KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 8, 2013

HAKUNA TATIZO SIMBA, HALI SHWARI


“LEO, Jumapili, Septemba 8, 2013, magazeti na vyombo vingine vya habari vimeripoti taarifa kwamba hali ndani ya klabu ya Simba si shwari. Sababu zilizotolewa ni kutoingia kambini kwa baadhi ya wachezaji, ‘kutoweka’ kwa wachezaji waliokwenda nchini Uganda na ubaguzi wa wazi unaofanywa na kocha Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo (Julio).
Klabu ya Simba imesikitishwa sana na habari zote hizo. Hizi ni habari ambazo zimeandikwa kwa lengo la kuibua migogoro isiyokuwepo. Na hata pale ambapo waandishi wamepata fursa ya kupata maelezo kutoka kwa wahusika, bado wameandika taarifa za kuonyesha migogoro.

Simba inaomba kutoa ufafanuzi kuhusu masuala machache.

 Klabu ya Simba kwa sasa ina wachezaji 49. Kati ya hao, wachezaji 29 wako katika kikosi cha kwanza na 20 ni wa kikosi cha pili maarufu kwa jina la Simba B.

 Kutokana na uwezo mkubwa wanaouonyesha, baadhi ya wachezaji walio katika kikosi cha pili, wameweza kupata namba katika kikosi cha kwanza mfano akiwa Saidi Ndemla, ambaye juzi tu alifunga bao la kwanza kwenye mechi dhidi ya KMKM.

Asilimia kubwa ya wachezaji hao 49 walisafiri, kufanya mazoezi na kucheza mechi kwa takribani miezi miwili chini ya Kibadeni na Julio, wakati timu ikijiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania.
Lakini sasa, benchi la ufundi limepata kikosi ambacho linadhani linaweza kufanya nacho kazi. Na haya ni maamuzi ya kiufundi.

Kuingia kambini katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa, benchi la ufundi limechagua wachezaji takribani 26.  Wachezaji 20 wameingia kambini jana na sita wengine (wanne walio katika timu ya Taifa Stars na wawili; Joseph Owino na Abel Dhaira- wenye ruhusa kwenda Uganda) watajiunga kuanzia kesho.

Ni kawaida kwa makocha kufanya mazoezi na idadi maalumu ya wachezaji inaowataka. Kwa mfano tu, Jose Mourinho wa Chelsea ya England, hupenda kufanya kazi na wachezaji 24 tu. Kibadeni ameamua kuwa na 26 tu.

Simba haiwezi kuingiza kambini wachezaji 49 kwa kipindi hiki ambapo mashindano yameanza. Kuna sababu kubwa mbili. Mosi, kiufundi, kwani mwalimu hawezi kufanya kazi na wachezaji wote hao kwani mechi zinahitaji maandalizi maalumu na uelewa wa kutosha wa kutosha wa wachezaji na mbinu zinazotumika.

Pili, kiuchumi, ni gharama kubwa sana kuingiza kambini wachezaji wote hao. Kwenye mechi moja, wachezaji 11 tu ndiyo wanaotumika. Watatu wanakuwa wa akiba. Hivyo, timu haihitaji wachezaji zaidi ya 14 kwa mechi moja. Ni wazi wachezaji hata 30 tu ni wengi sana katika mazingira haya.
Msimu uliopita, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig, aliamua kutumia wachezaji aliowataka kwenye mazoezi yake na uongozi ukamuunga mkono hata kama baadhi ya wapenzi na wanachama hawakumuunga mkono kwa vile wengi wa wachezaji waliokuwa wakiachwa walikuwa maarufu.

Ni sera ya uongozi wa Simba, chini ya Mwenyekiti, Mhe; Ismail Aden Rage, kwamba maamuzi yote ya benchi la ufundi yataheshimiwa na uongozi hautaingilia. Kama ambavyo haukumuingilia Liewig mwaka jana, uongozi pia hauna nia ya kuingilia maamuzi ya Kibadeni.

Tuhuma dhidi ya benchi la ufundi kwamba linaigawa timu hazina mashiko. Wachezaji waliofanya vizuri zaidi kwenye mazoezi na mechi za kirafiki chini ya Kibadeni ndiyo haohao wameingia kambini. Wale ambao hawajaingia kambini wataendelea na mazoezi na wataitwa kambini au kwenye mechi wakati Kibadeni atakapoona inafaa.

Klabu ya Simba ingeomba vyombo vya habari viripoti matukio kwa ukweli wake na si kwa ajenda binafsi dhidi ya uongozi huu, benchi la ufundi au wachezaji fulani.

Kuandika habari kuhusu migogoro wakati ambapo haipo hakusaidii kukuza michezo yote. Migogoro ya kila siku imekuwa chanzo cha kuzorota kwa michezo hapa nchini. Ni vema kama vyombo vingeamua kuripoti kwa dhati kuhusu migogoro kama ipo lakini Simba SC hailewi ni kwa vipi vyombo vinashiriki katika kuleta machafuko ambayo hayapo.

Vyombo vya habari vina kazi kubwa tatu muhimu; Kuelimisha, Kuburudisha na Kufundisha… Kuleta migogoro si miongoni mwa dhima zake na tungeomba sana kwamba weledi utazamwe sana kwenye mambo haya.

Owino na Dhaira
Kuna vyombo vimeandika kwamba wachezaji hawa wametoweka kambini. Lakini gazeti moja limekwenda mbali na kufanya mahojiano na Kibadeni. Kocha akawaambia wachezaji hao waliaga na wamepewa ruhusa. Lakini gazeti hilohilo limeona inafaa kuandika wachezaji hao.

WAMETOWEKA !
Kutoweka gani huku ambako watu wanaaga na kupewa ruhusa?
Owino na Dhaira wana matatizo yao binafsi na waliomba ruhusa  wakapewa. Wote wanarejea wiki inayoanza kesho. Ni sera ya uongozi huu kujali hali za wachezaji na mahitaji yao. Na ndiyo maana tumeamua kumruhusu mchezaji wetu tegemeo, Shomari Kapombe, abaki Ufaransa bila ya klabu kupewa chochote, kwa vile mchezaji atanufaika sana na mkabata huo.

Na uongozi huu hautasita kuweka mbele maslahi na mahitaji ya wachezaji wake mbele. Habari hiyo pia ni uthibitisho mwingine kuhusu agenda ya siri dhidi ya SIMBA SC inayoendelea.
Itoshe tu kusema kwamba SIMBA SC ina imani kubwa sana na vyombo vya habari vya Tanzania ambavyo vimefanya kazi kubwa sana kuufikisha mchezo wa mpira wa miguu hapa ulipo hivi sasa. Uongozi wa Simba SC unaahidi kwamba utaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari kwa kadri itakavyowezekana,”.
“Imetolewa na Ezekiel Kamwaga,
Ofisa Habari Simba SC,”.

No comments:

Post a Comment