KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, September 3, 2013

RUKWA YAIBONDA KATAVI 4-0 COPA COCA COLA



Rukwa imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya leo kuichapa Katavi mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga jijini Mbeya.

Mabao ya washindi yalitiwa wavuni na Tumaini Boniface dakika ya 13 na 65, Francisco Mkanga akipachika la pili dakika ya 29 wakati la mwisho lilifungwa dakika ya 75 na Innocent Ahombile.

Katika kituo cha Zanzibar, wenyeji Mjini Magharibi imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kaskazini Pemba kwa mabao ya Faisal Salum na Masoud Mohamed.

Mechi ya pili katika kituo hicho ilikuwa kati ya Kusini Pemba na Kusini Unguja. Bao pekee lililofungwa na Othman Abdallah lilitosha kuipa ushindi wa 1-0 timu ya Kusini Pemba.

Iringa imeanza kwa kishindo michuano ya Copa Coca-Cola kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 baada ya leo (Septemba 3 mwaka huu) kuitandika Ruvuma mabao 4-0.

Hadi mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga jijini Mbeya, washindi walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa dakika ya 14 na Justin Luvanda huku Alphonce Kalinga akifunga la pili dakika ya 43.

Mabao mengine yalifungwa na Juma Rogani katika dakika ya 49 na Luvanda akafumania tena nyavu dakika ya 59.

Hiyo ni mechi ya pili mfululizo kwa Ruvuma kupoteza ambapo ya kwanza ililala mbele ya wenyeji Mbeya kwa mabao 3-0.

No comments:

Post a Comment