KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 25, 2013

LIGI KUU BARA HAITABIRIKI



 

UNAWEZA kuiita kuwa ni ligi isiyotabirika. Ni kutokana na matokeo ya mechi 35 zilizochezwa hadi sasa, zikiwemo zilizowahusisha mabingwa watetezi Yanga na watani wao wa jadi.

Yanga ilianza ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuibugiza Ashanti mabao 5-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ni ushindi uliopokelewa kwa furaha na mashabiki wa klabu hiyo kongwe, waliokuwa na imani kubwa kwamba, wangeendeleza wimbi la ushindi kwa kila timu, ambayo wangekutana nayo.

Lakini mambo yaligeuka katika mechi ya pili baada ya mabingwa hao watetezi kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union mjini Dar es Salaam, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City mjini Mbeya na kulazimishwa tena sare hiyo ya mabao na Prisons mjini humo.

Hali ilikuwa mbaya kwa Yanga katika mechi yake ya tano iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuchapwa mabao
3-2 na Azam. Ni kipigo kilichopokelewa kwa huzuni kubwa na mashabiki wa klabu hiyo.

Kwa upande wa Simba, ilianza ligi hiyo vibaya baada ya kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers mjini Tabora, ikaichapa JKT Oljoro bao 1-0 mjini Arusha, ikaicharaza Mtibwa Sugar mabao 2-0 mjini Dar es Salaam kabla ya kuibugiza Mgambo JKT mabao 6-0.

Kasi ya Simba ilipunguzwa na vijana wa Mbeya City baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 baada ya wakongwe hao kuwa mbele kwa mabao 2-0. Ni moja ya mechi zilizokuwa na msisimko wa aina yake kutokana na timu zote mbili kuonyesha kiwango cha juu cha soka.

Timu zilizoanza ligi hiyo kwa kishindo ni maafande wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting, ambazo zinashika nafasi ya pili na ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, inayozishirikisha timu 14.
JKT Ruvu ilianza ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuwachapa ndugu zao wa Mgambo JKT mabao 2-0 mjini Tanga, ikaitandika Prisons mabao 3-0 mkoani Pwani na kuilaza Ashanti bao 1-0.

Mambo yaligeuka kwa JKT Ruvu katika mechi yake ya raundi ya nne baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa ndugu zao wa Ruvu Shooting kabla ya kupigwa mweleka mwingine wa idadi hiyo ya bao na JKT Oljoro.

Coastal Union nayo ilianza ligi hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Oljoro, ikatoka sare ya bao 1-1 na Yanga, ikatoka suluhu na Prisons, ikatoka sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers kabla ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.

Azam nayo ilianza ligi hiyo kwa kusuasua baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, ikaichapa Rhino Rangers mabao 2-0, ikatoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar, ikalazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Ashanti kabla ya kuzinduka na kuichapa Yanga mabao 3-2.

Mbeya City ndiyo timu pekee iliyoonyesha maajabu hadi sasa baada ya kulazimisha sare dhidi ya vigogo vya ligi hiyo, Yanga, Simba na Mtibwa Sugar. Ilitoka sare ya bao 1-1 na Yanga mjini Mbeya, ilitoka suluhu na Mtibwa mjini Morogoro na pia ilitoka sare ya mabao 2-2 na Simba mjini Dar es Salaam. Pia ilitoka suluhu na Kagera Sugar mjini Mbeya kabla ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1.

Mbali na kulazimisha sare, timu hiyo inayoundwa na wachezaji wengi chipukizi, imeonyesha kiwango cha juu cha soka na kuwa kivutio kwa mashabiki walioishuhudia ikicheza dhidi ya Simba na Yanga.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo, Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na JKT Ruvu, Azam, Ruvu Shooting na Coastal Union zenye pointi tisa kila moja.

Kagera Sugar inashika nafasi ya sita kwa kuwa na pointi nane, ikifuatiwa na Mbeya City yenye pointi saba, Yanga na Mtibwa zenye pointi sita kila moja, Rhino Rangera, JKT Oljoro na Mgambo JKT zenye pointi nne kila moja, Prisons yenye pointi tatu na Ashanti yenye pointi moja.

                                                        Tambwe anatisha
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Hamisi Tambwe amedhihirisha kwamba ni moto wa kuotea mbali kwa ufungaji wa mabao baada ya kupachika wavuni mabao sita hadi sasa.

Tambwe, aliyesajiliwa na Simba msimu huu, akitokea Vital'O ya Burundi, aliifungia Simba mabao manne kati ya sita, ilipoinyuka Mgambo JKT mabao 6-0 kabla ya kuongeza mengine mawili wakati Simba ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Mbeya City.

Jerry Tegete, Didier Kavumbagu wa Yanga na Haruna Chanongo wa Simba wanashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao matatu kila mmoja, wakifuatiwa na wachezaji  sita waliofunga mabao mawili kila mmoja.

Wachezaji waliofunga mabao mawili kila mmoja ni Jonas Mkude wa Simba, Elias Maguri wa Ruvu Shooting, Bakari Kondo wa JKT Ruvu, Paul Nonga wa Mbeya City, Saad KIpanga wa Rhino Rangers, Felix Themi wa Kagera Sugar na Kipre Tchetche wa Azam.

Mbali na kuongoza ligi, Simba pia inaongoza kwa ufungaji mabao baada ya kupachika wavuni mabao 13 katika mechi tano, ikifuatiwa na Yanga iliyofunga mabao 10 na Azam iliyofunga mabao manane.

Ashanti ndiyo pekee iliyofungwa mabao mengi hadi sasa, baada ya kuruhusu nyavu zake kutikisika mara 11, ikifuatiwa na Mgambo JKT iliyofungwa mabao 10 na Rhino Rangers na Yanga zilizofungwa mabao saba kila moja.
                                                    Mitazamo ya makocha
Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall amesema walianza ligi hiyo kwa kusuasua kutokana na baadhi ya wachezaji kushindwa kucheza kwa kujituma katika mechi za mwanzo.

Hall, ambaye ni rais wa Uingereza, aliwataja wachezaji walioonyesha kiwango cha chini hadi sasa kuwa ni Salum Abubakar 'Sure Boy' na Khamis Mcha 'Viali', ambao aliamua kuwaweka benchi katika mechi dhidi ya Yanga.

Kocha huyo alilazimika kuwatumia kwa mara ya kwanza wachezaji chipukizi, Joseph Kimwaga na Farid Mussa katika mechi dhidi ya Yanga na walioonyesha kiwango cha juu na hatimaye kuisaidia Azam kupata ushindi.

Kimwaga ndiye aliyeifungia Azam bao la tatu dakika za majeruhi baada ya kutanguliziwa mpira mrefu na kipa Aishi Manula na kuwazidi mbio mabeki wa Yanga kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

Farid na Kimwaga waliingizwa kwenye programu ya mchezo huo kwa shinikizo la wakurugenzi wa timu hiyo, ambao wanaheshimu uwezo wao, uliowawezesha kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza.
 
"Wachezaji kama Salum Abubakar, Mcha Khamis na Kipre Tchetche walicheza vizuri msimu uliopita, lakini kiwango chao kimeshuka msimu huu, hawajitumi, nadhani wanajiona wana nafasi kubwa kwenye kikosi cha kwanza,"alisema Hall.

Hall alisema mchezo wa soka unahitaji mazoezi na mchezaji kujituma na kwamba hayuko tayari kuwavumilia wachezaji wazembe. Alisema hiyo ndiyo sababu iliyomfanya awaweke pembeni wachezaji hao na kuanza kuwatumia chipukizi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amekiri kuwa, ligi ya msimu huu inazo changamoto nyingi na imekuwa ikimpa wakati mgumu kutokana na kupata matokeo wasiyoyatarajia.

Brandts, ambaye ni raia wa Uholanzi alisema, ushindani umekuwa mkali zaidi msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita, ndio sababu timu yake imambulia pointi sita katika mechi tano ilizocheza hadi sasa.

Akitoa mfano, alisema katika mechi kati yao na Azam, vijana wake walicheza vizuri, lakini walishindwa kutumia vyema nafasi walizopata kufunga mabao.

Hata hivyo, kocha huyo ameahidi kupambana kufa na kupona kuhakikisha timu yake inafanya vizuri katika mechi zinazofuata

Kocha Mkuu wa Simba, Abdalla Kibadeni anasema kuumia kwa wachezaji wawili, Nassoro Masoud 'Cholo' na Henry Joseph kulichangia kuifanya timu hiyo ishindwe kupata ushindi katika mechi yao dhidi ya Mbeya City.

Kibadeni alisema, iwapo kikosi kilichocheza na Mbeya City kingekuwa kilekile kilichoibamiza Mgambo JKT mabao 6-0, wangeweza kutoka uwanjani na ushindi dhidi ya vijana hao wa Mbeya.

Kocha huyo alikiri pia kuwa, bado wachezaji wake wanakabiliwa na tatizo na kuchoka haraka kipindi cha pili na kuongeza kuwa, ataendelea kulifanyia kazi kwa kuwapa mazoezi na kuongeza stamina na pumzi.

Kocha Juma Mwambusi wa Mbeya City anasema, vijana wake waliweza kuzidhibiti vyema Simba na Yanga kwa vile anazijua vyema mbinu zinazotumiwa na wapinzani wao uwanjani.

Akitoa mfano, alisema wachezaji wa Yanga walicheza kwa woga na kutumia zaidi pasi ndefu walipocheza nayo mjini Mbeya na kwamba kisingizio cha ubovu wa uwanja hakikuwa na maana.
Mwambusi alisema Simba ni timu nzuri, lakini waliweza kuibana kwa kupeleka mashambulizi yao pembeni ya uwanja ili kuwazuia mabeki wa timu hiyo wasipande mbele kusaidia mashambulizi.

Aliitaja mbinu nyingine waliyotumia kuwa ni kuongeza ulinzi, kuziba njia kwa kuboresha winga zake. Anasema hiyo ndiyo sababu iliyowawezesha kusawazisha mabao yote waliyofungwa na Simba.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena keshokutwa wakati Yanga itakapomenyana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Rhino Rangers na Kagera Sugar, Mbeya City na Coastal Union, Mgambo JKT na JKT Oljoro.

Jumapili Ashanti itacheza na Mtibwa Sugar, JKT Ruvu na Simba wakati Prisons itamenyana na Azam.

RATIBA YA MECHI ZIJAZO
Sept 28, 2013
Yanga na Ruvu Shooting
Rhino Rangers na Kagera Sugar
Mbeya City na Coastal Union
Mgambo JKT na JKT Oljoro
Sept 29, 2013
Ashanti na Mtibwa Sugar
 JKT Ruvu na Simba
 Prisons na Azam

Msimamo wa ligi hiyo hadi sasa ni kama ifuatavyo:
  P W D L GF GA PTS
1  Simba SC  5  3  2  0  13  4  11
2  JKT Ruvu  5  3  0  2  6  2  9
3  Azam   5  2  3  0  8  5  9
4  Ruvu Shooting  5  3  0  2  6  3  9
5  Coastal Union  5  2  3  0  5  2  9
6  Kagera Sugar  5  2  2  1  6  3  8
7  Mbeya City  5  1  4  0  5  4  7
8  Young Africans  5  1  3  1  10  7  6
9  Mtibwa Sugar  5  1  3  1  3  4  6
10  Rhino Rangers  5  0  4  1  5  7  4
11  JKT Oljoro  5  1  1  3  3  6  4
12  Mgambo JKT  5  1  1  3  2  10  4
13  Prisons  5  0  3  2  2  8  3
14  Ashanti United  5  0  1  4  2  11  1


No comments:

Post a Comment