'
Wednesday, September 4, 2013
BATULI: MAPEDESHEE WANAWAPA JEURI WAIGIZAJI WA KIKE
MCHEZA filamu machachari na mwenye mvuto, Yobnesh Yusuf 'Batuli'
amesema ugomvi unaotokea mara kwa mara kati ya wacheza filamu wa kike nchini unatokana na kugombea wanaume.
Batuli amesema wanaume hao, ambao ni maarufu zaidi kwa jina la 'Mapedeshee', ndio wamekuwa wakiwaweka mjini kwa kuwapangia nyumba za kuishi na kuwanunulia magari wanayotanua nayo mjini.
Mcheza filamu huyo aliamua kutoa siri hiyo hadharani wiki hii alipokuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu sababu ya kutokea kwa ugomvi wa mara kwa mara kati ya wachezaji filamu wa kike nchini.
"Chuki zinazojitokeza mara kwa mara kati yetu wasanii wa filamu wa kike ni kuchukuliana mabwana,"alisema Batuli.
"Ukiwa na mwanaume anayekusaidia, huwezi kabisa kumtambulisha kwa shoga yako kwa sababu ukimpa mgongo tu, huyo si wako tena,"aliongeza msanii huyo ambaye aling'ara katika filamu yake ya Ramadhan.
"Nazungumza hayo bila woga. Tunahitaji kuwa na maisha mazuri, lakini filamu hazilipi. Ukiona msanii anafanya kitu, lazima ujue nyuma yake kuna mtu na si kwa sababu ya malipo ya filamu, ni mapedeshee hao,"alisisitiza.
Batuli amewalaumu wasanii wenzake wa kike kwa kutokuwa wabunifu na kushindwa kutumia fursa wanazozipata kutoka sehemu mbalimbali kujiendeleza.
Alisema kuna wakati, mmoja wa wasanii nyota wa kike nchini alipata mwaliko wa kwenda kutembelea nchi jirani, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kutojiamini.
"Hakuna msanii wa kike anayeweza kusimama kama yeye zaidi ya kuwategemea 'mapedeshee' waliojificha nyuma yao,"alisema msanii huyo mwenye rangi ya kichotara.
Batuli amekiri kuwa, filamu yake ya Ramadhan, iliyosambazwa na Kampuni ya Leo Media, imemfundisha mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuishi kwa kufuata na kuheshimu mafunzo ya dini ya kiislam.
Alisema licha ya kuwa mtayarishaji na mwigizaji wa filamu hiyo, aliweza kujifunza mambo mengi kutoka kwa wasanii wenzake, ambayo hakuwa akiyafahamu.
"Nilikuwa sijui kwamba mwanaume haruhusiwi kuvaa vito vilivyotengenezwa kwa madini ya dhahabu mwilini mwake. Shehe mmoja alinipa mafunzo hayo, ambayo kwangu yalikuwa na faida kubwa,"alisema.
Aliyataja mafunzo mengine aliyoyapata kutokana na filamu hiyo kuwa ni uvaaji wa mavazi ya heshima kwa mwanamke wa kiislam, ambayo husitiri sehemu kubwa ya mwili wake.
"Filamu ya Ramadhan inapendeza kutazamwa wakati wowote, sio lazima mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa sababu inatukumbusha kufuata maadili mema,"alisema Batuli.
Mwigizaji huyo alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wakati anapokuwa akicheza filamu, hupatwa na tatizo la kupandisha maruhani, lakini haelewi ni kwa nini.
Batuli alisema hali hiyo inamkosesha raha kwa sababu haelewi chanzo cha tatizo hilo ni nini.
"Sipendi kumuhisi mtu vibaya, lakini nimekuwa nikijiuliza kwa nini niwe nikipandisha maruhani wakati wa kurekodi filamu? Kwa nini yasipande wakati mwingine?" Alihoji mwanadada huyo.
Alisema kuna wakati aliwahi kwenda hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kuhusu tatizo hilo, lakini hakuna kilichoonekana.
"Ni tatizo linalonitisha kwa sababu nikienda hospitali, halionekani. Namuomba Mungu anisaidie,"alisema.
Wasanii wengine walioshiriki kucheza filamu hiyo ni Haji Adam ‘Baba Haji’, Othman Njaidi ‘Patrick’ na Adam Melele ‘Swebe Santana’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment