KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 15, 2013

SIMBA YANGURUMA, YANGA, AZAM ZABANWA


MSHAMBULIAJI Haruna Shamte wa Simba akiruka juu kukwepa kwanja la beki Hassan Ramadhani timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana walilazimishwa sare ya bao 1-1 na watoto wa mjini, Mbeya City katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Wakati Yanga walilazimishwa sare, watani wao wa jadi Simba waliendelea kung'ara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya Yanga na Mbeya City lilikuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote mbili kucheza soka ya kuvutia, kushambuliana kwa zamu na kuwa na uchu wa kufunga mabao. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 50 lililofungwa na Mwigane Yeya baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya.

Bao la kusawazisha la Yanga lilifungwa na Didier Kavumbagu dakika ya 71 alipounganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo.

Kwa upande wa Simba, mabao yake yalifungwa na Henry Joseph na Betram Mombeki dakika ya 67 na 89.

Wakati huo huo, Azam jana iliendelea kubanwa katika ligi hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kagera ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Themi Felix dakika ya 25 kabla ya Khamis Mcha kuisawazishia Azam dakika ya 55.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union ilitoka suluhu na Prisons mjini Tanga wakati Rhino Rangers ilitoka sare ya bao 1-1 na JKT Oljoro mjini Arusha.

No comments:

Post a Comment