KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 15, 2013

SNURA KWA MINENGUO, WE ACHA TU


NA STEPHEN BALIGEYA
NI msichana mwenye kiuno cha nyigu, ambacho mkato wake unaonyesha namna, ambavyo kazi ya ziada ilifanywa na Manani katika kukiumba kiumbe hiki jalili.
Mwendo wake ni wa madaha, mithili ya Twiga katika Mbuga ya Taifa ya Serengeti. Tofauti ya miondoko yao ni kwamba, mmoja ni kiumbe cha mwituni na mwingine ni kiumbe katika makazi  rasmi ya binadamu.
Anavutia, anatia hamasa kumtazama hasa akiwa jukwaani, haoni ajizi kukitumia kiuno chake cha nyigu alichopewa kwa ustadi na Manani. Kweli ana haki ya kumvutia kila kiumbe jahiri.
Huyu si mwingine bali ni msanii wa nyimbo za kikazi kipya, Snura Mushi, kwa sasa ni maarufu kwa jina la ‘Mama wa Majanga’, ambaye anazidi kutisha katika sanaa ya muziki nchini.
Snura, ambaye historia yake ya muziki ilianzia katika kucheza ngoma za asili, kisha uigizaji, anatoa somo kwa vijana kwamba hutakiwi kukata tamaa wakati wa kutafuta na siku zote mvumilivu hula mbivu.
Snura anasema ana matumaini atafika mbali kimuziki ili aiwakilishe nchi yake katika nyanja za kimatifa.
”Sitaki mchezo kwenye muziki kwa sasa maana nataka kufika mbali na kufanikiwa zaidi,”anaeleza Snura wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio nchini hivi karibuni.
Snura anasema wimbo wa Majanga una mikasa mingi,  ambayo ni ya kweli, kwani hata yeye amejiimba katika wimbo huo kutokana na watu kugombania mali za marehemu wakati aliyetafuta mwingine.
“Wimbo wa Majanga hata mimi unanigusa, maana bibi yangu alipofariki ndugu walianza kugombania nyumba na nikaamua kuimba,  nyumba ajenge yeye kwanini sisi tugombane, kitu ambacho sio kizuri,”anaeleza Snura.
Vilevile, anasema wimbo wake wa ‘Nimevurugwa’ umetokana na uhalisia wa maisha katika jamii, kwani kuna watu wanafanya mambo ya hovyo na kisha huanza kujutia maisha.
BIFU LAKE NA WEMA LIMEKUWA SUGU
Pamoja na maelezo ya Snura katika muziki, hakusita kuelezea kuwa yeye na Wema Sepetu walikuwa chanda na pete, lakini urafiki wao wa karibu ulipotea bila yeye kufahamu sababu mpaka sasa.
Anaeleza kuwa walikuwa wakishinda pamoja na msanii huyo mwenzake kila sehemu na wakati mwingine watu walidhani kwamba labda wanaishi pamoja ingawa haikuwa hivyo.
“Mimi nadhani kuna mtu alituchonganisha kwa kumpa maneno, ambayo sio sahihi, maana mpaka leo sijui nilimkosea nini na hajaweza kuniambia sababu mpaka leo,”anaeleza.
Snura anasema kuwa urafiki wao uliishia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Juluius Nyerere, Dar es Salaam wakati wakitokea Arusha na waliachana kwa furaha kwa kila mmoja kwenda nyumbani kwake.
“Kilichonishangaza zaidi ni kwamba tuliagana kwa furaha pale uwanjani na kila mmoja akaenda kwake, lakini kesho yake nilipomtumia ujumbe wa salamu, hakujibu na nilipompigia simu hakupokea.
“Jambo hilo lilinishangaza kwani tulisafiri na kurudi salama bila ugomvi, sasa kama kungekuwa na tatizo angenambia kwa kuwa mimi nilikuwa rafiki yake wa karibu sana, lakini mwenzangu hakutaka kusema chochote na kukaa kimya,”anaeleza kwa masikitiko.
Msanii huyo mcheshi na mwenye mvuto awapo jukwaani kutokana na namna anavyokitumia vyema kiuoni chake alichokipachika kwa jina la ‘Majanga’, anasema kuwa mpaka sasa hajakaa vizuri na Wema ingawa yeye ameshasahau yaliyopita.
USHAURI WA SHARO WAMTOA
Snura, ambaye pia aliwahi kujitumbukiza katika muziki wa taarabu, anasema safari yake ya muziki iliwaunganisha na Sharo Milionea (sasa marehemu), wakati huo wakiwa pamoja katika kutafuta maisha.
“Mwenzangu aliwahi kutoka kwa kujikita katika maigizo na kisha  muziki na siku moja alinifuata na kunieleza kuwa, natakiwa kutosahau muziki pamoja na kwamba nilikuwa naigiza.
“Sharo alikuja nyumbani na kunambia, dada unatakiwa kutosahau muziki wetu, jaribu kurudi na kweli niliamua kurudi katika muziki, ambao sasa naanza kuona matunda yake,”anasimulia Snura.
Snura, msanii ambaye hukiita kiuno chake kwamba kimevurugwa kabla ya kukitumia jukwaani kwa jinsi kilivyojichonga mithili ya nyigu, anaeleza kuwa mihangaiko pia iliwahi kumkutanisha na  Masanja wa Original Komedy,  kabla ya kundi hilo kuteka soko la vichekesho nchini.
Anaeleza kuwa alikutana na Masanja na Mac Reagan katika filamu ya ‘Itunyama’, ambayo Snura aliigiza kama mhusika mkuu na kufanya vyema kiasi cha watu wengi kuanza kumtumia kwenye filamu zao.
Vilevile anasema kwa sasa anategemea kufanya muziki wa taarabu na Mzee Yusuph, ili kuongeza wigo wa muziki kwa wadau wake, ambao ni Watanzania wanaomuunga mkono.
Snura anaeleza kuwa hana ‘bifu’ na msanii mwenzake Shilole na kwamba watu wanaozungumzia uhasama wao wanalo jambo mioyoni mwao. Anasema anazungumza vizuri na Shilole, ambaye wanashindana kwa kukata viuno jukwaani.

No comments:

Post a Comment