'
Sunday, September 22, 2013
SIMBA YATOLEWA NISHAI NA MBEYA CITY, LEO NI YANGA NA AZAM
KIUNGO Amri Kiemba wa Simba akiwatoka mabeki wa Mbeya City wakati timu hizo zilipomenyana jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog)
VIJANA wa Mbeya City jana walidhihirisha kwamba hawakupanda daraja la ligi kuu kwa kubahatisha baada ya kuilazimisha Simba kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa mbele kwa mabao 2-1 hadi mapumziko, kabla ya vijana wa Mbeya City kuchachamaa na kusawazisha kipindi cha pili.
Kwa matokeo hayo, Simba bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano wakati Mbeya City imefikisha pointi saba.
Mshambuliaji Hamisi Tambwe kutoka Burundi aliendelea kung'ara na kuongoza kwa ufungaji mabao baada ya kuifungia Simba mabao yote mawili. Alifunga mabao hayo dakika ya 29 na 33.
Mbeya City, inayofundishwa na kocha mzoefu, Juma Mwambusi, ilipata bao la kwanza dakika ya 37 kupitia kwa Paul Nonga kabla ya Richard Peter kusawazisha dakika ya 69 na kuwaacha mashabiki wa Simba wakiwa wameduwaa.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, mabao ya Mbeya City yalionekana kuwa ya ufundi zaidi, hasa bao la pili, ambalo lilifungwa kwa mpira wa adhabu, ambao Richard alitanguliziwa kwa mbele na kuunganisha kwa shuti.
SimbaAbbel Dhaira , William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kaze Gilbert/Hassan Hatibu dk66, Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk50, Amri Kiemba/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk79, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo.
Mbeya City:Dvid Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Antony Matogolo, Yohana Morris, Mwagane Yeya/Richard Peter dk59, Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke na Yussuf Willson.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mgambo JKT ilitoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers mjini Tanga, Prisons ilitoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar mjini Mbeya wakati Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ashanti.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo wakati Azam itakapomenyana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, JKT Ruvu itacheza na JKT Oljoro kwenye uwanja wa Azam Complex wakati Ruvu Shooting itavaana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment