BALI, Indonesia
MREMBO kutoka Philippines, Megan Young jana usiku alitawazwa kuwa mrembo wa 63 kutwaa taji la mrembo wa dunia, baada ya kuwabwaga washiriki wenzake 127 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Shindano hilo lililofanyika kwenye kisiwa cha Bali, liliwekewa ulinzi mkali kufuatia maandamano ya kulipinga yaliyofanywa na waislamu wenye msimamo mkali.
"Naahidi kuwa mrembo bora wa dunia, ambaye hajapata kutokea,"alisema Young (23) baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa taji hilo.
Kauli yake hiyo ilipokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki kutoka Ufilipino waliosafiri naye kwenda Bali, huku wakirukaruka kwa furaha na kupunga bendera za nchi hiyo hewani.
Licha ya kuwepo kwa tishio la kuvuruga mashindano hayo kutoka kundi la Waislamu wenye msimamo mkali, polisi walisema hakukuwa na maandamano yoyote yaliyofanyika jana.
Kwa wiki kadhaa, kundi hilo lilikuwa likiitaka serikali ifute mashindano hayo kwa sababu yanakwenda kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu.
Washiriki wanne walitolewa mapema kabla ya fainali ya shindano hilo kutokana na kuwa wagonjwa. Washiriki walipita stejini wakiwa wamevaa mavazi ya kutokea nyakati za usiku.
Young, ambaye ametwaa taji hilo kutoka kwa mshindi wa mwaka jana, Wenxia Yu kutoka China, alizaliwa Marekani. Alihamia Philippines akiwa na umri wa miaka 10. Amewahi kushiriki mara kadhaa kwenye vipindi vya televisheni vya nchi hiyo.
Mshindi wa pili wa taji hilo ni Marine Lorphelin (20) kutoka Ufaransa wakati Mghana, Carranzar Naa Okailey Shooter (22) alishika nafasi ya tatu.
No comments:
Post a Comment