KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 25, 2013

KAMWAGA, KINDA WA AZAM ALIYEIZAMISHA YANGA



JINA la Joseph Kamwaga ni geni kwa mashabiki wa soka nchini. Ni mmoja wa wachezaji chipukizi wa Azam waliopandishwa kikosi cha kwanza msimu huu, akitokea kikosi cha pili.

Kabla ya mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Azam na Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kamwaga hakuwa akifahamika. Ni kwa sababu hakuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Lakini baada ya kucheza mechi hiyo, Kamwaga sasa amekuwa maarufu kutokana na kuifungia Azam bao la tatu na la ushindi dhidi ya Yanga na kuiwezesha kutoka uwanjani na ushindi wa mabao 3-2.

Kamwaga aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya kinda mwingine wa timu hiyo, Farid Musa na dakika chache baadaye akafanikiwa kuzitikisa nyavu za Yanga na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo.

Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa kipa Aishi Manula, ambaye baada ya kuokoa bao, alirusha mpira mrefu kwa Kamwaga, akawazidi mbio mabeki wa Yanga na kufumua kiki iliyompita kipa Ally Mustapha 'Barthezl na kujaa wavuni.

Kamwaga na Farid walichezeshwa mechi hiyo kwa mara ya kwanza na Kocha Stewart Hall wa Azam kutokana na shinikizo la wakurugenzi wa klabu hiyo baada ya baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kucheza chini ya kiwango.

Katika mechi hiyo dhidi ya Yanga, Stewart aliamua kuwaweka benchi kiungo Salum Abubakar na mshambuliaji Khamis Mcha kutokana na kucheza kwa kiwango cha chini katika mechi dhidi ya Ashanti, nafasi zao zikachukuliwa na Farid na Kamwaga.

Akizungumza na Burudani baada ya mechi hiyo, Kamwaga alisema amejisikia furaha kuifungia Azam bao hilo muhimu kwa vile ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza katika ligi na dhidi ya timu kongwe na maarufu.

Alisema siri ya mafanikio yake katika soka ni kufanya mazoezi kwa bidii na kufuata vyema mafunzo ya makocha wake, akiwepo Hall na wale wa kikosi cha pili.

"Hakuna njia ya mkato katika kupata mafanikio zaidi ya  kufanya mazoezi ya nguvu na  kwa bidii,"alisema kinda huyo, ambaye anaamini kuwa, iwapo Stewart ataendelea kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza, ataweza kuonyesha maajabu.

Alisema kitendo cha kuifungia Azam bao la tatu na la ushindi dhidi ya Yanga kilikuwa cha fahari kubwa kwake kwa vile kimeweza kutangaza jina lake na kumfanya ajulikane na mashabiki.

Kamwaga amewashukuru wachezaji wenzake wa Azam kwa kumpa ushirikiano mkubwa tangu alipopandishwa kikosi cha kwanza na kuongeza kuwa, ndoto yake kubwa ni kuipa mafanikio zaidi timu hiyo.

Aliyataja malengo aliyojiwekea kuwa ni pamoja na kuifungia bao Azam katika kila mechi atakayopangwa na pia kuwatengenezea wachezaji wenzake nafasi za kufunga mabao.

Kinda huyo alisema kikosi cha Azam kilishindwa kufanya vizuri katika mechi za mwanzo za ligi hiyo kutokana na baadhi ya wachezaji muhimu kuwa majeruhi na chipukizi waliopandishwa daraja kutokuwa na uzoefu wa ligi hiyo.

Alisema ana hakika iwapo yeye na chipukizi wenzake watauzoea mfumo wa Kocha Stewart, kikosi hicho kitafanya vizuri zaidi katika mechi zijazo na kutimiza malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa msimu huu.

"Unajua wanapoongezeka wachezaji wapya kwenye timu, lazima kunakuwa na mabadiliko kidogo, na hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Azam. Bado tunajifunza kutoka kwa wenzetu wazoefu kwenye kikosi cha kwanza,"alisema.

Kinda huyo amekiri kuwa, kucheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mbele ya umati mkubwa wa mashabiki kunataka moyo na uzoefu, vinginevyo kelele za mashabiki zinaweza kumwathiri mchezaji.

Kamwaga amesema anaridhishwa na mafunzo, ambayo yamekuwa yakitolewa na Stewart kwa vile ni kocha mwenye ujuzi na uzoefu na amemuomba awe akiwapatia nafasi ya kucheza kwenye ligi mara kwa mara ili kuwaongezea uzoefu.

Hata hivyo, Kamwaga amekiri kwamba anakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata namba kwenye kikosi hicho kutokana na kuwepo kwa wachezaji wazoefu kama vile John Bocco na Kipre Tchetche.

Kamwaga alisema anatamani kuvaa jezi za timu ya Taifa, Taifa Stars na kuongeza kuwa, iwapo atapata nafasi ya kuichezea Azam mara kwa mara, anaamini ipo siku ndoto yake hiyo itatimia.

No comments:

Post a Comment