KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, September 7, 2013

YANGA YAFAFANUA UJIO WA NAGGI


Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga
Patrick Naggi, mkenya aliyezua kizaazaa Yanga

Hatimaye uongozi wa Yanga umetangaza rasmi kumtambua Mkenya, Patrick Naggi, ambaye alijitambulishwa kwa wanachama wa klabu hiyo kwamba ni katibu mkuu mpya wa kuajiriwa.

Hata hivyo, Yanga imesema si kweli kwamba Naggi ni katibu mkuu mpya bali ni miongoni mwa watu watatu waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam juzi kuhusu ujio wa Mkenya huyo.

Sanga alisema uongozi wa Yanga unamtambua Naggi, lakini si kama katibu mkuu mpya. Alisema kwa sasa klabu ipo kwenye mchakato wa kumpata katibu mkuu mpya, kazi ambayo inafanywa na kampuni moja ya Jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo wa Yanga alisema, Naggi alikwenda makao makuu ya Yanga kutembelea mazingira na hakukuwa na ubaya kwake kufanya hivyo, lakini wanachama walitafsiri vibaya.

"Binafsi sioni kama alichokifanya Naggi kilikuwa kibaya. Yeye ni miongoni mwa watu kadhaa, ambao wamo kwenye mchakato wa kutaka ajira ya katibu mkuu, kutembelea mahali ambako huenda ukafanyakazi si vibaya,"alisema.

Sanga alisema kamati ya utendaji ya Yanga imetoa baraka ya kuboresha sekretarieti nzima, ikiwa ni pamoja na kuajiri katibu mkuu mpya kwa lengo zima la kujitegemea.

"Lengo letu ni kuwa na sekretarieti bora yenye watendaji wenye sifa na ari ya kuiendeleza Yanga. Kwa sababu hiuyo, tumeipa kazi kampuni moja ya Dar es Salaam, itusaidie kuwapata watendaji wenye sifa zinazokubalika,"alisema.

Sanga hakutaka kutaja jina la kampuni hiyo, lakini alisema itakapomaliza kaziyake, itawasilisha majina ili taratibu zingine zifuatwe kabla ya kumpata mwenye sifa na kupewa nafasi hiyo.

Amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wawe watulivu katika kipindi hiki uongozi ukiendelea na taratibu za kumpata katibu mkuu mpya.

Alisema kwa sasa, kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako ataendelea kushikilia wadhifa huo hadi katibu mkuu mpya atakapopatikana.

Alipoulizwa kuhusu katiba ya Yanga kutaka mfanyakazi wa klabu hiyo kuwa mwanachama, Sanga alisema dunia inabadilika na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kumhitaji mtendaji bora asiye mwanachama.

Hata hivyo, Sanga alisema iwapo Naggi atakidhi sifa za kushika nafasi hiyo, atapewa kadi ya uanachama wa Yanga.

"Wakati umefika watu waweze kubadilika kwa kuzingatia zaidi taaluma ya mtu. Tusipokuwa makini, tunaweza kukosa watendaji wazuri kwa kisingizio cha uanachama. Tutakuwa makini kuhakikisha kuwa, mamluki hawapati nafasi ya uongozi ndani ya Yanga,"alisisitiza.

No comments:

Post a Comment