'
Sunday, September 15, 2013
YANGA WATAKA MECHI YAO NA MBEYA CITY IRUDIWE
Wachezaji wa Yanga wakiwa wamemzonga mwamuzi Andrew Shamba baada ya kukataa bao lao
HABARI, PICHA KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam, imekata rufani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitaka mchezo wake wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City ulioisha kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Sokoine mjini hapa urudiwe katika Uwanja usiofungamana na timu yoyote baina yao.
Pamoja na hayo, Yanga SC pia imeomba mchezo wake mwingine dhidi ya Prisons Jumatano, uchezwe katika Uwanja mwingine badala ya Sokoine.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Yanga, Mkenya Patrick Naggi amewaambia Waandishi wa Habari leo katika Mkutano uliofanyika hoteli ya Paradise mjini kwamba, pamoja na Rufaa hiyo walicheza mechi ya jana chini ya kinga (Under Protest).
Mjumbe wa Sekretarieti ya Yanga SC, Patrick Naggo akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya Paradise leo. Kulia Ofisa Habari wa klabu, Baraka Kizuguto.
“Baada ya vurugu tulizofanyiwa jana wakati tunaingia uwanjani, tuliwasiliana na marefa na Kamisaa tukawapa taarifa ya kucheza chini ya kinga na taratibu zote zilifanyika. Baada ya mechi kumalizika na kuendelea kufanyiwa vurugu, tukakata Rufaa,”alisema Naggi.
Naggi ambaye pia ni Kamisaa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) alisema wana ushahidi na vielelezo vya kutosha juu ya vurugu walizofanyiwa jana tangu kabla ya mchezo, ikiwemo kushambuliwa kwa mawe wakati wanaingia.
Alisema basi lao lilivunjwa kioo na mashabiki uwanjani na dereva wake kujeruhiwa, hali ambayo iliwatia wasiwasi wachezaji na kucheza kwa woga jambo ambalo lilifanya wacheze ovyo na kulazimishwa sare.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto alisema kwamba mapema baada ya kufika Mbeya walijaribu kuwasiliana na uongozi wa Chama cha Soka Mbeya (MREFA) kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo usalama wao, lakini walikuwa wakipigwa chenga.
Kizuguto alisema kwamba kwa ujumla baada ya yaliyotokea jana, wameingiwa hofu kubwa kuelekea mchezo wa Jumatano dhidi ya Prisons mjini hapa, hivyo nao pia wameomba uchezwe kwenye Uwanja mwingine.
“Kwa hali hii kwa kweli tuna wasiwasi sana na tunaona hapa si salama tena kwetu, hivyo tunaomba na mchezo huo uchezwe Uwanja mwingine kwa usalama wetu,”alisema.
Kizuguto pia alimlalamikia refa wa mchezo wa jana Andrew Shamba wa Pwani kwa kukataa bao lao halali lililofungwa na Didier Kavumbangu na kwamba na hilo pia limo kwenye rufaa yao
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment