KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 26, 2013

MANJI ALIPUA BOMU YANGA


MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amewataka wachezaji wa timu hiyo kubadilika na kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizosalia za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Manji alitoa agizo hilo juzi alipokutana na wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi na kula nao chakula cha usiku kwenye hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, Manji aliwaeleza wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwamba hajafurahishwa na mwenendo wa timu hiyo katika ligi kuu hadi sasa.

Kwa mujibu wa habari hizo, Manji aliwaeleza wachezaji hao kwamba, timu ilicheza vizuri katika baadhi ya mechi alizozishuhudia, lakini haelewi kwa nini imekuwa ikikosa ushindi.

Mwenyekiti huyo wa Yanga anadaiwa kuwaeleza wachezaji hao kwamba, anahisi kuna njama zinazofanywa na watu wasioitakia mema timu hiyo ili kuihujumu isifanye vizuri katika ligi.

"Manji aliwaeleza wazi wachezaji na baadhi ya viongozi wa Yanga waliokuwepo kwenye kikao hicho kwamba, anahisi anafanyiwa hujuma na watu wanaompinga na alionya kuwa, iwapo wachezaji hawatabadilika, atajiuzulu,"kilisema chanzo cha habari.

Mwenyekiti huyo aliwaeleza wachezaji na viongozi wenzake kwamba yupo tayari kujiuzulu wakati wowote na kuwaachia nafasi watu wengine ya kuiongoza klabu hiyo kongwe nchini.

Chanzo hicho cha habari kilieleza kuwa, Manji aliamua kupasua bomu kwa kuwaeleza wachezaji kwamba, miongoni mwa watu wanaojaribu kuihujumu Yanga ni wale waliokuwa wamezoea kuchota mapato ya mechi za ligi holela.

"Kuna watu najua tumeziba mianya yao ya ulaji, sasa wanahaha kutaka kuikwamisha Yanga, kama na nyie mnatumika, niambieni nijiuzulu sasa hivi,"chanzo hicho cha habari kilimnukuu Manji.

Yanga inashika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa imeambulia pointi sita katika mechi tano, imefunga mabao 10 na kufungwa mabao saba.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, katika kikao hicho, Manji aliwauliza wachezaji matatizo yanayowafanya washindwe kushinda mechi zao na kuelezwa kuwa, hawajalipwa posho za mechi kadhaa.

Alipoulizwa kuhusu kilichojadiliwa kwenye kikao hicho, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema yalikuwa masuala ya kawaida, yaliyolenga kujua matatizo na kuimarisha timu yao.

“Lengo la mwenyekiti lilikuwa ni kuhakikisha tunajitazama upya na kuangalia wapi tumejikwaa na baada ya hapo tuendelee mbele,"alisema Cannavaro.

Kufuatia maamuzi yaliyofikiwa kwenye kikao hicho, Cannavaro alisema wameamua kutangaza kiama kwa timu zote watakazokutana nazo katika ligi hiyo kuanzia mwisho wa wiki hii.

Alisema wamepanga kuanza kuonyesha kucha zao keshokutwa katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umeamua kuongeza nguvu kwenye safu yake ya uongozi kwa kumrejesha kundini mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo ya mjini Dar es Salaam, Mohamed Msumi.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa, uongozi wa Yanga umefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, Msumi ni mtu muhimu na anakubalika na wanachama wengi kutokana na mchango wake ndani ya klabu.

Msumi aliamua kujiweka kando na masuala ya Yanga kwa kile alichodai kuwa, katiba ya Yanga imekuwa ikikiukwa tangu uongozi wa Manji ulipoingia madarakani mwaka jana.

Viongozi wa matawi ya Yanga wanatarajiwa kukutana kati ya leo na kesho kwa ajili ya kumkabidhi majukumu Msumi ili kuiwezesha timu hiyo kushinda katika mechi zake zilizosalia.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa kumrejesha kundini, Msumi alisema yupo tayari kuendelea kuitumikia Yanga wakati wowote.

No comments:

Post a Comment