'
Wednesday, September 4, 2013
YANGA YAIPIGIA HESABU MBEYA CITY
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga wameanza kuipigia hesabu Mbeya City kabla ya kupambana nayo Septemba 14 mwaka huu mjini Mbeya.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kaziguto alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo imekuwa ikiendelea na mazoezi kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo.
Mbeya City ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda daraja msimu uliopita na ilianza ligi kuu msimu huu kwa kutoka suluhu na Kagera Sugar kabla ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1.
Kwa sasa, Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi nne baada ya kuibugiza Ashanti mabao 5-1 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union.
Kaziguto alisema Yanga inafanya mazoezi bila ya wachezaji wake Kevin Yondan na Athumani Iddi 'Chuji', ambao ni majeruhi.Wengine wanaokosekana kwenye kikosi hicho ni Ally Mustafa, David Luhende, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub na Simon Msuva.
Kwa mujibu wa Kaziguto, Kocha Ernie Brandts amekuwa akiyafanyiakazi makosa yaliyojitokeza katika mechi dhidi ya Coastal Union ili kuhakikisha kikosi chake kinakuwa imara kabla ya kuvaana na Mbeya City.
Katika mechi hiyo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake wa pembeni, Saimon Msuva kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Matin Saanya katika mechi dhidi ya Coastal Union.
Baada ya pambano lake dhidi ya Mbeya City, mabingwa hao watetezi watashuka tena dimbani Septemba 18 kumenyana na Prisons.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment