KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 25, 2013

LATIFAH ASEMA ATATUMIA PESA ALIZOSHINDA KUJILIPIA ADA, CLARA ATOA YA MOYONI


MSHINDI wa pili wa shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania wa 2013, Latifah Mohamed amesema atatumia fedha za zawadi alizopata kujisomesha masomo ya chuo kikuu.

Latifah, ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita amesema, hapendi kuendelea kuwasumbua wazazi wake kumlipia ada ya chuo kwa sasa.

Binti huyo alishika nafasi hiyo baada ya kujibu vizuri swali aliloulizwa na jaji. Aliulizwa na kujibu swali hilo kwa lugha ya kiingereza.

Latifah ni miongoni mwa warembo waliokuwa wakishangiliwa kwa mayowe mengi na mashabiki kila alipopita jukwaani. Shindano hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

"Nataka wazazi wangu waone nimefanya kitu fulani muhimu katika maisha yangu,"alisema binti huyo, ambaye alizawadiwa pesa taslim sh. milioni 6.2.

Mbali na kutumia pesa hizo kujisomesha, Latifah alisema anatarajia kutumia kiasi kingine kuanzisha biashara. Alisema lengo lake kubwa ni kuwa mfanyabiashara.

"Nitaanzisha biashara yoyote kwa sababu wakati tulipokuwa kambini, tulipewa mafunzo ya jinsi ya kuwa wajasiriamali,"alisema.

Latifah alisema, wakati walipokuwa kambini, alifurahia mafunzo waliyopewa na mshindi wa taji hilo wa mwaka 2004, Faraja Kotta.

"Faraja alituonya, tusitumie urembo kuficha maovu. Alitutaka tujitambue. Kwangu, Faraja na Nancy Sumari ni mfano mzuri wa wanawake,"alisema.

Latifah alisema alifurahi alipotangazwa kuwa mshindi wa pili wa taji hilo kwa vile alikuwa amejiwekea malengo ya kuingia hatua ya tatu bora.

"Kusema kweli sikutarajia kushika nafasi ya pili, lakini namshukuru Mungu kwa sababu ushindani ulikuwa mkali,"alisema.

Latifah alisema alianza kuvutiwa na fani ya urembo tangu akiwa mdogo na alimtaja mrembo wa Tanzania wa 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe kuwa ni kichocheo kwake kushiriki shindano hilo.

"Kuna siku nilimwambia baba yangu mzazi, nataka niwe mrembo, akaniambia subiri kwanza umalize shule na sasa nimetimiza ndoto yangu,"alisema.

Binti huyo alisema amemaliza kidato cha sita mwaka huu na kwamba wazazi wake hawakuwa na kinyongo kwake kushiriki katika mashindano ya urembo.

Alisema alipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wazazi wake tangu alipoanza kushiriki shindano la Miss Kigamboni na kuibuka mshindi na baadaye shindano la Miss Temeke, ambapo pia aliibuka mshindi.

Wakati huo huo, mshindi wa tatu wa shindano la Miss Tanzania 2013, Clara Bayo amewataka wazazi nchini kuwaruhusu watoto wao wa kike kushiriki kwenye mashindano hayo ili waweze kuonyesha vipaji vyao.

Clara amesema fani ya urembo si ya kihuni kama inavyodhaniwa na wengi na kwamba, iwapo itatumika vizuri, inaweza kuleta manufaa makubwa kwa watoto wa kike.

Mrembo huyo alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Usiku wa Habari, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1.

"Zipo fursa nyingi kwa wasichana wanaoshiriki mashindano ya urembo na si vizuri kuzikosa fursa hizi,"alisema binti huyo, ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita.

Clara alisema tangu alipoanza kushiriki kwenye mashindano hayo, kuanzia kitongoji cha Dar City Centre na baadaye Kanda ya Ilala, alikuwa amejiwekea malengo ya kuingia hatua ya tano bora.

"Naweza kusema ilikuwa bahati kwangu kuingia hatua hiyo na tatu bora kwa sababu ushindani ulikuwa mkali,"alisema mrembo huyo.

"Nilifurahi sana kushinda nafasi niliyoipata, namshukuru Mungu,"aliongeza.

Clara alisema mwanzoni alikuwa akiogopa kushiriki kwenye mashindano hayo kutokana na msimamo wa wazazi wake.

"Mwanzoni wazazi hawakutaka kabisa nishiriki mashindano haya, walinishinikiza nisome kwanza. Nimemaliza kidato cha sita hivi karibuni na nilipowaambia nataka kushiriki, waliniunga mkono,"alisema.

Binti huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, fani ya urembo si ya kihuni kwa vile uhuni ni tabia binafsi ya mtu.

Alisema wasichana wanaoshiriki kwenye mashindano hayo wanapaswa kuwa makini kwa vile ni rahisi kufuatiliwa na vyombo vya habari kutokana na umaarufu walioupata.

"Ukiwa na tabia nzuri, huwezi kupata matatizo,"alisema.

Alisema anamshukuru mrembo wa Tanzania wa 2005, Nancy Sumari kwa kumpa mafunzo mazuri alipokuwa kambini, ambapo alimtaka kutofautisha urembo na maisha yake binafsi.

No comments:

Post a Comment