KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 4, 2013

ASHANTI YATOA ONYO KWA AZAM



KOCHA Mkuu wa Ashant United, Hassan Banyai ameionya Azam isitarajie mteremko katika mechi kati yao ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa Septemba 18 mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Akizungumza na Burudani mjini hapa wiki hii, Banyai alisema hawatarajii kurudia makosa waliyoyafanya katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Yanga na Mgambo JKT.

Banyai alisema vipigo walivyopata kutoka kwa Yanga na Mgambo JKT vimewapa funzo kubwa, hivyo hawatarajii kurudia makosa.

"Tumeshapoteza mechi mbili na katika ligi hili si jambo zuri, tutacheza na Azam tukiwa na dhamira ya ushindi,"alisema kocha huyo.

Ashanti ilianza vibaya ligi hiyo baada ya kubugizwa mabao 5-1 na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kuchapwa bao 1-0 na Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Banyai alisema katika mechi hizo mbili, safu yake ya ulinzi ilikosa umakini na amekuwa akilifanyia kazi tatizo hilo ili kuhakikisha makosa hayo hayajitokezi tena.

"Mechi yetu dhidi ya Mgambo ilikuwa nzuri na tulistahili ushindi, lakini uzembe wa mabeki ulitugharimu na wenzetu walitumia nafasi waliyopata kutufunga,"alisema.

Kocha huyo alisema anatarajia mshambuliaji wao mpya, Saidi Maulid atacheza mechi za hivi karibuni baada ya kupatiwa hati ya uhamisho wa kimataifa kutoka Angola, alikokuwa akicheza soka ya kulipwa.

Kabla ya kuvaana na Azam, Ashanti inatarajiwa kumenyana na JKT Ruvu. Mechi hiyo itapigwa Septemba 14 mwaka huu kwenye  Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment