KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 22, 2013

YANGA PWAA, YAPIGWA 3-2 NA AZAM


Wachezaji wa Azam wakimpongeza mfungaji wao wa bao la tatu katika mechi dhidi ya Yanga leo. Picha kwa hisai ya Bin Zubeiry

MWANZONI ilionekana kama vile hadithi ingekuwa ni ile ya kutangulia si kufika. Ni baada ya Yanga kufunga bao la kusawazisha na hatimaye kuongeza la pili.

Lakini mambo yalibadilika dakika chache baadaye baada ya Azam kufunga bao la kusawazisha na kuongeza la tatu dakika moja kabla ya mchezo kumalizika.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga na kuzima shangwe na nderemo zilizokuwa zikisikika kutoka kwa wapinzani wao.

Mshambuliaji chipukizi, Joseph Kimwaga ndiye aliyeibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia bao la tatu baada ya kutanguliziwa mpira mrefu uliopigwa na kipa Aishi Manula na kuwazidi mbio mabeki wa Yanga kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 34 lililofungwa na mshambuliaji John Bocco baada ya kuuwahi mpira wa uliokolewa na beki Kevin Yondani wa Yanga. Timu hizo zilikwenda mapumziko Azam ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Yanga ilisawazisha dakika ya 48 kwa bao lililofungwa na Didier Kavumbagu aliyeuwahi mpira mrefu, akamkodolea macho kipa Manula kabla ya kuupachika mpira wavuni.

Bao hilo liliiongezea nguvu Yanga, iliyofanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Hamisi Kiiza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Simon Msuva.

Kibao kiliwageukia Yanga dakika ya 69 baada ya beki Yondani kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga na Kipre Tchetche kuukwamisha mpira wavuni kwa njia ya penalti.

Wakati mashabiki wakiamini pambano hilo lingemalizika kwa sare, ndipo Kamwaga alipoifungia Azam bao la tatu. Kwa matokeo hayo, Azam sasa inazo pointi tisa baada ya kucheza mechi tano wakati Yanga inazo pointi sita.

Yanga SCAlly Mustafa ‘Barthe z’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.

Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo/Said Mourad, Himid Mao, Farid Mussa/Joseph Kimwaga, Kipre Balou, John Bocco, Humphrey Mieno na Brian Umony/Kipre Tchetche.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezws leo, JKT Ruvu ilifungwa 1-0 na JKT Oljoro Uwanja wa Azam Complex. Bao pekee Oljoro lilifungwa na Paul Malipesa dakika ya 79.

Ruvu Shooting ilishindwa kukwea kileleni baada ya kuchapwa bao 1-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Bao pekee la Coastal Union lilifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 82.

No comments:

Post a Comment