KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 15, 2013

ALLY BUSHIRI: STARS INACHEZA SOKA YA ULAYA ILIYOTUSHINDA


KUTOLEWA mapema kwa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014, kumepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa michezo nchini. Kocha Msaidizi wa zamani wa timu hiyo, Ally Bushiri ni miongoni mwa, ambao kwa sasa hawafurahishwi na mwenendo wa timu hiyo hivi sasa. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kocha huyo anaelezea sababu za kuvurunda kwa timu hiyo.

SWALI: Kwa mara nyingine, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars imetolewa mapema katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014. Nini mtazamo wako kuhusu kufanya vibaya kwa timu hiyo katika michuano ya kimataifa?

JIBU: Zipo sababu nyingi, lakini kubwa ninayoiona kwa sasa ni kutoshirikishwa kwa wadau katika muundo unaofaa kutumika katika kuijenga timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
 
Kwa kipindi kirefu sasa, Taifa Stars imekuwa ikiundwa na wachezaji wengi kutoka timu za Yanga, Simba, Azam na Mtibwa, tofauti na miaka ya nyuma, ambako baadhi ya wachezaji nyota walitoka mikoani kwenye timu, ambazo hazikuwa na majina makubwa.

Binafsi naamini Tanzania inayo hazina ya wachezaji wengi wenye vipaji vya kucheza soka, lakini tatizo kubwa lililopo ni ufuatiliaji wa wachezaji hao na kuwaendeleza. Haiwezekani kwa timu ya Taifa kuundwa na wachezaji kutoka klabu nne tu kila mwaka. Huu ni utaratibu mbovu na hautatuwezesha kufika mbali.

SWALI: Nini kifanyike ili kuondokana na utaratibu huo, ambao umeuelezea kuwa ni mbovu?

JIBU: Nadhani mfumo unaotumika sasa katika uteuzi wa wachezaji wa timu hiyo unapaswa kubadilika. Wakati umefika kwa Kocha Kim Poulsen kuelezwa kwamba, uchezaji wa wachezaji wa Ulaya ni tofauti na wa hapa Tanzania.

Wachezaji wetu wanapenda kucheza mpira wa kasi na kupeana pasi fupi fupi, lakini Poulsen anataka wacheze mfumo wa Kiulaya wa kutumia nguvu, kitu ambacho kwa wachezaji wetu hakiwezekani.

Kiukweli wachezaji wetu wa sasa hawana nguvu kama ilivyokuwa kwa wachezaji wa zamani na hawana uwezo wa kucheza kwa kasi muda wote wa dakika 90. Udhaifu huu ndio umekuwa ukisababisha Taifa Stars ishindwe kufurukuta inapocheza na timu zingine kubwa za Afrika, japokuwa wakati mwingine imekuwa ikionyesha maajabu kama vile kuzifunga Morocco, Zambia na Cameroon.

SWALI: Kwa maana hiyo, unadhani kuna umuhimu kwa Taifa Stars kurudia mfumo wa Kibrazil, ambao wachezaji waliuzoea wakati timu ilipokuwa chini ya Marcio Maximo na wewe ukiwa msaidizi wake?

JIBU: Kwa mtazamo wangu,suala la mfumo linapaswa kuwa ajenda kubwa katika kujadili maendeleo ya timu hiyo. Tunapaswa kutafakari kwa makini ni mfumo upi unaoweza kuifaa timu yetu ya taifa badala ya kubadili mfumo mara kwa mara.

Inawezekana pia kuwa, benchi la ufundi la Taifa Stars halimpi ushirikiano wa kutosha Maximo ili aweze kujua hali halisi ya uchezaji wa soka hapa nchini. Hili ni jukumu la mkurugenzi wetu wa ufundi, Sunday Kayuni na wasaidizi wake. Vinginevyo hadithi itaendelea kuwa ile ile ya kutolewa mapema.

SWALI: Huoni kama wachezaji wetu nao wana matatizo?

JIBU: Hilo lipo kwa sababu baadhi ya wachezaji walioteuliwa kuunda timu hiyo, uwezo wake umeshuka, hawapaswi kuendelea kuwemo kwenye timu hiyo.

Tatizo lingine ni kwamba baadhi ya wachezaji wanaoteuliwa kuunda timu hiyo, hawana mapenzi ya dhati ya kuichezea Taifa Stars. Hawachezaji kwa kujituma kama wanavyofanya wanapokuwa kwenye klabu zao. Wachezaji wa aina hii wanapaswa kuondolewa kwa vile wanawavunja nguvu wenzao.

SWALI: Nini ushauri wako kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)?

JIBU: Naushauri uongozi wa TFF uwashirikishe wadau wake katika kujadili matatizo haya na kupanga mikakati ya kuyatatua. Ni vyema TFF ikutane na wachezaji wa zamani waliowahi kung'ara Taifa Stars ili kupata mawazo na ushauri wao.

Upo umuhimu mkubwa wa kuifanyia marekebisho makubwa timu hiyo, kuanzia katika uteuzi, mafunzo na saikolojia ili kuwafanya wachezaji wacheze kwa ari na kujituma badala ya ilivyo sasa. Binafsi nipo tayari kutoa mchango wangu wa mawazo iwapo nitahitajika.

Nimecheza soka kwa miaka mingi na kwa kiwango cha kimataifa, nimekuwa kocha katika klabu nyingi na hata Taifa Stars ilipokuwa chini ya Maximo, hivyo nina uzoefu wa kutosha.

Tunapaswa kuanza mageuzi haya mapema kwa sababu tunakabiliwa na mashindano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za 2015, hivyo hatupaswi kurudia makosa. Tunapaswa kusonga mbele.

Haiwezekani tuwe na mashindano mazuri ya Copa Coca Cola na Kombe la Uhai, lakini tunashindwa kuwa na timu nzuri ya taifa. Kuna wakati timu yetu ya Copa Coca Cola iliwahi kutwaa kombe la kimataifa kule Brazil, lakini wale vijana hawajulikani wako wapi?

SWALI: Nini mwito wako kwa serikali kuhusu maendeleo ya soka nchini?

JIBU: Kwanza naipongeza serikali yetu kwa kuwa mstari wa mbele katika kuinua viwango mbalimbali vya michezo nchini, hasa kuajiri makocha kutoka nje kuja kuzifundisha timu zetu za taifa.

Ushauri wangu kwa serikali ni kutoiachia TFF pekee usimamizi wa timu yetu ya taifa. Inapaswa kuwatumia wataalamu wake katika kuisimamia na kutoa ushauri wa kuiboresha timu hii ili kuondokana na hadithi ya 'kichwa cha mwendawazimu'.

No comments:

Post a Comment