'
Wednesday, September 4, 2013
RAIS TPBO ASIMULIA KILICHOMSIBU BONDIA WA MAREKANI
RAIS wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdalla 'Ustaadh' amethibitisha kuwa, bondia Phil William wa Marekani hajalipwa pesa anazomdai promota Jay Msangi.
Akizungumza na TBC 1 juzi usiku kupitia kipindi cha Usiku wa Habari, Yassin alisema bondia huyo wa Marekani anamdai Msangi dola 8,200 za Marekani (sh. milioni 14).
Yassin alisema Phil alitakiwa kulipwa pesa hizo kabla ya kupanda ulingoni mwishoni mwa wiki iliyopita, kuzipiga na Francis Cheka wa Tanzania katika pambano la kuwania ubingwa wa dunia wa uzito wa kati linalotambuliwa na WBF.
Rais huyo waTPBO alisema Msangi alishindwa kumlipa Phil pesa hizo kutokana na kampuni moja iliyojitokeza kudhamini pambano hilo, kushindwa kutoa sh. milioni 20 ilizoahidi.
"Hao wadhamini walimwambia Msangi aandae pambano hilo kisha awapelekee gharama alizotumia ili wamrejeshee pesa zake, jambo ambalo halikuwezekana kwa sababu wadhamini ndio waliopaswa kutoa pesa mapema,"alisema Yassin.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, kampuni hiyo pia ndio iliyopaswa kulipa fedha za nauli kwa ajili ya Phil na watu wengine wawili kutoka Marekani pamoja na waamuzi kutoka Afrika Kusini, lakini ilishindwa kufanya hivyo.
"Zizzouf Fashion ndio waliokuja kuokoa jahazi baada ya kulipa pesa za nauli kwa ajili ya Phil na wenzake pamoja na majaji kutoka Afrika Kusini na hadi sasa hawajarejeshewa fedha zao,"alisema.
Kwa mujibu wa Yassin, mabondia wote wa Tanzania waliocheza mapambano ya utangulizi pamoja na Cheka, walilipwa pesa zao kabla ya kupanda ulingoni kutokana na pesa za viingilio.
Alisema Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ndiye aliyetoa agizo hilo baada ya kupata taarifa kwamba mabondia hao walitishia kutocheza mapambano yao iwapo wasingelipwa pesa zao mapema.
"Hali ilikuwa mbaya sana kwa Msangi baada ya kukosa mdhamini kwa sababu hata pesa ya ada ya kupima uzito, zililipwa na mtu mwingine,"alisema Yassin, ambaye chama chake kilishiriki katika kuandaa mapambano hayo.
Yassin alisema busara za Dk. Mukangara ndizo zilizomwezesha Phil kukubali kupanda ulingoni kuzipiga na Cheka kwa ahadi kwamba angelipwa baada ya pambano hilo. Katika pambano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Cheka alimdunda Mmarekani huyo kwa pointi.
Rais huyo wa TPBO alisema Msangi alilazimika kuokolewa na polisi baada ya pambano kati ya Cheka na Phili kumalizika baada ya bondia huyo kutoka Marekani na wenzake kutishia kumpiga.
Alisema mapromota wawili walijitolea kulipa dola 10,000 kwa masharti ya kutaka Msangi aweke rehani magari yake mawili, lakini promota huyo aligoma kwa madai kuwa, hayakuwa ya kwake.
"Walitaka kumpiga Msangi hotelini, lakini aliokolewa na polisi na kuwekwa ndani kwa simu moja,"alisema.
Pamoja na kujitokeza kwa kasoro hizo, Yassin alimpongeza Msangi kwa kuweza kuandaa mapambano hayo kwa vile yameiletea heshima kubwa Tanzania kimataifa na kuzitaka taasisi mbalimbali zijitokeze kumsaidia.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema, linaendelea na upelelezi kuhusu tuhuma zinazomkabili Msangi kabla ya kuamua kulifikisha suala hilo mahakamani.
Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema juzi kuwa, upelelezi bado unaendelea na iwapo Msangi atashindwa kulipa pesa hizo, jalada lake litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali ili aweze kufikishwa mahakamani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment