KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 13, 2013

MSHINDI MISS TANZANIA 2013 KUPATA GARI NA MILIONI NANE







MSHINDI wa taji la Redd’s Miss Tanzania mwaka huu anatarajiwa kuondoka na gari dogo lenye thamani ya Sh milioni 15, huku akipewa kitita taslimu cha fedha cha Sh milioni 8.
Shindano hilo linatarajiwa kufanyika Septemba 21, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, huku kukiwa na burudani za kila aina kutoka kwa wasanii maarufu wa ndani pamoja na mwingine kutoka nje.

Akitangaza zawadi hizo jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria Kimaro alisema, wameamua kutangaza mapema zawadi hizo, ili kuleta morali kwa washiriki wote wa shindano hilo.

“Tunaamini shindano la mwaka huu litakuwa na ushindani mkubwa zaidi na zawadi hizi zitakidhi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya warembo,” alisema Victoria. Shindano hilo litashirikisha warembo 30 kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Meneja wa kinywahji cha Redd’s Original Victoria Kimaro akitangaza zawadi za washindi wa shindano la Redd’s Miss Tz jijini Dar Es Salaam kwa waandishi wa habari,Katikati ni Hashim Lundenga na Bosco majaliwa wa kamati ya Miss Tanzania

Mbali na mshindi kutwaa zawadi hizo, mshindi wa pili atapata Sh milioni 6.2, mshindi wa tatu Sh milioni , mshindi wa nne Sh milioni 3, mshindi wa tano Sh milioni 2, mshindi wa sita hadi 15 atapata Sh milioni 1.2 na waliobaki watapata Sh 700,000 kila mmoja.

“Thamani ya fedha taslimu itakuwa ni kiasi cha Sh milioni 46.1 na zawadi zote hizi watakabidhiwa warembo wa Redd’s Miss Tanzania siku inayofuata baada ya kufanyika kwa fainali hizo,” alisema Victoria.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga ambao ndio waandaaji aliwashukuru wadhamini na kusema wamefanya kazi kubwa zaidi katika kuyakuza mashindano hayo.

“Kwa mara nyingine tena tunapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wadhamini wetu wakuu Redd’s Original na wadhamini wenza ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa zuri zaidi,” alisema Lundenga.

Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred aliyelitwaa taji hilo mwaka jana na kukabidhiwa gari aina ya Noah pamoja na kitita cha Sh milioni 8.

Nafasi ya pili katika shindano hilo alikuwa Eugene Fabian kutoka Kanda ya Ziwa, Edda Sylvester aliyekuwa Miss Temeke akishika nafasi ya tatu, ya nne ikienda kwa mrembo kutoka Kinondoni, Magdalena Roy na nafasi ya tano ikienda Happyness Daniel kutoka Kanda ya Ziwa.

Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original, huku wadhamini wenza wakiwa Zanzi, Giraffe Hotel, Star TV, Nipashe, Uchumi Supermarket, Marie Stopes na Clouds FM

No comments:

Post a Comment