KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 29, 2013

NGASA AREJESHA NEEMA YANGA



BAO lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza jana liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa pili katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kiiza alifunga bao hilo baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ngasa kuichezea Yanga msimu huu baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa kucheza mechi sita na kutozwa faini ya sh. milioni 45.

Ngasa alipewa adhabu hiyo baada ya kubainika kuwa, aliingia mkataba na Simba na kulipwa sh. milioni 30. Alitakiwa kulipa sh. milioni zingine 15 kama riba.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mbeya City ilitoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Coastal walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya saba kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ kabla ya Mbeya kusawazisha kupitia kwa Mwagane ‘Morgan’ Yeya dakika ya 70.

Katika mchezo huo, Richard Peter wa Mbeya City na Markus Ndeheli na Haruna Moshi wa Coastal walipewa kadi nyekundu.

Rhino Rangers ya Tabora ilipata kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

No comments:

Post a Comment