KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 26, 2013

NGASA KUREJEA DIMBANI JUMAMOSI



MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa Yanga anatarajiwa kurejea dimbani keshokutwa wakati timu hiyo itakapomenyana na Ruvu Shooting katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Ngasa alisema uongozi wa Yanga umekubali kumlipia deni la sh. milioni 45 anazodaiwa na klabu ya Simba pamoja na faini.

Ngasa alisema alifikia makubaliano hayo na Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji wakati wa kikao cha faragha kati yao kilichofanyika juzi kwenye hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.

"Namshukuru mwenyekiti wangu kwamba tumeshakubaliana kuhusu suala hilo na pesa hizo zinaweza kupelekwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wakati wowote,"alisema.

Ngasa alifungiwa kucheza mechi sita za ligi na kutakiwa kurejesha sh. milioni 30 alizolipwa na Simba pamoja na faini ya sh. milioni 15. Jumla ya fedha alizotakiwa kulipa ni sh. milioni 45.

Awali, kulikuwepo na taarifa kwamba, Manji alikataa kumlipia Ngasa fedha hizo na kumtaka azilipe mwenyewe. Manji anadaiwa kuweka msimamo huo, alipokutana na Ngasa mjini Mbeya wiki mbili zilizopita.

Lakini baada ya kikao cha juzi, pande hizo mbili zilikubaliana kuhusu taratibu za kulipa fedha hizo ili kumwezesha mchezaji huyo arudi dimbani kuisaidia timu yake.

Ngasa hakuwa tayari kutaja utaratibu huo, lakini habari za uhakika zimeeleza kuwa, amekubali kukatwa sh. 500,000 kila mwezi katika mshahara wake ili kufidia deni hilo. Ngasa analipwa mshahara wa sh. milioni mbili kila mwezi.

Mshambuliaji huyo alimweleza Manji kuwa, ana hamu ya kuanza kuitumikia Yanga baada ya kumaliza adhabu yake ya kutocheza mechi sita aliyopewa na TFF.

Alipoulizwa jana kuhusu makubaliano hayo, Manji alijibu kwa ufupi akisema: "Subirini, akicheza mtamuona."

No comments:

Post a Comment