KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, September 28, 2013

NGASA AKATA MZIZI WA FITINA, AILIPA SIMBA MIL 45/-, KUICHEZEA YANGA LEO


Mrisho Ngasa akikabidhiwa jezi ya Yanga baada ya kurejea rasmi kwenye klabu hiyo msimu huu.


MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa Yanga anatarajiwa kuanza kuonekana rasmi uwanjani leo baada ya kulipa deni la sh. milioni 45 kwa klabu ya Simba.

Ngasa atashuka dimbani leo kuichezea Yanga katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji huyo alifungiwa kucheza mechi sita baada ya kamati ya sharia, katiba na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kubaini kwamba alitia saini mkataba wa kuichezea Simba na kulipwa sh. milioni 30.

Kamati hiyo ilimtaka Ngasa arejeshe fedha hizo pamoja na kulipa fidia ya sh. milioni 15 na mshambuliaji huyo, ametekeleza hilo.

Ngasa aliwasilisha fedha hizo makao makuu ya TFF jana saa tisa alasiri akiwa amefuatana na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto na Mhasibu, Rose Msamila.

Akizungumza baada ya kukabidhi hundi ya fedha hizo, Ngasa alisema hana kinyongo na Simba licha ya kumsainisha mkataba mpya bila kujijua.

Alisema alikubali kutia saini mkataba huo akielewa kwambani wa mkopo, kumbe Simba walimsainisha mkataba mpya wa mwaka mmoja kinyume na makubaliano kati yao.

Ametoa mwito kwa wanasoka wa Tanzania, wasikubali kutia saini mikataba na klabu bila ya kuwashirikisha wanasheria.

Alisema ni vyema kwa mchezaji kutia saini kitu anachokielewa badala ya kulazimishwa ama kushawishiwa kufanya hivyo bila kujua lolo.

Pambano kati ya Yanga na Ruvu Shooting linatarajiwa kuwa gumu kutokana na kila timu kupania kushinda ili kujiweka kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Ruvu Shooting inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tano, sawa na timu za JKT Ruvu, Azam na Coastal Union. Yanga ni ya tisa ikiwa na pointi sita.
Mrisho Ngasa akikabidhiwa jezi namba 16 ya Simba na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu'

No comments:

Post a Comment