KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 19, 2013

YANGA MAJANGA





Na Solomon Mwansele, Mbeya

MAMBO bado si shwari kwa Yanga baada ya kuendelea kubanwa katika mechi za ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara.

Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu, jana walilazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini hapa.

Sare hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Yanga baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kulazimishwa kutoka sare hiyo ya mabao na Mbeya City kwenye uwanja huo.

Kwa matokeo hayo, Yanga imeambulia pointi sita katika mechi nne ilizocheza, ikiwa imefungana na timu za Azam, Coastal Union na Mbeya City. Prisons ni ya pili kutoka mwisho ikiwa imeambulia pointi mbili.

Yanga ilihesabu bao la kuongoza dakika ya 41 lililofungwa na Jerry Tegete, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa krosi maridadi iliyopigwa na  Simon Msuva kutoka pembeni ya uwanja.

Bao la kusawazisha la Prisons lilifungwa na Peter Michael dakika ya 77 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Omega Seme.

Pambano hilo lilihudhuriwa na mashabiki wachache, tofauti na siku Yanga ilipocheza na Mbeya City na timu hizo kutoka sare mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika dakika 30 za kwanza, timu zote mbili zilicheza kwa kasi ndogo huku zikisomana na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Prisons ilipata nafasi nzuri ya kusawazisha dakika ya 48 baada ya Six Ally kuwatoka mabeki wa Yanga na kufumua shuti kali, lakini lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Ally Mustapha.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Athumani Iddi, Simon Msuva/ Nizar Khalfan, Salum Telela/Frank Dumayo, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete/Saidi Bahanuzi, Haruna Niyonzima.

Prisons:Benno David, Salum Kimenya, Mika Shaban, Jumanne Elfadhili, Nurdin Issah, Lugano Mwangama, Jimmy Shoji, Freddy Chudu, Ibrahim Issaka, Six Ally/Peter Michael na Jeremiah Juma/ Omega Seme.

Wakati huo huo, JKT Ruvu jana ilishushwa kileleni mwa ligi hiyo baada ya kupigwa mweleka wa bao 1-0 na ndugu zao wa Ruvu Shooting katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Azam imeendelea kuchechemea katika ligi hiyo baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Ashanti katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kipre Tchetche aliifungia Azam bao la kuongoza kipindi cha kwanza kabla ya Anthony Matangalu kuisawazishia Ashanti kipindi cha pili.

Azam ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki  wake, Aggrey Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kucheza rafu mbaya.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union ilitoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga wakati Mtibwa Sugar ilitoka suluhu na Mbeya City kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani Morogoro.

No comments:

Post a Comment