KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 15, 2013

LULU: NIMEZALIWA UPYA



MCHEZA filamu nyota wa kike nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' amesema tangu alipotoka jela, anajiona amezaliwa upya.

Lulu amesema kwa sasa amekuwa mtu mzima na mwenye majukumu ya kuielimisha jamii, tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Msanii huyo amesema kukua kwake kiakili na kimaisha ndiko kulikomfanya azindue filamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la Foolish Age. Filamu hiyo ilizunduliwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Mlimani City mjini Dar es Salaam.

Lulu, ambaye ni mwigizaji bora wa kike wa 2012/2013 kupitia tuzo za ZIFF, alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akihojiwa na mtandao wa filamucentral.

Msanii huyo aliachiwa kwa dhamana mapema mwaka huu na kubadilishiwa mashtaka ya tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba kuwa ya kuua bila kukusudia.

Lulu alisema anaishukuru Kampuni ya Proin Promotion, inayosimamia kazi zake
kwa kumpa nafasi ya kutoa mafunzo ya mambo aliyopitia kwa watu wengine kupitia fani ya filamu.

Alisema chanzo cha matatizo yaliyomkuta katika maisha ya utoto wake ni kutopenda kusikiliza ushauri na maonyo kutoka kwa wakubwa zake.

Binti huyo, ambaye hivi karibuni alitimiza rasmi umri wa miaka 18 alisema, amepitia mambo mengi katika maisha yake na kumpa usumbufu na mateso makubwa mama yake mzazi.

Alisema mkasa uliompata kwa marehemu Kanumba ni miongoni mwa sababu zilizomfanya aandae filamu ya Foolish Age, inayoelezea maisha yake alipokuwa na umri wa chini ya miaka 18.

"Nimetumia filamu hii kuwaelimisha vijana wenzangu kwamba wanapokuwa na umri kama wangu, wasipuuze ushauri kutoka kwa wakubwa zao,"alisema Lulu, ambaye kipaji chake kiliibuliwa na kundi la sanaa za maonyesho la Kaole.

“Sikumsikiliza mama yangu na wakubwa zangu. Nilikuwa gizani. Yale
niliyoyafanya niliamini kuwa ndio sahihi. Sikuweza kuona hatari iliyokuwa mbele
yangu.

" Lakini nahisi ulikuwa mpango wa Mungu kwa tukio lililonitokea. Watu
walinihukumu, lakini ukweli wa hili ni Mungu pekee anayeujua. Kwa sasa
nampenda Yesu, ninaomba na kusali. Nimekuwa Lulu mpya na ninataka
kuielimisha jamii  kupitia maisha yangu ya utoto,”alisema binti huyo
mantashau.

Lulu alisema asingependa kuzungumzia kilichotokea kati yake na marehemu Kanumba kwa sababu kesi aliyofunguliwa bado ipo mahakamani. Alisema amepania kufanyakazi kwa nguvu baada ya kuwa amejifunza mengi na hataki kurudi alikotoka.

Alisema anaishukuru kampuni ya Proin Promotion, inayosimamia kazi zake na kuongeza kuwa, hawezi kufanyakazi ya kucheza filamu nje ya kampuni hiyo.

Mama wa msanii huyo, Lukiresia Kagilla amesema alikuwa akipata shida na mateso makubwa kutokana na vitendo alivyokuwa akivifanya Lulu wakati wa utoto.

“Lulu alinitesa hadi nilikuwa napata shida na kuhaha, lakini
 nimejifunza kwake kwani mwanangu kabadilika na kuwa mtu mzima
 anayejua nini anafanya. Kumbe ilikuwa ni utoto tu," alisema mama huyo.

"Nami pia nimejifunza kutoka kwake, nilikuwa mkali sana na hiyo ilichangia Lulu
kuniogopa na kuwa mbali na mimi pale anapokosa. Wazazi inabidi tuongee na
watoto wetu kwa upole,”alisema mama huyo.

Alikiri kuwa kwa sasa Lulu ndiye mlezi wa familia yake na kwamba amekuwa akifaidika kutokana na mapato ya binti yake huyo, ambaye anamsomesha mdogo wake wa kike katika shule ya kimataifa kwa kumlipia ada na gharama zote muhimu.

"Mwenyewe anasema anafanya mpango wa kuendelea na shule kwani moja ya malengo yake ni kuwa mwigizaji wa kimataifa na kuitangaza Tanzania kupitia filamu, anaamini anaweza kufanya hilo kwa kwenda shule zaidi na anamuomba Mungu amsaidie,"alisema mama Lulu.

Kwa mujibu wa Lulu, baada ya kung'ara katika filamu ya Foolish Age, sasa
anajiandaa kutengeneza  filamu nyingine, itakayojulikana kwa jina la
Mapenzi ya Mungu.

Alisema katika filamu hiyo, amemshirikisha mama mzazi wa marehemu Kanumba,
Frola Mtegoa. Alisema filamu hiyo pia itazungumzia maisha na mikasa iliyowahi kumtokea katika maisha yake.

Msanii Mahsen Awadh 'Dr. Cheni' ndiye aliyeibua kipaji cha Lulu na kumkabidhi katika kundi la Kaole, ambako alicheza tamthilia kadhaa kama vile Tetemo, Jahazi, Dira, Tufani, Gharika na Baragumu.

No comments:

Post a Comment