za ZFA wilaya ya kusini na anachosubiri ni maamuzi yake.
Kwa upande wake, Khalid alikanusha kutaka kumdhuru mwamuzi huyo. Alisema alichokifanya ni kumsogelea kwa lengo la kumfahamisha jambo fulani.
ZFA yakiri waamuzi wanapokea rushwaCHAMA cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wilaya ya Kusini Unguja kimekiri kuwa, baadhi ya waamuzi wa mchezo huo wamekuwa wakijihusisha na upokeaji rushwa ili wachezeshe kwa upendeleo.
ZFA imesema vitendo hivyo hufanyika katika mechi mbalimbali za michuano ya ligi daraja la pili na la tatu katika wilaya hiyo.
Mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amesema, timu nyingi za wilaya hiyo zimeanza kuwasilisha malalamiko kuhusu vitendo hivyo.
Kiongozi huyo aliyezungumza na Burudani mwishoni mwa wiki iliyopita alisema, baadhi ya waamuzi wamekuwa wakipindisha sheria kwa makusudi baada ya kupokea rushwa.
“Ni vitendo vya kusikitisha sana kwa sababu baadhi ya waamuzi wamekuwa wakipindisha sheria baada ya kupewa rushwa na hivyo kuzipendelea baadhi ya timu,”alisema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, waamuzi wengine wamekuwa wakipindisha sheria baada ya kupewa magunia ya mkaa na samaki badala ya pesa taslimu.
Alisema chama chake kimekuwa kikitupiwa lawama nyingi kutokana na uchezeshaji mbovu wa waamuzi wakati hakihusiki kupanga matokeo ama kutoa maelekezo yoyote kwa waamuzi.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kwa sasa chake chake hakiwezi kuchukua hatua yoyote kwa waamuzi wanaolalamikiwa kwa vile hakina ushahidi wa kujihusisha kwao na vitendo hivyo.
“Suala hili linahitaji uchunguzi wa kina, ukilihusisha jeshi la polisi ili upatikane ushahidi wa kutosha. Hatuwezi kumuhukumu mwamuzi bila ya kuwa na ushahidi,”alisema.
Habari zote na Abood Mahmoud, Zanzibar