'
Tuesday, September 3, 2013
40 WAPITISHWA KUGOMBEA TFF, BODI YA LIGI
Kamati ya Uchaguzi imepitisha majina ya waombaji 40 kati ya 58 kwa ajili ya uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utakaofanyika mwezi ujao.
Waliopitishwa katika orodha hiyo ya awali kwa upande wa Bodi ya Ligi ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti).
Kwa upande wa Kamati ya Uendeshaji (Management Committee) ni Kazimoto Miraji Muzo na Omar Khatib Mwindadi. Walioondolewa kwa vile si wenyeviti wa klabu za daraja la kwanza kama kanuni zinavyotaka ni Michael Njuweni Kaijage, Salum Seif Rupia na Silas Masui Magunguma.
Kanda namba moja (Kagera na Geita) aliyepitishwa kuwania nafasi ya ujumbe Kamati ya Utendaji ya TFF ni Kaliro Samson wakati Abdallah Hussein Musa ameondolewa kwa kutojaza fomu ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
Jumbe Oddessa Magati, Mugisha Galibona na Vedastus Lufano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba mbili (Mara na Mwanza). Samwel Nyalla ameondolewa kwa kutojaza kikamilifu fomu namba 1 ya maombi ya kugombea uongozi wa TFF kwa kutoonesha malengo yake.
Waliopitishwa katika Kanda namba tatu (Shinyanga na Simiyu) ni Epaphra Swain a Mbasha Matutu wakati Stanslaus Nyongo ameondolewa kwa kukosa sifa ya uongozi wa angalau uzoefu wa miaka mitano kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.
Kanda namba nne (Arusha na Manyara) wamepitishwa wote watatu; ambao ni Ali Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omar Walii Ali. Kanda namba tano (Tabora na Kigoma) nao wamepitishwa wote; Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamis Kitumbo.
Blassy Kiondo amepitishwa peke yake kuwania ujumbe Kanda namba sita (Katavi na Rukwa) huku Ayoub Nyaulingo aliondolewa kwa kutokuwa na uzoefu uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
Naye Nazarius Kilungeja, Kamati ilikataa maombi yake ya kugombea ujumbe kutokana na vitendo vyake visivyo vya kimichezo ambavyo kwa kiasi kikubwa vilisababisha migogoro kwenye Mkoa wa Rukwa, hivyo suala lake litawasilishwa kwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Kanda namba saba (Iringa na Mbeya) waliopitishwa ni David Samson Lugenge, John Exavery Kiteve na Lusekelo Elias Mwanjala. Cyprian Kuyava hakupitishwa kwa vile hana uzoefu wa uongozi kwa mujibu wa Katiba ya TFF huku Ayoub Shaib Nyenzi akiondolewa kwa kushindwa kuthibitisha uraia wake.
Elliud Peter Mvella ameondolewa kwa kushindwa kuheshimu Kanuni za Uwajibikaji wa Pamoja (collective responsibility) baada ya kushiriki kufanya uamuzi ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF bila ya kutaka msimamo wake wa kupinga uwekwe kwenye muhtasari na baadaye kuupinga uamuzi huo akiwa kwenye uongozi wa mkoa. Suala lake limewasilishwa katika Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Waliopitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba nane (Njombe na Ruvuma) ni James Patrick Mhagama na Stanley William Lugenge wakati Kamanga Tambwe ameondolewa kwa vile alipatikana na hatia ya kushiriki kwenye tuhumu za rushwa kwa waamuzi na kufungiwa na TFF.
Kanda namba tisa (Lindi na Mtwara) waombaji wote watatu wameptishwa. Waombaji hao ni Athuman Kingome Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Pia waombaji wote wa Kanda namba kumi (Dodoma na Singida), Hussein Zuberi Mwamba, Stewart Ernest Masima na Charles Komba wamepitishwa.
Waombaji wanne kati ya watano wamepitishwa kwa Kanda namba 11 (Morogoro na Pwani). Waliopitishwa ni Farid Mbarak, Geofrey Nyange, Juma Abbas Pinto na Twahil Twaha Njoki.
Riziki Juma Majala ameondolewa kwa vile akiwa mtendaji mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) alishindwa kusimamia Kanuni za Ligi kwa kuruhusu timu ambayo si mwanachama wa wanachama wa COREFA kucheza ligi, hivyo kusababisha mgogoro mkubwa kiasi cha mwananchi mmoja kufungua kesi ya kusimamisha Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL). Suala lake litawasilishwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Kanda namba 12 (Kilimanjaro na Tanga) wamepitishwa waombaji wote wawili. Waombaji hao ni Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed. Waombaji wawili kati ya watano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba 13 (Dar es Salaam).
Wagombea wawili kati ya watano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba 13 (Dar es Salaam). Wagombea hao ni Alex Crispine Kamuzelya na Muhsin Said Balhabou.
Walioondolewa ni Omar Isaack Abdulkadir kutokana na vitendo vyake vya kutoheshimu na kutotekeleza maagizo ya TFF kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF. Atapelekwa katika Kamati ya Maadili kwa hatua zaidi.
Shaffii Kajuna Dauda ameondolewa kwa kutumia nyaraka ya mawasiliano baina ya FIFA na Rais wa TFF bila idhini na kuiweka hadharani kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, hivyo kukiuka maadili kwa kumiliki nyaraka ambazo hazikuwa kwenye mamlaka yake. Suala lake linapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Naye Wilfred Kidao ameondolewa kwa kutumia nyaraka za Kamati ya Utendaji ya TFF bila ridhaa ya kamati, hivyo kukosa uadilifu. Suala lake linawasilishwa kwenye Kamati ya Maadili kwa hatua zaidi.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu wa Rais, waombaji wote watatu wamepitishwa. Waombaji hao ni Imani Omari Madega, Ramadhan Omari Nassib na Wallace John Karia.
Athuman Jumanne Nyamlani na Jamal Emil Malinzi wamepitishwa kuwania nafasi ya Rais. Omari Mussa Nkwaruro ameondolewa kwa kuwasilisha cheti chenye utata, hivyo kukiuka utashi wa Ibara ya 27(7) ya Katiba ya TFF. Pia aliwasilisha taarifa za uongo kuhusu uzoefu na kukiuka Kanuni za Maadili, hivyo suala lake linapelekwa Kamati ya Maadili.
Naye Richard Julius Rukambula ameondolewa kwa hakukidhi matakwa ya kugombea uongozi kwa mujibu wa Ibara ya 12(2)(e) ya Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kupelekwa katika mahakama za kawaida. Hivyo naye anapelekwa katika Kamati ya Maadili kwa hatua stahiki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment