'
Wednesday, September 4, 2013
MKENYA AZUA BALAA YANGA
HALI si shwari ndani ya klabu ya Yanga baada ya Baraza la Wazee kutangaza kumtimua Katibu Mkuu mpya aliyeajiriwa kutoka Kenya.
Baraza hilo la wazee lilifikia uamuzi huo jana katika kikao chake kilichofanyika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Mkenya huyo, Patrick Naggi aliripoti makao makuu ya klabu hiyo juzi na kujitambulisha kuwa, ameajiriwa na Yanga katika nafasi ya katibu mkuu.
Hata hivyo, Naggi hakuwa tayari kumtaja kiongozi aliyemwajiri kwa vile ajira za viongozi hutolewa na kamati ya utendaji, ambayo haijawahi kukutana katika siku za hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali alisema hawana taarifa ya kuondolewa kwa Kaimu Katibu Mkuu wa sasa, Lawrence Mwalusako.
Akilimali alisema kiutaratibu, iwapo yanafanyika mabadiliko ya uongozi ndani ya Yanga, lazima kamati ya utendaji ikutane na kutoa uamuzi.
Katibu huyo wa wazee wa Yanga alisema, baraza lake pamoja na viongozi wa matawi pia wanapaswa kujulishwa kuhusu jambo hilo, kitu ambacho hakikufanyika.
"Tulichogundua au tunachohisi ni kwamba huyu mkenya anayeitwa Patrick Naggi ni tapeli na tumemtaka aondoke kwenye klabu yetu kwa sababu hatumtaki,"alisema Akilimali.
Akisimulia ujio wa Mkenya huyo, Akilimali alisema alifika klabuni Jumanne iliyopita na kujitambulisha kwamba, yeye ni katibu mkuu mpya wa Yanga.
"Tulimuuliza nani aliyempa kazi hiyo, akashindwa kumtaja, tukaamua kumtimua ili aende kwa mtu aliyemleta nchini ampe nauli arudi kwao Kenya,"alisema.
"Sisi tunaendelea kumtambua Mwalusako kuwa ndiye kaimu katibu mkuu wa Yanga, hayo mabadiliko hayapo kwa sababu taratibu hazikufuatwa. Kunapokuwa na nafasi ya kazi, lazima tangazo litolewe kupitia kwenye vyombo vya habari na kamati ya utendaji ndiyo inayomuidhinisha,"aliongeza.
Akilimali alisema baraza lake linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kiongozi aliyetaka kumwajiri Mkenya huyo kinyume cha taratibu kwa ajili ya kumchukulia hatua za kinidhamu.
Baadhi ya wanachama wa Yanga waliozungumza na Burudani juzi na jana makao makuu ya klabu hiyo walisema, wanahisi Mkenya huyo ameajiriwa na Mwenyekiti wao, Yusuf Manji.
Hata hivyo, Manji hakuweza kupatikana jana kwa vile yuko nje ya nchi kikazi. Makamu wake, Clement Sanga naye hakuweza kupatikana.
Kwa upande wake, Mwalusako alisema hatambui kuajiriwa kwa mtu mwingine kushika wadhifa wake kwa sababu hakupewa taarifa yoyote na viongozi wake.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti jana kuwa, klabu ya Yanga imeamua kufanya mabadiliko katika sekretarieti yake kwa kumwondoa Mwalusako na kumwajiri Naggi.
Naggi aliwahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na Ofisa Mtendaji wa klabu ya Tusker.
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, Naggi aliwahi kufukwa kazi KFK kutokana na upotevu wa mipira 100.
Hata hivyo, Mkenya huyo aliwahi kulalamika kwamba mipira hiyo iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) haikuwa katika kiwango kinachostahili. Pia aliwahi kulalamika kwamba hakupewa nafasi ya kujieleza kutokana na kilichotokea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment