KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 25, 2013

HAPPINESS: NILIJUA NITASHINDA



MREMBO wa Tanzania wa 2013, Happiness Watimanywa amesema alikuwa na uhakika mkubwa wa kushinda taji hilo kutokana na maandalizi aliyoyafanya na pia kujiamini.

Happiness amesema tangu alipofuzu kuingia fainali ya shindano hilo, alikuwa amejiwekea malengo ya kuingia hatua ya tano bora na tatu bora.

"Nilitarajia kushinda kwa sababu nilijiamini, lakini kuna washiriki wachache tuliokuwa tunachuana kwa sababu tulikuwa na sifa zinazolingana," alisema mrembo huyo alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita.

Happiness alishiriki katika fainali za mwaka huu za shindano hilo akiwa mshindi wa mkoa wa Dodoma na Kanda ya Kati. Pia alishinda taji la mrembo mwenye mvuto katika hatua ya awali ya shindano la taifa.

Ushindi huo ulimwezesha Happiness kuzawadiwa gari lenye thamani ya sh. milioni 15 pamoja na fedha taslim sh. milioni nane. Shindano hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Mrembo huyo alisema anaamini majaji walitenda haki kwa kumchagua kuwa mshindi kwa vile anazo sifa zote za kumwezesha kuipeperusha vyema bendera ya taifa katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia.

"Sijahonga ili nipate ushindi, majaji walitenda haki," alisisitiza huku akiangua kicheko. Happiness alishinda taji hilo baada ya kuwabwaga washiriki wenzake 29 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Mrembo huyo alisema hakuwa akifahamiana na majaji wa shindano hilo kwa vile walitambulishwa kwao wiki moja kabla ya shindano.

"Wapo tuliokuwa tukiwafahamu, lakini wengine hatukuwajua kabisa. Wapo waliokuja kutuona tulipokuwa kambini na kutupa mafunzo juu ya mambo mbalimbali,"alisema mrembo huyo mwenye jisimu lenye mvuto.

Miongoni mwa majaji wa shindano la mwaka huu walikuwa warembo wa Tanzania miaka ya nyuma. Warembo hao ni Faraja Kotta, Nancy Sumari na Jacqueline Ntuyabaliwe.

Kwa mujibu wa Happiness, wazazi na ndugu zake waliupokea ushindi wake kwa furaha kubwa kwa vile mara baada ya kutangazwa mshindi wa taji hilo, walirukaruka kwa furaha ukumbini.

Happiness alisema fani ya urembo si ya kihuni kama watu wengi wanavyofikiria na kwamba uhuni ni tabia ya mtu.

"Iwapo wewe mwenyewe utajitambua na wazazi wako wakikuelewa, watakuruhusu kushiriki mashindano haya. Kama huna tabia ya kihuni, huwezi kufanya vitendo vya kihuni,"alisema.

Alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia watoto wao wa kike kushiriki kwenye mashindano hayo kutokana na tabia na mwenendo wao kuwa mbaya katika jamii.

Happiness alisema anatambua wazi kwamba, jukumu alilonalo kwa sasa ni gumu, lakini atajitahidi kushirikiana na wadhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na waandaaji, Kampuni ya Lino Agency International kulitimiza.

"Zipo kazi nyingi za kufanya za kijamii mbele yangu, kuna programu binafsi za Miss Tanzania na wadhamini, nitahakikisha zote nazifanya kadri ya uwezo wangu,"alisema.

Mrembo huyo alisema pia kuwa, atashirikiana vyema na kamati na wadhamini kuhakikisha anajiandaa vyema kwa shindano la dunia, litakalofanyika Septemba mwakani nchini Uingereza.

No comments:

Post a Comment